Waridi wa BBC- Ninajilaumu kwa kupewa talaka

glady

Chanzo cha picha, Gladys

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Bi Gladys Kagendo , mama ya mtoto mmoja , mnamo Juni mwaka huu alitimu miaka 30 .Ila katika umri huu ambao bila shaka bado yuko kwenye ujana wake , tayari alikuwa amefunga ndoa , kupata ujauzito na kupewa talaka yote haya yakifanyika katika kipindi cha miezi 7 pekee .

Hatahivyo licha ya hali inayomkabili ameamua kujilaumu yeye mwenyewe kwa kuwa alichangia pakubwa sababu zilizoangamiza ndoa yake .

"Nadhani kuwa matukio katika maisha yangu ya ndoa , yamekuwa ni somo kuu kwangu . Sitaki kulaumu mtu yeyote kwa sababu naamini kila mhusika alikuwa na kosa moja au jingine ,kwa kila aliye kwenye ndoa ni muhimu kufahamu ni kipi anachoweza kuvumilia na ni kipi hawezi , tuwache kurushiana lawama za ni huyu alifanya kosa hili na kadhalika "anasema Gladys

Maisha mafupi ya ndoa .

Mwanamke huyu alifunga ndoa mwezi Julai 2017 , katika sherehe ya kukata na shoka iliofanyika katika kaunti ya Embu,katikakati mwa Kenya.

Alipofunga ndoa alikuwa na ujauzito wa miezi minane

Chanzo cha picha, Gladys Kagendo

Maelezo ya picha, Alipofunga ndoa alikuwa na ujauzito wa miezi minane

Gladys anasema kuwa walitumia zaidi ya dola elfu tano kufanikisha sherehe hio ilyowavutia wakaazi wengi wanaoishi katika eneo hilo kutokana na ufahari wake .

La kushangaza ni kwamba hakufahamu hata chembe kwamba kitumbua chake kilikuwa kimeingia mchanga na kwamba sio muda mrefu ndoa yake ingeanza kuyumbayumba.

Kumbuka kwamba wakati alipofunga ndoa alikuwa na ujauzito wa miezi minane ila hakuna aliyefahamu isipokuwa watu wa karibu na wale wa jamii yake .

"Hakuna mtu yeyote ambaye huingia kwenye ndoa na kupanga kuondoka kesho yake , hasa kwa upande wa wanawake , wengi huingia kwa furaha na ari ya kuifanikisha kwa vyovyote vile "Grace anasema .

Kabla ya sherehe ya ndoa , Gladys alikuwa amechumbiana na aliyekuwa mume wake kwa miaka mitano , baada ya kukutana naye mwaka 2013 wakati alipokuwa akijiandaa kujiunga na chuo kikuu.

Maisha ya uchumba anasema yalikuwa mazuri kwani kilikuwa kipindi ambacho walikuwa wameanza kufahamiana, asijue kuwa vituko na malimwengu yalikuwa yanamsubiria kwenye ndoa yake mpya.

Licha ya udhaifu uliokuwa na mpenzi wake, Bi Gladys alipiga moyo konde na kuendelea kuishi naye bila kujali vishawishi ambavyo vingemfanya kuondoka katika uchumba.

Mchumba wake alianza kuwaleta wanawake tofauti tofauti ndani ya nyumba yake.

Chanzo cha picha, Gladys kagendo

Maelezo ya picha, Mchumba wake alianza kuwaleta wanawake tofauti tofauti ndani ya nyumba yake.

Anasimulia kwamba wakati mmoja alitumwa katika eneo lililo mbali na anakoishi na mchumba wake na ni wakati huo ndiposa aligundua udhaifu wa mpenzi wake.

Mchumba wake alianza kuwaleta wanawake tofauti tofauti ndani ya nyumba yake.

"Sio mara moja au mbili nilimfumania na mwanamke ndani ya nyumba yake , na kila wakati alikuwa anasema kuwa hawa ni binamu zake au ni watoto wa ndugu zake , lakini ukweli ni kwamba alikuwa na mipango ya kando "anakumbuka Gladys

Jambo jingine ambalo mwanadada huyu anasema alipitia wakati wa uchumba wake ni kupigwa na mchumba wake alipotaka kujua kuhusu mwenendo wa mchumba wake kuwa na wanawake wengine .

Licha ya yote hayo bi Gladys aliamua kufunga ndoa sababu kuu ikiwa ni ujauzito aliokuwa nao na pili akidhania kwamba mchumba wake angebadilika.

Lakini akiwa mwanamke aliyekuwa akifuata dini sana hakutaka watu wajue kwamba alipata ujauzito nje ya ndoa.

Siku ya ndoa ilipofika kulikuwa na shamra shamra za aina yake, umati wa watu ulijitokeza na yeyote aliyepita katika eneo la sherehe bila shaka alijionea fahari ya harusi hiyo.

Sio magari ya kifahari, mapambo , vyakula na wageni waheshimiwa kila kitu kilikuwa cha kifahari.

Lakini licha ya yote yaliokuwa yakiendelea bi Gladys anasema hakuwa bi harusi aliyefurahia harusi yake kwani bwana harusi alifika katika uwanja wa kanisa akiwa amechelewa na hakuonyesha hisia za kujali.

Mbali na hilo bi harusi anadai kwamba wakati wote walipokuwa wakila kiapo cha ndoa ,alihisi kana kwamba moyo wa mume wake haukuwa umetulia kwenye shughuli ile .

"Nilishangaa mno kumuona mume wangu akiwa kwa simu yake ya mkononi wakati tuko kwenye ibada ya harusi yetu, kama kawaida , bwana harusi huwa hatoi macho kwa maua yake ambayo ni bi harusi , lakini katika sherehe ya ndoa yetu mambo yalikuwa tofauti ni mimi nilikuwa nampa macho ya mahaba ila yeye alionekana kuwa mbali'',Gladys anasema .

Maisha magumu baada ya sherehe ya ndoa

ndoa

Chanzo cha picha, Glady

Sio ajabu kuwa maisha baada ya ndoa yangekuwa na machungu na kero nyingi.

Mwanadada huyu anasema kuwa hakupelekwa fungate angalau hata siku mmoja , jambo ambalo lilimshangaza sana .

Lakini kwa kuwa aliamini kwamba mambo yatabadilika alipiga moyo konde na kuendelea kuishi.

Hatahivyo kadri alivyoendelea kuishi alihisi kana kwamba alikuwa akijilazimisha kuishi katika ndoa hiyo

Baada ya mwezi mmoja ilifika wakati wa kujifungua , alikwenda hospitali ila aliyekuwa mume wake hakuwa na muda wa kumfariji hospitali .

Siku ambayo Gladys alikuwa akijifungua, mchumba wake hakuonekana hospitali, tukio ambalo lilimvunja nguvu dada huyu.

Mwanadada huyo anasema mume wake alipofika hospitalini ,dada yake tayari alikuwa amemaliza mipango yote ya kuwaondoa hospitalini , kwa hivyo hakutekeleza jukumu lolote .

Wakati wa harusi yake

Chanzo cha picha, Gladys Kagendo

Na kwa kuwa alikuwa amejifungua kwa njia ya upasuaji bi Gladys hakuwa nguvu ya kufanya lolote .

Na kipindi chote hicho baba ya mtoto wake hakumsaidia na chochote.

"Kabla ya wiki moja kuisha baada ya kutoka hospitali , aliyekuwa mume wangu alikuwa na desturi ya kusema kila wakati ana shughuli ambazo zinamlazimu awe nje ya nyumba , katika pilka pilka zangu za kumshawishi akae nyumbani ili kunisaidia , alinipiga na kwa bahati mbaya nilimwangukia mtoto wangu mchanga "anakumbuka Gladys

Misukosuko katika ndoa yake iliendelea na Gladys alisahau ni vipi wanawake waliopo kwenye ndoa hutabasamu .

Mwanadada huyu anasema kuwa hakuwa na wa kumfariji katika ndoa hii kwani anadai kuwa mashemeji zake hawakuingilia kati na kuokoa ndoa hiyo iliokuwa inakaribia kuanguka.

Lakini kwanini Gladys hakutoka kwenye ndoa hiyo?

Gladys anasema kuwa kama mwanamke alikuwa ameamua kuwa hatatoka kwenye ndoa yake ,na kwamba alikuwa tayari kuipigania na akiwa na imani kwamba mambo yatabadilika.

Licha ya matumaini ya kuboresha ndoa yake mwanadudu huyo alipata mshangao mkubwa.

Miezi mitano tu baada ya ndoa hiyo , mume wake alifunga virago vyake na kuondoka , na hatua hiyo iliashiria mwisho wa ndoa yao .

Gladys anasema kuwa anajilaumu kwa yote yaliokabili ndoa yake bila kusahau udhaifu wake wa kuwa na hasira .

Hatahivyo anasema kwamba hasira zake zilitokana na mumewe kushindwa kumtosheleza katika tendo la ndoa .

Talanta ya uimbaji

glady

Chanzo cha picha, Glady

Baada ya ndoa yake kugonga mwamba, ilibidi aanze maisha upya .

Mwanadada huyu anasema kuwa amepitia mahangaiko mengi katika kutafuta riziki yake na mwanae . Mojawapo ya njia alizozitumia kuendelea na maisha yake ni kuvumbua kipaji chake cha uimbaji ambacho kwa hivi sasa anakiendeleza .

Cha pili amekuwa ni mtoa nasaha hasa kwa upande wa mabinti na wanawake, wanaokimbilia ujauzito kwa lengo la kufunga ndoa.

Gladys anasema kuwa ni afadhali mzigo wa kumlea mtoto umuangukie mama pekee , kuliko kulazimisha ndoa ambayo itakuwa na athari nzito kwa mfano kuzua magonjwa ya kiakili na msongo wa mawazo .

"Usifuatane na mwanamume kwa sababu yoyote , iwe ni kupata ujauzito , iwe ni fedha au chochote kwani mwisho wa siku , ndoa ya kulazimisha huwa na madhara yake ."asema Gladys .