Je, Shilingi ya Tanzania inaporomoka?Fahamu vigezo vya thamani na ufanisi wa sarafu

Sh

Chanzo cha picha, BOT

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kumekuwa na mjadala mkali nchini Tanzania kwa karibu juma moja sasa kuhusu hali ya shilingi ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mjadala unabebwa na taarifa zilizoeleza kwamba Shilingi ya Tanzania ndiyo sarafu inayofanya vibaya zaidi duniani kwa sasa, ikihusisha mwenendo huo na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje, ongezeko la deni la taifa, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida, pamoja na utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambao bado haujaanza.

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imekanusha madai haya ya kwamba shilingi ya Tanzania ndiyo inayofanya vibaya zaidi duniani kwa sasa. Hata hivyo taarifa ya Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba inakiri kwamba mwenendo wa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani, katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita hadi sasa, Shilingi ilishuka kwa asilimia 3.6.

Lakini je, tunaposema sarafu ina thamani kubwa au inafanya vizuri, tunamaanisha nini hasa? Makala hii inachambua vigezo vinavyotumika kupima thamani na ufanisi wa sarafu.

Thamani ya Sarafu na vigezo vya upimaji wake

Thamani ya Sarafu uhusisha kiwango ambacho sarafu moja inaweza kubadilishwa na nyingine, mara nyingi ikilinganishwa na Dola ya Marekani. Na sarafu huwa na mabadiliko ya kupanda na kushuka thamani.

Njia ya kawaida ya kujua thamani ya sarafu au kuithaminisha sarafu ni kupitia kiwango chake cha ubadilishaji (Exchange Rate), ambacho kinaonesha ni kiasi gani cha sarafu moja kinaweza kubadilishwa na sarafu nyingine.

'Ukiacha mipango ya kiuchumi ya nchi, kwa mtu mmoja mmoja, hili ni muhimu kuelewa jinsi viwango vya ubadilishaji huamuliwa na ni nini huchochea kubadilika kwake kunaweza kukusaidia kunufaika zaidi na fedha zako unaposafiri nje ya nchi au kutuma fedha kuvuka mipaka ya nchi," anasema Beatrice Kimaro, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Tanzania.

Katika uchumi, mifumo ya viwango vya ubadilishaji vinaweza kuwa vya kudumu (Fixed) au vinavyobadilika (Floating). Viwango vya kudumu vinahusishwa na sarafu moja au kikapu cha sarafu kwa ajili ya uthabiti, ilhali viwango vinavyobadilika hubadilika kulingana na upatikanaji na mahitaji sikoni.

Thamani ya sarafu huamuliwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji na mahitaji yake katika soko la fedha za kigeni. Ni sera inayotumika na mataifa mengi ikiwemo Tanzania, kuacha soko liamue thamani ya Sarafu ya nchi. Ikiwa mahitaji ya sarafu yanaongezeka, thamani yake hupanda, na kinyume chake. Kwa kifupi, bei ya sarafu itapanda ikiwa mahitaji yatakuwa juu, na bei yake itashuka ikiwa mahitaji ni ya chini.

Sarafu zenye thamani kubwa ndiyo sarafu zenye nguvu kubwa, ambapo nguvu ya sarafu inatafsirika kama daftari la ripoti ya fedha ya nchi. Inaonesha afya ya kiuchumi, utulivu na nguvu ya biashara ya kimataifa ya nchi.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Njia ya kawaida ya kujua thamani ya sarafu au kuithaminisha sarafu ni kupitia kiwango chake cha ubadilishaji (Exchange Rate),
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kawaida, watu wengi huamini kuwa sarafu yenye thamani kubwa ni ile inayoweza kubadilishana kwa kiwango cha juu dhidi ya Dola ya Marekani au sarafu nyingine kuu. Hili lina ukweli wake, lakini thamani ya sarafu huathiriwa na mambo mengi zaidi, yakiwemo haya matatu makubwa:

Kwanza, nchi zilizo na uchumi thabiti (Economic stability) na mfumuko wa bei wa chini huwa na sarafu zenye nguvu zaidi. Wakati bei ni thabiti na uchumi unaweza kukua kwa kasi, sarafu kwa kawaida hufuata mkondo huo.

Pili, hifadhi ya fedha za kigeni (Foreign reserves) ni kigezo muhimu. Ni kwamna kiasi cha fedha za kigeni kinachoshikiliwa na benki kuu ya nchi kinaweza kuathiri thamani ya sarafu yake.

'Akiba kubwa inaweza kusaidia kuimarisha sarafu dhidi ya shinikizo la soko', anasema Beatrice Kimaro, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi.

