Iran: Tuna masharti matatu ya mazungumzo na Marekani

.

Chanzo cha picha, EPA

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika mkesha wa mazungumzo na nchi tatu za Ulaya, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi kwa mara nyingine amesisitiza masharti ya Tehran katika mazungumzo na Washington na kusema kwamba Marekani lazima ipate imani ya Iran, si kutumia mazungumzo kwa ajili ya ajenda fiche kama vile hatua za kijeshi, na kutambua haki za Iran chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezi, ikiwa ni pamoja na kurutubisha.

Bwana Gharibabadi, ambaye yuko New York, alitoa ripoti kwenye Mtandao wa X kuhusu shughuli zake tatu katika Umoja wa Mataifa na kwa mara nyingine akaorodhesha masharti ya Iran ya kufanya mazungumzo na Marekani.

Anatarajiwa kufanya mazungumzo kesho asubuhi na wawakilishi wa nchi tatu za Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani katika Ubalozi mdogo wa Iran mjini Istanbul, Türkiye.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amesema kuhusu mazungumzo ya kesho: "Mazungumzo ya kesho ni mwendelezo wa mazungumzo ya awali, na walimwengu wanapaswa kujua kwamba misimamo yetu iko wazi na haijabadilika.

"Hasa baada ya vita vya hivi majuzi, ilikuwa ni lazima kwao kufahamu kwamba misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuwa imara na thabiti. Urutubisjhaji wetu utaendelea na sio kwamba tunaacha haki hii ya watu wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia alisema katika siku za hivi karibuni kwamba Tehran haitarudi nyuma kutoka kwa haki yake ya kurutubisha madini ya uranium na mpango wake wa makombora.

Vile vile amezungumzia utayarifu wake wa kufanya mazungumzo na kufikia mapatano sawa na JCPOA na serikali ya Marekani, ingawa amesisitiza kuwa kwa mtazamo wa Tehran, "masharti ya mazungumzo ya moja kwa moja hayawezekani kwa sasa," lakini Iran iko tayari kuihakikishia Marekani kwamba mpango wake wa nyuklia utaendelea kuwa wa amani badala ya kuondolewa vikwazo vya Magharibi.

Kulingana na ripoti, Bwana Gharibabadi alifanya mikutano tofauti mjini New York na mabalozi wa Urusi na China (wajumbe wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama) na wanachama 10 wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bw. Gharibabadi ni mmoja wa wapatanishi watakaokutana kesho mjini Istanbul na wawakilishi wa nchi tatu: Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.

Mazungumzo haya yanafanyika katika ngazi ya manaibu waziri wa mambo ya nje

Pia unaweza kusoma
h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Araqchi: Urutubishaji utaendelea
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Makubaliano ya mazungumzo haya yalitangazwa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrow kuonya kuhusu uanzishaji wa chombo hicho karibu siku kumi zilizopita, akisema kwamba ikiwa hakuna maendeleo madhubuti yatapatikana katika makubaliano ya nyuklia na Iran, nchi hizo tatu - Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani - zitaanzisha utaratibu wa hatua za kuchukua mwishoni mwa Agosti.

Aliwaambia waandishi wa habari: "Ufaransa na washirika wake wana haki ya kuweka tena vikwazo vya kimataifa [dhidi ya Iran] kwa silaha, benki na zana za nyuklia ambavyo viliondolewa miaka 10 iliyopita."

Ijapokuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inasisitiza kwamba utaratibu wa kuchukua hatua "hauna msingi wa kisheria na kimaadili," imekubali kufanya mazungumzo na nchi tatu za Ulaya huko Istanbul.

Baada ya kusitishwa kwa vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika azimio la pande mbili lenye kichwa "Sheria inayowajibisha Serikali Kusimamisha Ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki" iliweka vikwazo kwa ushirikiano wa serikali ya Iran na Shirika hilo.

.

Chanzo cha picha, Anadolu Agency via Getty Images

Maelezo ya picha, Katika mkesha wa mazungumzo na nchi tatu za Ulaya mjini Istanbul, Uturuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi kwa mara nyingine alisisitiza masharti ya Iran kwa mazungumzo na Marekani

Bwana Gharibabadi alisema jana kwamba Iran imekubali ziara ya timu ya kiufundi ya IAEA mjini Tehran katika muda wa wiki mbili hadi tatu zijazo, lakini ujumbe huo hautatembelea vituo vya nyuklia vya Iran katika safari hii.

Baada ya kuafikiwa kwa makubaliano ya JCPOA mwezi Julai 2015, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha makubaliano hayo katika azimio na kufuta maazimio yote ya hapo awali, ikiwemo vikwazo dhidi ya Iran.

Katika utaratibu wa utatuzi wa mizozo uliokusudiwa katika JCPOA, inawezekana kwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kurejesha vikwazo vilivyoondolewa iwapo hawataridhika na utekelezaji wa Iran wa majukumu yake.

Kwa mujibu wa JCPOA, mara tu utaratibu wa kichochezi utakapoanzishwa, hakuna mwanachama yeyote wa kudumu wa Baraza la Usalama anayeweza kupinga rasimu ya azimio hilo la kuzuia kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran.

Ikiwa nchi itatumia kura yake ya turufu, kwa hakika inapinga kuendelea kuondolewa kwa vikwazo, jambo ambalo lina maana ya kurejeshwa mara moja kwa maazimio yote ya Baraza la Usalama dhidi ya Iran.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla