WARIDI WA BBC: 'Kuvunjika kwa ndoa yangu kumekuwa funzo kubwa kwangu'

Shil Oloo Nyapengo

Chanzo cha picha, Shil Oloo Nyapengo

Shil Oloo Nyapengo kutoka nchini Kenya, ni miongoni mwa wanawake wachache ambao wamepata ujasiri kuzungumzia masaibu ya kuporomoka kwa ndoa yake,hatua ambayo si kawaida kwa wale ambao wametoka kwenye ndoa kwa sababu mbalimbali kujitokeza kuzungumza bayana kuhusiana kilichosababisha kuporomoka kwa ndoa zao.

Ila mwanamke huyu amekiri kwamba kuvunjika kwa ndoa yake, ndiko kumesababisha yeye kujifunza mengi.

Kiwango cha yeye kuandika simulizi la hali hiyo katika kitabu kwa jina Suddenly single, ni kitabu ambacho ameorodhesha hatua kwa hatua kufeli kwa ndoa yake na jinsi machozi , machungu na sonona ya miezi mingi ilikuwa sababu ya yeye kujitambua upya.

Japo kwa mwendo wa kobe, hayo yalisababisha mafunzo makubwa sio tu kwake yeye bali kwa makundi kama wajane, waliopewa talaka au waliotelekezwa katika mahusiano ya kimapenzi.

Ndoa yake ilikuwaje?

Shil aliolewa akiwa na umri wa miaka 17 ,baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari, anakiri kwamba kama kawaida na mahusiano yeyote hakukosi changamoto, ila hakuna siku aliwahi kudhani kwamba ndoa yake ingeporomoka na kuishia kwa talaka.

“Niligeuka na kuwa muathiriwa wa kukataliwa na hatimaye kupewa talaka , mwanaume ambaye nilikuwa nimempenda, kumuamini na kumthamini kwa aliondoka ghafla na kwa usiri mkubwa kutoka kwa ndoa yangu hadi ndoa nyengine mpya”anakumbuka Shil

Wakati huo maisha yalikuwa ni magumu sana kwake mwanadada huyu kwa kiasi kwamba sonona ilianza kuwa sehemu ya maisha yake kilichomuuma zaidi ni kwamba yeye kama muumini wa dini ya kikristo alikuwa ameshika sana Imani ya kwamba Talaka ni dhambi.

Kipindi hicho mwanadada huyu ambaye ni mama wa watoto wawili anasema alikosa utamu wa maisha na ladha ya kuishi ilikuwa haipo tena hakuamini kwamba ndoa yake ya miaka 9 ilikuwa imefika kikomo bila yeye kufahamu ni kwanini.

“Kilichofuata baada ya mume wangu kuondoka kwenye ndoa , nilianza kujihisi kana kwamba sikuwa kamili, kana kwamba nilikuwa sifai na kwamba sikuwa na uzuri wowote , ndiposa mume aliamua kuniacha na kuanza mahusiano mapya ”anakumbuka Shil

Mwanamke huyu anasema kwamba kutokana na kwamba mume wake aliondoka ghafla kutoka makazi yao, aliachwa katika mazingira ambayo jamaa wa karibu yaani mashemeji waliokuwa wanaishi huko walianza kumsimanga na kumkejeli sana , kwa kiasi anadai kwamba walimnyanyasa kwa dhuluma za kichapo mwilini mwake , haya yote anahoji ni kutokana na kwamba walihisi kana kwamba Shil hakustahili kuitwa mke wa ndugu wao .

Shil Oloo Nyapengo

Chanzo cha picha, Shil Oloo Nyapengo

Kwa kipindi ambacho anasema mume wake aliondoka katika ndoa , kila kitu kilikuwa kimepangwa na ni kana kwamba ni yeye tu ambaye hakuwa na ufahamu wa mipango mahususi iliyokuwa imewekwa ya mume wake kufunga ndoa kwa siri na mwanamke mwingine.