Kuwait ina akiba ya fedha za kigeni zaidi ya mara tano ya akiba ya Tanzania. Marekani yenyewe akiba yake ni wastani wa mara 7 ya Tanzania. Akiba hizi zimekuwa msaada mkubwa kwenye kuiimarisha sarafu za nchi hizo ambazo ni miongoni mwa Sarafu zenye nguvu na thamani kubwa duniani.

Akiba hii ya fedha za kigeni hutumika kuingilia katika soko la ndani la fedha za kigeni ili kuleta utulivu pale ambapo haupo pamoja na kufanya malipo ya fedha za kigeni.

K

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sarafu ya KWD ya Kuwait ina thamani takiriban mara tatu na nusu ya Dola ya Marekani kwa sasa. Ni moja ya Sarafu zenye thamani kubwa duniani.

Aidha uwiano wa kibiashara ni muhimu kuzingatiwa (Trade balance). Wakati nchi inapouza nje zaidi (export) kuliko inachoagiza (import), husaidia kutengeneza ziada ya biashara, kwa kufanya hivyo huimarisha sarafu yake. Hili linamaanisha wanunuzi zaidi wa kigeni wanahitaji sarafu ya ndani, na hivyo kuongeza thamani yake na nguvu yake sokoni.

Kwa ripoti za mashirika ya fedha ya kimataifa kama IMF na Benki ya dunia, Sarafu zenye thamani kubwa zaidi duniani zinajumuisha sarafu ya Dinar ya Kuwait (KWD), Dinar ya Bahrain (BHD), Rial ya Oman (OMR), Pauni ya Uingereza (GBP), na Dinar ya Jordan (JOD).

Kwa msingi huo, sarafu kama Dinar ya Kuwait (KWD), Dinar ya Bahrain (BHD) na Rial ya Oman (OMR) zinaendela kuwa na thamani kubwa zaidi duniani kwa sababu ya hifadhi kubwa ya fedha za kigeni kama moja ya sababu. Lakini zaidi pia wanabebwa na hifadhi zao za mafuta na sera thabiti za kifedha zinazosimamiwa na serikali zao.

Ufanisi na kufanya vizuri kwa Sarafu

Thamani ya sarafu ni suala pana zaidi ya ubadilishaji wake dhidi ya dola ya Marekani. Ni muhimu kutofautisha kati ya sarafu yenye thamani kubwa na sarafu inayofanya vizuri zaidi, kwa sababu ni vipimo viwili tofauti.

Sarafu inayofanya vizuri (best-performing currency) ni ile inayoongezeka thamani kwa kasi ndani ya kipindi fulani, hata kama bado ina kiwango cha chini cha ubadilishaji ama thamani yake iko chini.

Kwa mfano, ikiwa sarafu ilikuwa inabadilishwa kwa 1 USD = 100 TZS mwezi uliopita, lakini sasa inabadilishwa kwa 1 USD = 90 TZS, inamaanisha kuwa shilingi imeimarika kwa asilimia 10. Kasi hii ya kuimarika ndiyo huifanya iwe miongoni mwa sarafu zinazofanya vizuri zaidi, hata kama bado ina thamani ndogo ukilinganisha na sarafu nyingine.

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sarafu ya Peso ya Mexico (MXN), ilikuwa moja ya safari zilizokuwa zinafanya vibaya zaidi mwaka 2016, na ikaendelea kutofanya vizuri na kutokuwa imara dhidi ya dola ya Marekani mpaka mwanzoni mwa 2020.

Vigezo vinavyotumika kupima kasi ya kuongezeka kwa thamani ya sarafu ni pamoja na kiwango cha ubadilishaji wa sarafu (exchange rate movements), uwekezaji wa kigeni, urari wa malipo, mfumuko wa bei na sera za kifedha za benki kuu.

Kwa mujibu wa Shirika la fedha duniani (IMF) baadhi ya sarafu zinazofanya vizuri duniani ni pamoja na;

  • Ruble ya Urusi (RUB). Licha ya vita vya Ukraine vinavyoendelea, sarafu hii imekuwa ikifanya vizuri hivi karibuni kutokana na mahitaji yake, kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa nje, wanaolazimika kutumia sarafu hii kwa baadhi ya bidhaa na huduma za Urusi badala ya dola.
  • Peso ya Mexico (MXN): Sarafu hii imepata nguvu kutokana na uwekezaji mkubwa wa kigeni na biashara za kigeni.
  • Real ya Brazil (BRL) imeongezeka nguvu sokoni kutokana na ukuaji wa sekta ya kilimo.
  • Dola ya Singapore (SGD), ambazo zote zimeimarika kwa sababu ya kuongezeka kwa uwekezaji wa kigeni na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
  • Baht ya Thailand (THB), ambayo imeimarika kutokana na ukuaji wa sekta ya utalii na mauzo ya bidhaa za nje.

