Boko Haram: Hizi ndizo sababu sita za serikali ya Nigeria kushindwa kuliangamiza kundi la kigaidi la Boko Haram

Boko haram imeaihangaisha Nigeria kwa miaka kadhaa

Chanzo cha picha, AFP

Msemo kwamba kundi la wanamgambo wa Nigeria Boko Haram lilikuwa "limeangamizwa" sasa umeanza kukosa maana.

Miezi saba tangu muhula wake wa kwanza mnamo 2015 Rais Muhammadu Buhari alianzisha msemo huo , lakini kundi hilo na yake halijawahi kuondoka.

Wanajeshi wameweza kuchukua maeneo yaliyokuwa yamekaliwa na Boko Haram na kuwaondoa wapiganaji kutoka katika baadhi ya maficho yao. Lakini kuongezeka kwa mashambulizi mabaya hivi karibuni, hasa kaskazini mashariki, ambapo kikundi hicho kilianza uasi wake mnamo 2009, kumesababisha wengi kuuliza ni nini chanzo cha kutofaulu kwa mamlaka za Nigeria.

Tayari mwaka huu kumekuwa na mashambulio karibu 100, kulingana na tathmini moja, huku raia na jeshi wakilengwa. Mamia wameuawa na silaha, chakula na dawa zote zimeporwa.

Kuna sababu kuu sita kwa nini Boko Haram haijashindwa licha ya madai ya serikali, wataalam wanasema.

1. Kiini cha matatizo hakijashughulikiwa

Kutegemea zaidi mkakati wa kijeshi kukabiliana na Boko Haram ni kiini cha hali ya serikali kutoweza kukabiliana na tishio hilo , anasema mchambuzi wa usalama Kabiru Adam kutoka Beacon Consulting.

Hundreds of thousands have fled their homes in north-east Nigeria and found shelter in displaced people's camps

Chanzo cha picha, AFP

"Ndiyo sababu, kwa bahati mbaya, karibu miaka 11 au 12 katika operesheni ya kupambana na uasi, hatuoni mafanikio makubwa," aliiambia BBC.

"Ndio, jeshi litawaondoa magaidi lakini kwa sababu bado wana uwezo wa kutumia ushawishi, wana uwezo wa kuajiri, wana uwezo wa kutoa ufadhili, wana uwezo wa kupata silaha, kisha wanajipanga upya."

Wataalam wanasema kwamba sio kuwa watu wa kaskazini mashariki wanahurumia Boko Haram na washirika wake , Islamic State West Africa Province, lakini kwamba kupuuzwa kutoka kwa mamlaka na kukata tamaa mara nyingi huwashawishi watu kujipata mikononi mwa wapiganaji hao

"Ukweli ni kwamba kushughulikia uasi au ugaidi, unahitaji zaidi ya operesheni ya kijeshi. Unahitaji kushughulikia sababu kuu za uasi," Bw Adamu anasema.

"Kwa bahati mbaya hatujaona juhudi za kutosha katika suala hilo."

Anaashiria ukosefu wa utawala bora ambao unawaacha watu wakiwa masikini, wamechanganyikiwa na hawajasoma kama "sababu kuu".

Kuna mipango mikubwa ya serikali ambayo imekusudiwa kuharakisha maendeleo kaskazini mashariki, lakini maendeleo adimu sana yamepatikana.

Kuna pia Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ugaidi ambao pia unajumuisha maendeleo ya uchumi na kupambana na itikadi kali , pamoja na kupelekwa kwa wanajeshi. Lakini Bw Kabiru anasema inaonekana mkakati huo hautekelezwi kikamilifu.

Wengine, kama mchambuzi wa Usalama katika Taasisi ya Mabadiliko ya Tony Blair, Bulama Bukarti, wanasema kuwa pamoja na kumaliza mafunzo ya itikadi kali azima kuwe na kuongezwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi sawa na ile iliyoonekana huko Iraq na Syria wakati wa mapambano dhidi ya kundi la Islamic State

2: Uwezo wa Boko Haram kuwasajili vijana

Umaskini wa kawaida katika sehemu za mkoa huo na vile vile njia za vurugu za waasi zinawezesha kuendelea kuajiri kizazi baada ya kizazi cha wapiganaji, wataalam wanasema.

"Watu wanapatikana kwa urahisi kuajiriwa ili kuishi tu," mtaalam wa usalama Abdullahi Yalwa alisema, akitoa mfano wa shida za ukosefu wa ajira na utawala duni.

Bwana Bukarti anaangazia "kampeni ya kimfumo ya kuajiri vijana kwa lazima".

Gavana wa jimbo la Borno, Babagana Zullum, hivi karibuni aliambia BBC kwamba waasi walikuwa wakiajiri hata watu ambao hapo awali walilazimishwa kutoka nyumbani mwao na mzozo wenyewe.

3: Ukosefu wa vifaa

Hata linapokuja suala la mapigano kuna shida ya silaha, kulingana na Bw Adamu, ambaye anasema kuwa jeshi halina silaha zifaazo

Utafiti wa kampuni yake, Beacon Consulting, uligundua kwamba kulikuwa na silaha ndogo ndogo na nyepesi milioni 6.5 zinazosambazwa nchini Nigeria lakini ni 586,000 tu mikononi mwa vikosi vya usalama.

