Waridi wa BBC: 'Niliozwa kwa mzee wa 70 nikiwa na miaka 13'
Na Anne Ngugi
BBC Swahili

Chanzo cha picha, Nancy Milanoi
Nancy Milanoi,42, ni mwanamke kutoka jamii ya kimasaai nchini Kenya. Kila mara anaporejesha nyuma mawazo yake, hasa kukumbuka miaka yake ya utotoni anabubujikwa na machozi kutokana na kile anachokitaja kuwa dhulma za utotoni ambazo zilimpa kionjo cha maisha machungu, wakati ambapo alitarajia mambo tofauti.
Bi Milanoi anasema yote hayo yanatokana na baadhi ya mila za jamii ya Wamaasai ambazo zinawaandaa watoto wa kike kwa tohara na hatimaye ndoa za mapema, licha ya mila hizo kupingwa kupitia sheria za kimataifa na elimu kwa umma.

Chanzo cha picha, Nancy Milanoi
Masaibu ya kung'olewa meno
Akiwa na miaka tisa Milanoi alipitia dhuluma yake ya kwanza ya utotoni, wakati huo ikiwa ile mila ya kungo’lewa meno mawili ya sehemu ya chini.
Mwanadada huyu anakumbuka jinsi alivyoshikwa kwa nguvu na kisu butu kupenyezwa kati kati ya meno yake ya sehemu ya chini, na kuelezea jinsi alivyohisi uchungu ambão hajawahi kusahau ingawa alifanyi hivyo miaka kadhaa iliyopita.
“Hakuna mtu aliyenifahamisha kuhusu mila ya kung’oa meno kwetu, ila nilikuwa ninawaona wakubwa kwa wadogo wakiwa hawana meno ya sehemu ya chini ,na nikadhani ni maumbile ya kawaida. Siku niliyong’olewa meno yangu nilihisi uchungu mwingi katika desturi ya kuyang’ao meno hakuna dawa ya kutuliza uchungu niliyopewa ” anakumbuka Milanoi
Mama huyu anasema kuwa hilo ilikuwa daraja la kwanza la kuwekwa alama ya utamaduni wao.
1993 Mwaka alioozwa kwa mzee wa miaka 70
Kulingana na Milanoi, “Wasichana wa Kimasai hasa wale wanaoishi vijijini wanafanya kazi za nyumbani na wakati mwingine wanawapeleka mbuzi na kondoo malishoni”.
Likizo ya shule kwake alikuwa anadhani kuwa ingemruhusu kuchanganyika na wasichana wa rika lake kushiriki hadithi nyingi za maisha yao ya utotoni .
Haikufanyika hivyo kwa Milanoi. Wazazi wake walikuwa wamepanga kumuoza, kwa mzee wa miaka 70, ambapo mila ya kimasaai haingemruhusu kumuoa kabla hajafayiwa tohara.
Ili kukidhi matakwa ya mchumba wa Milanoi, wazazi wake, ambao walikuwa wakijadili uwezekano wa kumuoza, walichagua siku ya kukeketwa kwake , ni mama yake aliyemweleza .
“Jioni hiyo, nilikuwa narejea nyumbani nilipofika niligundua , kulikuwa na nyuso tofauti, nisijue kisu cha ngariba kilikuwa kinanisubiri usiku huo ”Milanoi anasema.
Usiku huo Milanoi alipashwa tohara japo kama anavyosimulia ilikuwa kinyume na jinsi yeye mwenye alivyotaka.

Chanzo cha picha, Nancy Milanoi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miongoni mwa wamasai, msichana akishakeketwa , anatakiwa kuolewa na mtu ambaye tayari amemtolea mahari na hatakiwi kuchanganyika na watoto shuleni.
Shule zilipofungwa kwa likizo ya Aprili mwaka wa 1993, mchumba wa Milanoi, alifika katika kijiji cha Olorien kumchagua mke wake mdogo.
"Nilikuwa ndani ya nyumba, na baba yangu akatangaza kwamba ni wakati wa kufunga kilicho changu kwa sababu mume wangu amekuja kunichukua," Milanoi alisema.
Milanoi anasema baada ya babake kuzungumza, mwili wake ulikufa ganzi kwa takriban dakika 30. Kichwa chake, anasema, kilikuwa kinamzunguka kana kwamba hakikuweza kunga’mua uzito wa habari hizo .
Wakati huo alikuwa na umri wa 13 na hakuweza kuelewa wazazi wake walikuwa wanafanya nini. Alitaka kuendelea na elimu yake na hakuwa tayari kuwa mke wa mtu yeyote.
Anakumbuka Baba yake na watu wengine kijijini wakimshika Milanoi na kumuweka ndani ya gari na kumfungia ndani kwa kuwa mchumba wake alikuwa na mkutano mfupi na wanafamilia.
“Nilitazama nikiwa kwenye gari walichokuwa wakifanya kwa mbali huku nikiishiwa na nguvu, Milanoi anasema.
Siku ya kwanza kama mke
Milanoi hakuwa tayari kuozwa kwa nguvu kwa mara tatu mwanamke huyu anasimulia alivyojaribu kujinasua kutoka kwenye minyororo ya ndoa hiyo.
Siku ya kwanza, alilala na mke wa kwanza wa mume wake. Asubuhi iliyofuata, alifanya hila ya kutorokea vichakani, baada ya kutembea kwa saa kadhaa, alifika nyumbani kwa mjomba wake, ila hata huko hakuwa salama.
“Siku ya tatu nikiwa nyumbani kwa mjomba wangu, ambako nilifikiri kwamba sasa niko salama, niliona gari likija. Mzee yuleyule walishuka na mjomba wangu akanikabidhi kwake tena ,” Milanoi alisema.

Chanzo cha picha, Nancy Milanoi
Hatimaye alifaulu kutoroka ndoa ya lazima
Hatimaye mwanadada huyu aliweza kutoroka ndoa hio kabla ya kukutana kimwili na mzee huyo , aliishia kutafuta kazi za ndani kwa kuwa jamii yake wakati huo ilimtelekeza kwa kukataa kuolewa .
Ila simulizi ya maisha ya mwanzo ya mama huyu yalimpa nguvu mpya na mwelekeo mpya wa maisha ambapo alijiamini kuwa atakuwa mtetezi wa watoto wa kike ambao wanajipata kwenye mila iliyomwathiri akiwa binti .
Nancy Milanoi kwa miaka zaidi ya 15 amekuwa mwanaharakati wa kuwaokoa wasichana wa kimasai wanaokeketwa na kuozwa wakiwa na umri mdogo.
Mama huyu anasema miaka ya hivi karibuni mambo yamebadilika na watu wameanza kuacha mila inayowakandamiza watoto wa kike .