Shil anasema kwamba kama mke ambaye alikuwa na hamu ya ndoa alianza harakati za kupigania ndoa yake sio kwa fujo ila kuanza mazungumzo na mama mkwe pamoja na marafiki wao ambao alikuwa anatumai kwamba watawasaidia kusuluhisha ndoa yao.

Ni jambo lililoambulia patupu na Shil alijipata na upweke mkubwa ilipobainika kwamba mume wake alikuwa ameamua kuanza maisha mapya na mwanamke mwingine.

Kama mwanamke aliyekuwa amempenda mume wake sana anasema alijaribu kila awezalo kuokoa ndoa yao ila harakati zake hazikufaulu.

Pigo baada ya ndoa kufeli

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Haikuwa rahisi kwa Shil kusonga mbele na maisha yake , kuna kipindi anakumbuka alijawa na upweke , machungu na machozi ya kila siku , asiweze kufanya lolote ila kulia kwa kuhisi kama aliyekosea kuwa duniani.

Shila anasema katika kitabu chake kwamba mume alipoondoka alimwachia wanae wawili .Kipindi ndoa yake ilipovunjika alikuwa ameajiriwa katika kampuni ya aliyekuwa mume wake , kwa hiyo ilibidi aachishwe kazi , kuishi maisha bila ajira , yakiandamana na pigo la kutupwa kama mke kulipelekea mama huyu kuwa mngonjwa wa moyo .

''Maisha yangu yalibadilika mno, mume wangu alikuwa ni tajiri , na alikuwa amenipatia maisha mazuri, nilikuwa na gari na nilikuwa naishi katika mazingira ya kuenziwa baada ya mwisho wa ndoa maisha yaligeuka sana , na marafiki zangu wengi walinipa kisogo”

Shil anasema kwamba kuvunjika kwa ndoa inakwa na uchungu ambao huwezi elezeka, mama huyu anakumbuka wakati ambao watu walimsema vibaya sana kila alipopita na kumcheka sana kwa kuwa maisha yaligeuka ghafla.Ni siku nyingi ambazo alishindwa kutoka hata chumbani mwake nahata wakati mmoja anakiri kulała kwa kipindi cha wiki nzima bila kula chochote isipokuwa kulia na machungu.

''Nilikuwa na machungu yasiyoelezeka, kila mwanaume niliyekutana naye nilimuona kama adui, moyo wangu ulikuwa mtupu, ni nyakati hizo nilianza kuomba Mungu kuniponya na kuniondolea machungu mengi yalionizingira ”Shil anasema.

Kukubali hatma ya talaka

Shil Oloo Nyapengo

Chanzo cha picha, Shil Oloo Nyapengo

Ilimchukua muda mwanadada huyu kukubali kwamba maisha yalikuwa yamebadilika na kwamba alikuwa ameanza tena maisha ya kuwa mama mlezi wa watoto wake pekee, kila wakati anasema alijikumbusha kwamba alikuwa na uwezo wa kupona na kuendelea na maisha kama watu wengine .

Ndiposa anasema kwamba kuvunjika kwa ndoa ni kitu chenye uchungu mwingi na watu huchukua muda kupona ni sawa na mume au mke wa mtu kufariki ghafla wakati wa ndoa ndivyo anavyolifananisha suala hilo.

Pindi siku zilivyokuwa zinakwenda ndivyo alivyozidi kujipa moyo kukubali hatma na hali yake mpya , anataja hatua hizo kama mchakato wa kila siku wakati mtu anatoka kwenye ndoa.

Mafunzo mengi anasema ni kwamba alijifahamu vizuri yeye ni nani , aligundua pia katika undani wake alikuwa na uwezo wa kurejeha ujasiri , kujiamini tena kama mwanamke kwamba ni ngangari na anaweza kumudu maisha bila ya usaidizi wa mume .

Tangu wakati ndoa yake ilipoporomoka Shil amejizatiti sana kujitolea kuwa mzungumzaji katika jamii kuhusiana na jinsi mtu anaweza kusonga mbele baada ya kupatwa katika hali ya kuwa njia panda.