Je, sera ya "Tazama Mashariki" iliilinda Iran?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow katika siku za mwisho za vita vya Israel na Iran.
Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati mwandishi wa habari wa Marekani Tucker Carlson alipomuuliza Rais wa Iran Masoud Pezzekian ikiwa China au Urusi ingeiunga mkono Iran iwapo mzozo kati ya Marekani au Israel utaongezeka, Pezzekian alikwepa jibu la moja kwa moja.

Tehran haijaikosoa rasmi Beijing au Moscow kwa kukataa kutoa msaada wa moja kwa moja wa kijeshi wakati wa vita vya siku 12 na Israel mwezi Juni. Hata hivyo, kuna sauti ndani ya Iran zinazozungumzia hisia ya kuwa "pweke" mbele ya mashambulizi ya Marekani na Israel.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imepitisha fundisho la "Tazama Mashariki", kama ilivyoainishwa na Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei. Sera hiyo inalenga kukabiliana na vikwazo vya Magharibi kwa kuimarisha uhusiano na China, Urusi na mataifa mengine yenye nguvu za kikanda.

Kama sehemu ya mkakati huu, Tehran imejiunga na jumuiya za kimataifa kama vile BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na pia imepanua ushirikiano wake wa kijeshi na Moscow, ikiwa ni pamoja na kutuma ndege zisizo na rubani kusaidia Urusi katika vita vyake nchini Ukraine.

Iliaminika sana kuwa Iran ilitarajia kupokea ndege za kivita za Urusi na mifumo ya ulinzi wa anga kama malipo. Lakini kukataa kwa Urusi kutoa vifaa hivi, kwa kuzingatia vita vya Ukraine, kumezua mashaka juu ya nguvu ya muungano huu.

Pia unaweza kusoma

Iran na Urusi: Washirika wasio na muungano?

Kulikuwa na wasiwasi nchini Iran kwamba nchi hiyo inaweza kutumika kama "kadi ya maafikiano" kati ya shughuli za Moscow na Washington. Wasiwasi huu uliongezeka baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kufafanua wakati wa vita kwamba makubaliano yaliyotiwa saini hivi karibuni na Tehran hayakujumuisha kifungu cha ulinzi wa pande zote, na kwamba Iran haikuomba msaada wa kijeshi hapo awali.

Katika kile kilichoonekana kuwa ni jaribio la kudhibiti matarajio, tovuti ya lugha ya Kiajemi inayohusishwa na serikali ya Urusi Sputnik ilimnukuu mchambuzi akisema kwamba Moscow haitaunga mkono upande wowote katika vita kati ya Iran na Israel, kwani ina "uhusiano hai wa kidiplomasia" na nchi zote mbili.

Vyombo vya habari vya Iran vinavyopenda mageuzi, ambavyo kijadi vinaitazama Urusi na jicho la pili, vilikosoa Urusi, kwamba haikuchukua "hatua zozote za maana" - kama vile kutuma wanajeshi au ndege za kivita kama onyo kwa Marekani - na hazikujaribu kuishinikiza Washington kusitisha vita.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ingawa ukosoaji ulikuwa na nguvu zaidi katika vyombo vya habari , baadhi ya vyombo vya habari vya kihafidhina na vyenye misimamo mikali pia vilionyesha kutofurahishwa kwao.

Mnamo Julai 15, gazeti la kihafidhina la Farhikhtegan lilimnukuu mtaalamu akisema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi aliwasilisha hasira za Khamenei kwa Putin wakati wa ziara yake huko Moscow katika siku za mwisho za vita.

Baadaye gazeti hilo lilifafanua kwamba taarifa za mtaalamu huyo "hazikuwa na usahihi unaohitajika."

Gazeti lenya msimamo mkali la Tandro Javan, lenye mafungamano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, liliandika katika ripoti yake kuhusu mkutano wa Julai 20 kati ya Putin na Ali Larijani, mshauri wa Khamenei, kwamba "Warusi na Wachina lazima wagharamike zaidi kwa kuushinda utawala wa Marekani nchini Iran.

Nematollah Izadi, balozi wa zamani wa Iran nchini Urusi, aliiambia tovuti ya wanamageuzi ya Jamaran kwamba Urusi "bila shaka" itaichagua Israel ikiwa itapewa chaguo kati ya Iran na Israel.

Pia aliikosoa Iran kwa kutoweka uwasilishaji wa ndege zisizo na rubani kuwa na masharti ya kupokea uungwaji mkono wa kijeshi.