The military have managed to capture some weapons from Boko Haram, as seen here in 2019

Chanzo cha picha, AFP

Bw Adamu pia anasema kuwa "tunachokiona kulingana na ushahidi ni kwamba vikundi hivi [vyenye silaha] vina silaha kali kwa bahati mbaya, kuliko jeshi".

4: Ufisadi

Rushwa inaweza kuwa jambo moja ambalo linawarudisha nyuma jeshi wakati wa kuboresha vifaa vyake. Inashukiwa kuwa pesa nyingi zilizokusudiwa kuimarisha kampeni dhidi ya Boko Haram zimeishia mifukoni mwa maafisa.

Bwana Yalwa anasema kuwa katika visa vingine vita dhidi ya Boko Haram haipiganiwi kwa "uaminifu" na "inaonekana watu wengine wameigeuza kuwa bidhaa na wamejitajirisha".

Katika miaka ya hivi karibuni, jeshi limelemazwa na vikwazo vya kununua silaha kutoka Marekani juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Rais Buhari na mtangulizi wake, Goodluck Jonathan, wote walilalamika kuwa hii ilikuwa ikikwamisha juhudi za kupambana na uasi.

Lakini vikwazo hivyo viliondolwa na Rais Donald Trump mnamo 2018 na kwa sababu hiyo Nigeria inatarajia ndege za Super Tucano. Hii inapaswa kuipa uwezo zaidi wa angani ambao Bwana Adamu anaamini haitumiwi kwa faida yake kamili.

Ingawa kuna madai kwamba hata ubora huu haulipi.

5: Mikakati ya kijeshi haina ufanisi

Bw Bukarti aliiambia BBC waasi hao wanaonekana kuwa "wameelewa na kukabiliana na mtindo wa mashambulizi ya angani" na wanatumia hali ngumu ya kijiografia katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kukwepa mashambulio ya kijeshi.

Boko Haram:Historia fupi

• Ilianzishwa mnamo 2002

• Hapo awali ililenga kupinga elimu ya Magharibi

• Ilizindua shughuli za kijeshi mnamo 2009

• Ilitambulika mnamo 2014 na utekaji nyara wa Chibok

• Iliapa kutii uongozi wa kundi la Islamic State mnamo 2015

• Liligawanyika katika vikundi viwili mnamo 2016

Kuna pia mambo mengine ya kimkakati ambayo pia yamekosolewa.

Katika kipindi cha mwaka uliopita jeshi limekuwa likiondoa wanajeshi kutoka kwa vituo vidogo na kuwaweka katika makundi makubwa kwenye kambi zinazojulikana kama Super Camps.

Mkakati huu ulipitishwa mwanzoni mwa 2020 wakati wanajeshi walikuwa wakishambuliwa mara kwa mara na silaha zao kuibwa

Walakini, imeacha idadi kubwa ya jamii za vijijini bila kinga, wachambuzi wanasema.

"Tuna ushahidi unaopendekeza kuongezeka kwa mashambulio kwa jamii kati ya kipindi ambacho Kambi Kuu ziliundwa na sasa. Kwa hivyo ni wazi kwamba Kambi kuu ziliacha jamii za vijijini zikiwa hatarini zaidi," anasema Bw Adamu.

Hii pia imeharibu maisha ya watu wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wanaotegemea uvuvi na kilimo cha mazao, na ikaathiri uzalishaji wa chakula.

Wanajeshi pia wanakwamishwa na mapungufu katika ukusanyaji wa habari za ujasusi na vile vile hawawezi kuziba uvujaji wa habari.

Hii inamaanisha kuwa wakati mwingine inaonekana kwamba "waasi wako mbele ya jeshi", Bw Yalwa anasema.

Jeshi hata hivyo linapinga madai hayo. Msemaji wake Mohammed Yarima hivi karibuni alisema kwamba "wanajeshi wako tayari kupigana na wameamua kama wakati wowote kuwaondoa waasi kutoka maeneo ya [kaskazini-mashariki]

6: Ushawishi wa Boko Haram unasambaa

Kuongezea tatizo la kukabiliana na Boko Haram ni kwamba uasi, uliokuwa unafanyika kaskazini mashariki tu, unaonekana kuenea.

Kuna wasiwasi kwamba magenge ya wahalifu wenye silaha katika maeneo mengine ya kaskazini na katikati mwa nchi yanaunda uhusiano na wanamgambo hao.

Mwaka jana, Boko Haram ilitoa video inayodai kuwapo katika jimbo la Niger ambalo ni mbali na eneo lake la kawaida la shughuli. Mamlaka huko ilitoa taarifa mnamo Machi ikisema wapiganaji wa Boko Haram walikuwa wamejipenyeza katika jimbo wakijificha kwenye misitu na kushambulia jamii.

Mnamo Desemba iliyopita, mkuu wa jeshi wakati huo Luteni Jenerali Yusuf Tukur Buratai alisema kwamba vita dhidi ya Boko Haram vinaweza kuendelea kwa miaka mingine 20 ikiwa za kijeshi hazingeweza kuratibiwa vizuri.

Wakazi wenye taabu sana wa kaskazini mashariki mwa Nigeria watatumai utabiri huo hautatimia kwani itamaanisha mateso kwa miaka mingine 20