Je, Shilingi ya Tanzania inafanya vibaya?

Kwa kuzingatia vigezo vya kupima thamani ya sarafu na takwimu za hivi karibuni, shilingi ya Tanzania haioneshi kufanya vibaya sana kama inavyotajwa. Imekuwa ikishuka na kupanda kwa viwango visivyotisha. Vigezo vinavyohusisha uchumi wenyewe, utulivu wa bei, kupungua kwa nakisi ya urari wa malipo ya kawaida, na uimara wa sekta ya fedha ni muhimu kwenye kuipima thamani ya shilingi ya Tanzania na kufanya kwake vizuri ama vibaya.

Kumekuwa na kupanda na kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita mpaka kufikia Machi, 2025. Katika kipindi hicho Shilingi ilishuka thamani kwa asilimia 3.6. Lakini kuanzia Julai hadi Desemba 2024, Shilingi iliongezeka thamani kwa asilimia 9.51.

Kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, hiyo iliifanya "kuwa Sarafu iliyofanya vizuri zaidi duniani (kwa kipindi hicho) kabla ya kubadilika tena kuanzia Januari 2025'.

A

Chanzo cha picha, Ge

Ziko sababu kadhaa za kuporomoka tena kuanzia Januari, 2025 kama BOT ilivyobainisha; kwamba kulitokana na mzunguko wa msimu wa mabadiliko ya fedha za kigeni nchini na sera ya fedha za kigeni ya BOT, inayoruhusu kubadilika kwa thamani ya sarafu kulingana na nguvu za soko. Kama ilivyo nchi nyingi, thamani ya Shilingi ya Tanzania inaendelea kuamuliwa na nguvu ya soko na upatikanaji wa fedha za kigeni sokoni, huku Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ikishiriki kwa kiwango kidogo kupitia sera za kifedha.

'Kuimarika kwake na kufanya vizuri kwake dhidi ya Dola ya Marekani mwishoni mwa mwaka jana, udhibiti wa mfumuko wa bei, na ongezeko la akiba ya fedha za kigeni ni viashiria vya uchumi unaoimarika", anasema mchumi, Beatrice Kimaro.

Hili la uchumi kuimarika, linabebwa na ukuaji wa kasi wa uchumi wa kiwango cha asilimia 5.4 mwaka 2024, ambao si haba, na kupungua kwa nakisi ya urari wa malipo ya kawaida hadi kufikia asilimia 2.7 ya Pato la Taifa mwaka 2024 kutoka asilimia 3.7 miaka miwili iliyopita (2023). Hilo linaipa thamani Shilingi ya Tanzania kunakobebwa pia na kuimarika kwa mauzo ya nje, hasa katika sekta za kilimo, madini na utalii katika kipindi husika.

a

Chanzo cha picha, BOT

Maelezo ya picha, Viwango vya kubadilisha fedha dhidi ya Shilingi, kwa mujibu wa BOT, kwa siku ya Machi 25, 2025

Ingawa shilingi ya Tanzania imepungua thamani kwa kiasi fulani sasa, hiyo haimaanishi kuwa ni mojawapo ya sarafu zinazofanya vibaya zaidi duniani. Hali ya uchumi wa dunia, uwekezaji wa kigeni na sera za kifedha ndizo zinazoamua mwenendo wa sarafu.

Badala ya kuhofia kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania, ni muhimu kuelewa vyanzo vya mabadiliko haya na kuchukua hatua za kuimarisha uchumi ili kuhakikisha sarafu inakuwa thabiti kwa muda mrefu.

'Kwa sababu shilingi ilifanya vizuri mwishoni mwa mwaka hadi Disemba, lakini ulipoanza mwaka, imeonesha kuyumba, ni lazima kudhibiti uimara na nguvu yake kwa muda mrefu', anasema Kimaro.

Analosema mchumi huyu, linawezekana na muhimu kwa mamlaka za kifedha kuendelea kufuatilia na kushughulikia changamoto zinazoweza kuathiri uthabiti wa shilingi katika muda mrefu.

Hakuna njia ya mkato kwenye eneo hili, inapaswa kuendelea kudumisha uthabiti wa uchumi kupitia sera za kifedha zinazotekelezeka, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha utulivu wa bei ya Shilingi ya Tanzania.