Mbunge wa zamani Heshmatollah Falahatpisheh pia alisema kuwa Iran "ililipa gharama ya vita vya Ukraine" wakati wa mzozo na Israel na kuelezea matamshi ya Putin kama jaribio la "kuepuka madeni ya kihistoria."

Mbunge wa zamani Ali Motahari pia alilaani msimamo wa Putin, akisema kwamba wakati Iran imeipa Urusi ndege zisizo na rubani, Moscow imekataa kuuza mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kwa Tehran, lakini imewasilisha mfumo huo kwa Uturuki na Saudi Arabia.

Baadhi ya wachambuzi wa kimataifa wanaamini kwamba uwezo mdogo wa Moscow wa kuisaidia Iran unatokana na mzozo wake wa kijeshi nchini Ukraine, sawa na vile ilivyopata shida kumuunga mkono Rais wa Syria, Bashar al-Assad, mshirika wa pamoja wa Moscow na Tehran.

Kwa upande mwingine, Iran haionekani kuwa na ushawishi mkubwa juu ya Urusi. Moscow imeweka ndani uzalishaji wa ndege zisizo na rubani za Iran huko Tatarstan, ili juhudi zake za vita zisitegemee tena moja kwa moja vifaa vya Iran.

.

Chanzo cha picha, Russia Defence Force

Je, Iran inaweza kutegemea China kama msaidizi wake wa kijeshi?

Kwa kuzingatia kutotaka au kutokuwa na uwezo wa Urusi kutoa msaada wa kijeshi, Iran inaweza kugeukia China - mshirika wake mkuu wa kiuchumi na mnunuzi mkubwa wa mafuta.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa vita hivyo, chombo cha habari cha Middle East Eye kiliripoti kuwa China imewasilisha mifumo mipya ya ulinzi wa anga nchini Iran.

Ripoti hii ilikanushwa mara moja na ubalozi wa China nchini Israel, lakini pia ilizua ukosoaji mpya katika vyombo vya habari vya Iran, ambavyo viliita Beijing "rafiki wa nusu-nusu."

Katika mahojiano yake na Jamaran, Izadi alisema kuwa uhusiano wa Iran na China ni wa kiuchumi.

Gazeti la wanamageuzi Hammihan pia lilisema kuwa uhusiano wa Beijing na Israel uliweka "vizuizi vya kimkakati" katika kuisaidia Iran katika migogoro inayohusisha Marekani na Israel. Gazeti hilo lilihitimisha kuwa hakuna mhimili wa Iran-Urusi-China.

Je, Iran imeteseka kutokana na "kutengwa kijiografia"?

Chaguzi za Iran zinaonekana kuwa na mipaka. Inategemea uhusiano wake wa kiuchumi na Urusi na China na uungaji mkono wao wa kisiasa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hasa hivi sasa ambapo nchi zilizotia saini makubaliano ya JCPOA zimetishia kuamsha utaratibu wa vichochezi vya kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Ingawa baadhi ya maingiliano ya hivi majuzi, kama vile uwepo wa Waziri wa Ulinzi Aziz Nasirzadeh katika mkutano wa Larijani na Putin, yanaweza kuashiria makubaliano ya siri ya kijeshi, Iran inahitaji zaidi ya uwasilishaji wa vifaa vya hapa na pale.

Utawala wa anga wa Israeli juu ya anga ya Iran wakati wa vita ulionyesha hitaji la msaada mkubwa wa ulinzi.

"Mhimili wa Upinzani" - mtandao wa vikundi vya wakala wanaounga mkono Iran kote Mashariki ya Kati - umedhoofishwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika makabiliano ya kikanda na Israel, na kuiacha Iran kwa mara nyingine tena katika nafasi ya kutengwa kijiografia katika tukio la vita vikubwa na Israeli na labda Marekani.

Hisia hii ilionekana wazi katika ripoti katika shirika la habari la Tasnim. Afisa mmoja wa usalama na kijeshi ambaye jina lake halijatajwa aliliambia shirika la habari linaloshirikiana na IRGC tarehe 21 Juni kwamba licha ya juhudi za ndani za kutengeneza silaha za hali ya juu, vikwazo vya Marekani vimeinyima Iran fursa ya kupata teknolojia ya hali ya juu na ushirikiano wa kisayansi na nchi zilizoendelea.

Alihitimisha kwamba Iran inasalia katika hali ya "kutengwa kisiasa kijiografia

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla