Kenya yawasilisha malalamiko rasmi kwa EAC dhidi ya hatua ya Tanzania kupiga marufuku biashara za kigeni

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Kenya imeiandikia rasmi Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupinga agizo tata la Tanzania la kupiga marufuku watu wasio raia kujihusisha na shughuli mbalimbali za kibiashara, ikionya kuwa hatua hiyo inatishia ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Caroline Karugu Alhamisi alithibitisha kuwa Kenya iliwasilisha malalamiko rasmi kwa jumuiya hiyo ya kikanda, na kuitaka kuishinikiza Tanzania kupitia upya Agizo la Leseni za Biashara (Marufuku ya Shughuli za Biashara kwa Wasio Raia), 2025.
Agizo hilo lililotolewa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Tanzania, Selemani Saidi Jafo Jumanne, linawawekea vikwazo wageni kujihusisha na aina 15 za biashara, linatoa adhabu kubwa ikiwa ni pamoja na faini isiyopungua TSh10 milioni (Ksh.501, 584), kifungo cha hadi miezi sita, na kufutiwa viza na vibali vya ukaazi.
Dkt. Karugu amesema maagizo hayo “yanakiuka moja kwa moja” Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC, hasa Ibara ya 13(1), 13(3)a, 13(5), 13(8), na 13(9), ambayo inalinda uhuru wa watu, huduma, na haki ya kuanzishwa miongoni mwa nchi washirika.
"Agizo hili linadhoofisha malengo ya msingi ya ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na kurudisha nyuma kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyopatikana chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC," Dkt. Karugu alisema.
Kenya sasa inataka Sekretarieti ya EAC kuitaarifu Tanzania kuhusu wajibu wake chini ya Mkataba wa EAC na sheria za jumuiya na kushinikiza kuangaliwa upya kwa agizo hilo.













