Papa Leo kuzuru miji minane katika safari ya kwanza nje ya nchi
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 69 ametumia muda wake mwingi akitumikia nchini Peru, na ana uraia wa Marekani na Peru.
Papa Leo atatembelea miji minane nchini Uturuki na Lebanon baadaye mwaka huu, Vatican ilisema Jumatatu ya tarehe 27 Mwezi Oktoba mwaka huu.
Itakuwa safari yake ya kwanza nje ya Italia kama papa, na anatarajiwa kutoa wito wa amani katika eneo lote.
Leo, papa wa kwanza wa Marekani, atazuru Uturuki kuanzia Novemba 27 hadi 30 na kisha atakuwa Lebanon kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 2.
Mtangulizi wa Leo Papa Francis alikuwa amepanga kuzuru nchi zote mbili lakini hakuweza kwenda kwa sababu ya afya yake kuwa mbaya.
Francis alifariki Aprili 21 na Leo alichaguliwa kuwa papa mpya Mei 8 na makadinali wa dunia.
Leo pia atakutana na Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan katika mji mkuu Ankara, atatembelea Msikiti wa Blue huko Istanbul, na ataadhimisha Misa ya Kikatoliki katika uwanja wa Volkswagen Arena wa Istanbul.
Kusafiri ng’ambo kumekuwa sehemu kubwa ya upapa wa kisasa, huku mapapa wakitafuta kukutana na Wakatoliki wenyeji, kueneza imani, na kufanya diplomasia ya kimataifa.
Safari za kwanza za papa mpya kwa kawaida huonekana kama dalili ya masuala ambayo papa anataka kuangazia wakati wa utawala wake.
Uturuki na Lebanon ni nchi zenye Waislamu wengi, na Francis alitilia mkazo sana mazungumzo ya Waislamu na Wakatoliki wakati wa utawala wa miaka 12 uliojumuisha safari 47 nje ya nchi.
Kauli mbiu rasmi ya safari ya Leo Lebanon ni "Heri wapatanishi".
Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon asema nyumba yake inashambuliwa
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kiongozi wa upinzani nchini Cameroon Issa Tchiroma Bakary anasema watu wawili wameuawa na wavamizi mbele ya nyumba yake huko Garoua, huku mvutano ukizidi baada ya uchaguzi.
Katika chapisho kwenye mtandao wake wa kijamii, alisema raia waliopiga kambi nje ya nyumba yake walikuwa wakipigwa risasi "karibu." "Heri mniue lakini nitaikomboa nchi hii kwa njia yoyote ile," Tchiroma Bakary alitangaza, akielezea vitendo hivyo kama "udubutu uliyopitiliza wa uvunjaji wa sheria"
Aliweka mtandaoni picha na video ya watu wenye silaha wakiwa juu waliokuwa juu ya nyumba wakifyatua risasi mara kadhaa.
BBC haijathibitisha uhalisia wa video na picha hizo, au majeruhi waliotajwa.
Matukio haya yanajiri baada ya Rais aliye madarakani Paul Biya akitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa takribani asilimia 54 ya kura
Upinzani ulitangazwa kuwa wa pili, kwa asilimia 35.
Maandamano yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa huku baadhi ya raia wakihofia kuwa taifa hilo la Afrika ya Kati lhuenda likatumbukia katika mgogoro wa baada ya uchaguzi.
Chanzo cha picha, Issa Tchiroma Bakary/Facebook
Kenya, Tanzania kukabiliwa na dhoruba ya tropiki inayojulikana kama 'Chege' - KMD
Chanzo cha picha, Meteo/X
Maelezo ya picha, Idara ya hali ya hewa nchini Kenya yatoa onyo ya mvua kubwa inayoambatana na upepo mkali pwani ya Afrika Mashariki
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya (KMD) imetahadharisha kwamba mvua kubwa inatarajiwa kunyesha katika pwani ya kusini kutokana na dhoruba ya kitropiki inayoitwa “Chenge”.
Dhoruba hii, inayojulikana kama Chenge residual depression, ni eneo la shinikizo la chini katika Bahari ya Hindi, likisogea magharibi kwa kasi ya 11 km/h, takriban kilomita 500 kaskazini mwa Madagascar, likiwa na upepo wa 55 km/h, milipuko hadi 75 km/h, na shinikizo karibu na 1000 hPa.
KMD imesema katika taarifa Jumapili kuwa dhoruba inaendelea kudhoofika wakati ikisogea magharibi kupitia Kituo cha Kaskazini cha Mozambique, lakini ukaribu wake na pwani unaweza kuathiri hali ya hewa nchini Kenya na baadhi ya maeneo ya Tanzania.
“Mvua kubwa inatarajiwa kunyesha sehemu mbalimbali za nchi, huku upepo mkali wa zaidi ya 25 knots uwezekano kufika pwani ya kusini Jumatatu na Jumanne,” taarifa hiyo ilisema.
Wakazi wa maeneo haya, hasa wanaojihusisha na shughuli za baharini, wametakiwa kuwa makini, kuwa macho, na kuchukua tahadhari zote zinazohitajika.
Uchaguzi Cameroon: Maandamano ya vurugu yazidi huko Douala - ripoti
Maandamano yamezuka huko Douala, mji mkuu wa kiuchumi wa Cameroon, kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Picha zilizochapishwa na kituo cha habari cha Mimi Mefo Infos, zinaonyesha watu kadhaa wakikimbia barabarani, wakiimba jina la Issa Tchiroma Bakary kwa pamoja.
Shirika la Habari la Cameroon lilichapisha video, nje inayoonyesha jengo la baraza lililoharibiwa, linalodaiwa kushambuliwa na waandamanaji.
Rais mteule Paul Biya bado hajawahutubia wananchi wa Cameroon baada ya kuchaguliwa tena Jumatatu, lakini chama tawala kimepongeza ushindi wake "chini ya ishara ya ukuu na matumaini" katika machapisho ya mtandaoni.
Hakujawa na maoni yoyote kutoka kwa serikali kuhusu ripoti kwamba watu wenye silaha wamefyatua risasi na kuua watu wawili karibu na nyumba ya mshindi wa pili Issa Tchiroma Bakary.
Akizungumza katika kumuunga mkono rais siku ya Jumatatu, mpiga kura kwa jina Serge Pascal Eyango aliambia shirika la habari la Reuters:
"Kati ya mikoa 10 ya Cameroon, Rais wa Jamhuri alishinda saba. Na mgombea ambaye alijaribu kufanya jambo muhimu katika mikoa mitatu, Issa Tchiroma [Bakary], pongezi kwake. "Lakini... inathibitisha ni kwa kiasi gani watu wa Cameroon bado wanamuunga mkono mkuu wao wa nchi. Hilo ndilo jambo muhimu. Yeye ni mtu wa amani, sura inayounganisha, baba kwa watoto, na bado tuna matumaini makubwa kwake. Hilo ndilo tu tulilotarajia."
Mali yafunga shule na vyuo vikuu nchini kote kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Milolongo mirefu ya magari na watu imeshuhudiwa katika vituo vya mafuta vya Bamako katika wiki za hivi karibuni
Serikali ya Mali imesimamisha masomo katika shule na vyuo vikuu vyote nchini humo kufuatia uhaba mkubwa wa mafuta uliosababishwa na wanamgambo kuzuia uingizaji wa bidhaa za mafuta nchini.
Waziri wa Elimu, Amadou Sy Savane, ametangaza kuwa taasisi zote za elimu zitasalia kufungwa hadi tarehe 9 Novemba, akieleza kuwa walimu, wahudumu na wanafunzi wamekosa usafiri kutokana na hujuma zinazofanywa na wanamgambo hao.
Waziri Savane aliongeza kuwa serikali inafanya kila juhudi kumaliza mzozo huo ili masomo yaanze tena kuanzia tarehe 10 mwezi Novemba.
Kwa wiki kadhaa sasa, Mali imekumbwa na uhaba wa mafuta, hasa katika mji mkuu Bamako, baada ya wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wanaohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda kuanza kushambulia malori ya mafuta katika barabara kuu za nchi hiyo.
Kwa kuwa Mali haina bandari, bidhaa zote za mafuta husafirishwa kwa malori kutoka nchi jirani kama Senegal na Ivory Coast.
Hali hiyo imesababisha foleni ndefu katika vituo vya mafuta jijini Bamako, huku barabara ambazo kwa kawaida huwa na shughuli nyingi sasa zikiwa kimya na tupu.
Serikali ya kijeshi inayoongozwa na Jenerali Assimi Goïta, ambaye alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 2021, iliwahakikishia raia hivi karibuni kwamba uhaba huo wa mafuta ni wa muda mfupi.
Hata hivyo, hali imeendelea kuzorota zaidi ya ilivyotarajiwa. Wiki iliyopita, ubalozi wa Marekani mjini Bamako ulitangaza kuwa utaondoa wafanyakazi wake wasio wa lazima pamoja na familia zao kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama na athari za uhaba huo wa mafuta, ambao umelemaza usafiri na huduma za umeme nchini.
Licha ya jeshi kushika hatamu za uongozi, wanamgambo wenye misimamo mikali wameendelea kudhibiti maeneo mengi ya kaskazini na mashariki mwa Mali.
Baada ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani (MINUSMA) na vikosi vya Ufaransa kuondoka nchini humo, serikali ya Jenerali Goïta sasa inategemea mamluki wa Urusi kushughulikia masuala ya usalama nchini humo.
Watu wapigwa risasi nje ya nyumba ya Tchiroma Bakary - ripoti
Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi karibu na makazi ya Tchiroma Bakary katika mji wa Garoua, mwandishi wa habari wa eneo hilo aliyepo kwenye eneo la tukio ameiambia BBC.
Milio ya risasi ilisikika wakati mwandishi wa habari akiongea kwenye simu.
Wakati huo huo, Tchiroma Bakary aliandika kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba risasi zilikuwa zikipigwa kuelekea kwa raia waliokusanyika nje ya nyumba yake.
Mamlaka bado haijatoa maoni yoyote kuhusu ripoti hizo.
Habari za hivi punde, Paul Biya atangazwa mshindi wa uchaguzi Cameroon
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Rais Paul Biya atangazwa mshindi wa Urais nchini Cameroon
Baraza la katiba la Cameroon limemtangaza Rais aliye madarakani Paul Biya kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa karibu asilimia 54% ya kura.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Biya alipata asilimia 53.66 ya kura, huku mpinzani wake mkuu na aliyekuwa mshirika wake wa zamani, Issa Tchiroma Bakary, akipata asilimia 35.19.
“Mgombea Biya Paul ametangazwa kuwa Rais wa Jamhuri, baada ya kupata wingi wa kura halali zilizopigwa,” alisema Clement Atangana, Rais wa Baraza la Kikatiba.
Ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 57.76, huku asilimia 42.24 wakijiondoa katika mchakato wa kupiga kura.
Jumla ya watu zaidi ya milioni nne walishiriki katika uchaguzi huo. Wagombea kumi walikuwa wakigombea urais, na Biya ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote tangu aanze kutawala mwaka 1982 alionekana tangu awali kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Hata hivyo, matokeo haya yanapingana na madai ya Issa Tchiroma, ambaye kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.
Katika mahojiano ya hivi karibuni na BBC, Tchiroma alisisitiza kwamba amemshinda bosi wake wa zamani, Paul Biya, akidai kwamba uchaguzi ulighubikwa na udanganyifu mkubwa na dosari za wazi katika uendeshaji wake.
Madai hayo yamechochea hasira na maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo hadi sasa watu wasiopungua watano wameripotiwa kuuawa.
Waandamanaji wengi wamekuwa wakisisitiza madai ya Tchiroma kwamba yeye ndiye mshindi halali.
Serikali imetaja maandamano hayo kuwa haramu, na imewakamata viongozi kadhaa wa upinzani pamoja na wanaharakati.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa wimbi hili jipya la maandamano linaweza kuisukuma Cameroon taifa lililokuwa likijulikana kwa utulivu wake wa kisiasa kuelekea kwenye ghasia na machafuko ya kisiasa, endapo matokeo ya uchaguzi hayatakubalika kama yanayoakisi matakwa ya wananchi.
Biya iliingia madarakani kwa mara ya kwanza mnamo 1982, matokeo haya ya uchaguzi sasa yanamaanisha kuwa ataendelea kutawala hadi 2032.
Vikosi vya kimataifa havitakubali kulazimisha amani Gaza - Mfalme wa Jordan
Maelezo ya picha, Mfalme wa Jordan
Nchi nyingi hazitakubali jukumu la “kulazimisha” amani Gaza endapo zitatumwa chini ya mpango wa kusitisha mapigano wa rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Mfalme Abdullah wa Jordan katika mahojiano maalum na BBC.
Kupitia mpango huo wa amani wa vipengele 20, Marekani ilipendekeza kwamba mataifa ya Kiarabu na washirika wa kimataifa yatoe vikosi maalum vya uthabiti ambavyo “vitatoa mafunzo na msaada kwa vikosi vya polisi vya Wapalestina vilivyothibitishwa Gaza, na vitashauriana na Jordan na Misri, ambazo zina uzoefu mkubwa katika masuala ya usalama wa kikanda.”
Mpango huo pia unaitaka Hamas kuvunja silaha na kuachia madaraka ya kisiasa katika eneo hilo.
“Ni mamlaka gani yatakayotolewa kwa vikosi vya usalama ndani ya Gaza? Tunatumaini kwamba itakuwa operesheni ya kulinda amani, kwa sababu kama itakuwa ya kulazimisha amani, hakuna nchi itakayopenda kujihusisha nayo,” alisema Mfalme Abdullah.
Katika mahojiano hayo maalum kwa kipindi cha BBC Panorama, Mfalme huyo alisema Jordan na Misri ziko tayari kusaidia katika kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Wapalestina.
“Kulinda amani ni kuwasaidia polisi wa wenyeji yaani Wapalestina jambo ambalo Jordan na Misri ziko tayari kulifanya kwa wingi, ingawa linahitaji muda. Lakini ikiwa tutakuwa tunazunguka Gaza kwenye doria tukiwa na silaha, hiyo si hali ambayo taifa lolote lingependa kujihusisha nayo,” aliongeza.
Kauli za Mfalme Abdullah zinaakisi wasiwasi wa Marekani na mataifa mengine kuhusu hatari ya kuvutwa katika mzozo unaoendelea kati ya Hamas na Israel, au kati ya Hamas na makundi mengine ya Kipalestina.
Mfalme huyo pia alisisitiza kwamba Jordan haitatuma wanajeshi wake Gaza, akieleza kuwa nchi yake “iko karibu sana kisiasa” na mzozo huo.
Zaidi ya nusu ya wananchi wa Jordan ni wenye asili ya Kipalestina, na kwa miongo kadhaa taifa hilo limewapokea wakimbizi wa Kipalestina wapatao milioni 2.3 waliokimbia vita vya awali na Israel idadi kubwa zaidi katika eneo hilo.
Alipoulizwa kama ana imani kwamba Hamas itatekeleza ahadi yake ya kuachana na siasa katika ukanda wa Gaza, alijibu: “Siwajui moja kwa moja, lakini wale wanaofanya kazi kwa karibu nao – Qatar na Misri – wana matumaini makubwa kwamba watatii makubaliano hayo.”
Mfalme Abdullah alionya kuwa mustakabali wa amani Mashariki ya Kati unategemea kutatuliwa kwa mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina.
“Iwapo hatutatua tatizo hili, iwapo hatutapata mustakabali wa pamoja kwa Waisraeli na Wapalestina na kuimarisha uhusiano kati ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na Israel, basi tutaangamia,” alisema.
Kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Trump kulifuatwa na kuachiliwa kwa mateka 20 wa Kiyahudi waliokuwa hai kutoka Gaza, huku juhudi zikiendelea kurejesha miili ya waliouawa.
Israel nayo iliwaachilia wafungwa 250 wa Kipalestina waliokuwa wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo mauaji na mashambulizi dhidi ya raia wa Israel, pamoja na takribani wafungwa 1,700 kutoka Gaza waliokuwa wakizuiliwa bila mashitaka.
UN yaomba njia salama kwa raia waliokwama katika mji wa el-Fasher, Sudan
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Maelezo ya picha, Mamia kwa maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao kwa sababu ya mzozo nchini Sudan
Umoja wa Mataifa umezitaka pande zinazopigana nchini Sudan kuhakikisha raia waliokwama mjini el-Fasher wanapatiwa njia salama ya kuondoka, baada ya wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) kutangaza kuwa wametwaa udhibiti wa kambi kuu ya jeshi katika mji huo.
Jeshi la Sudan halijathibitisha kupoteza kambi hiyo, jambo ambalo, likithibitishwa, litakuwa ushindi mkubwa kwa RSF katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema mapigano hayo mapya ni “ongezeko baya mno la machafuko,” na kuongeza kuwa mateso wanayopitia raia ni “yasiyovumilika,” kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
El-Fasher, ambayo ni ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan katika eneo pana la magharibi mwa Darfur, imekuwa chini ya mzingiro wa RSF na washirika wake kwa zaidi ya miezi 18.
Mapigano makali yamezuka tangu Jumamosi, baada ya wapiganaji wa RSF kuteka makazi ya gavana wa jimbo la Kaskazini mwa Darfur.
Video zilizothibitishwa na BBC kutoka mitandao ya kijamii zinaonyesha wapiganaji wa RSF wakisherehekea baada ya kuteka makao makuu ya jeshi mjini el-Fasher.
RSF inadai kudhibiti mji mzima, lakini washirika wa kijeshi wa serikali katika eneo hilo wanasema mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya mitaa.
Kundi hilo limekosolewa kwa kushambulia raia kwa mabomu ya angani na kuwazuilia takribani watu 250,000, baada ya kuuzungushia mji huo ukuta wa udongo, hali iliyowaacha wengi katika njaa kali na kukosa msaada wa kibinadamu.
Mji wa el-Fasher sasa unatajwa kuwa moja ya maeneo yenye mapigano makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambapo Umoja wa Mataifa umeueleza kama “kitovu cha mateso.”
Afisa Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, alisema ameshtushwa sana na taarifa za vifo na mateso ya raia.
“Wapiganaji wanapozidi kusonga kuelekea katikati mwa mji na njia za kutoroka zikifungwa, mamia ya maelfu ya raia wamekwama wakiwa na hofu ya kushambuliwa, wakikabiliwa na njaa, bila chakula, huduma za afya, wala usalama,” alisema Fletcher kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Tangu machafuko kuanza, zaidi ya watu 150,000 wameuawa kote nchini, huku takribani watu milioni 12 wakiyakimbia makazi yao, hali ambayo Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa ni moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani.
Kwa sasa, jeshi la Sudan linadhibiti maeneo mengi ya kaskazini na mashariki mwa nchi, huku el-Fasher ikiwa mji wa mwisho mkubwa katika Darfur uliokuwa bado chini ya udhibiti wa serikali na washirika wake.
RSF, kwa upande wake, inadhibiti karibu eneo lote la Darfur na sehemu kubwa ya mkoa wa Kordofan, na imewahi kutangaza azma ya kuunda serikali pinzani mjini el-Fasher pindi itakapodhibiti eneo hilo kikamilifu.
Muunganisho wa intaneti umekuwa si dhabiti katika siku za hivi majuzi nchini Cameroon.
Siku ya Alhamisi, mfuatiliaji wa mtandao wa NetBlocks aliripoti "kuvurugika kwa muunganisho wa intaneti" ambao unaweza "kuzuia utangazaji wa matukio mashinani huku kukiwa na wito wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais huku Rais Biya akitafuta kuongeza miaka 43 madarakani".
Siku hiyo hiyo, kampuni ya kitaifa ya mawasiliano ya Camtel ilisema kumekuwa na "tukio la kiufundi".
Wakati huo huo, barabara za jiji la Bamenda, magharibi mwa nchi inayozungumza Kiingereza, hazina watu na raia wako ndani ya nyumba.
Mapema sana asubuhi ya leo, mashabiki wa michezo walikuwa mitaani; wengine wakitembea kwa kasi huku wengine wakikimbia.
Hata hivyo, kufikia saa 10:00 (09:00 GMT) mitaa ilikuwa haina watu.
Wanajeshi wapo kwenye makutano yote makubwa.
Uwepo wao unaonekana unanuiwa kuzuia maandamano yoyote yanayohusiana na uchaguzi.
Kwa sasa, mawingu meusi yanaonekana yakikusanyika, kuashiria mvua mchana.
Rais wa Argentina apata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Javier Milei ameshinda karibu 41% ya kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Argentina
Rais wa Argentina, Javier Milei amekiongoza chama chake katika ushindi wa
kishindo katika uchaguzi wa katikati ya muhula siku ya Jumapili, baada ya miaka
miwili ya kwanza ya urais wake wa kubana matumizi na mageuzi ya soko huria.
Chama chake, La Libertad Avanza, kimepata karibu asilimia 41 ya kura,
kikichukua viti 13 kati ya 24 vya Seneti na 64 kati ya viti 127 vya mabunge ya
chini vilivyokuwa vikiwaniwa.
Mafanikio yake yatarahisisha zaidi kuendelea na mpango wake wa
kupunguza matumizi ya serikali na kudhibiti uchumi katika taifa hilo la Amerika Kaskazini,
Kabla ya upigaji kura, mshirika wa Milei, Donald Trump, aliweka
wazi kuwa msaada uliotangazwa hivi karibuni na Marekani wa dola bilioni 40
kwa Argentina utategemea ushindi wa Milei.
Wafuasi wa Milei walifurahia hilo, ingawa wakosoaji walimshutumu Donald
Trump kwa kuingilia kati uchaguzi wa Argentina.
Milei aliwaambia wafuasi wake waliokuwa
wakishangilia: "Lazima tuendelee na mageuzi ambayo tumeyaanzisha ili kuibadilisha
historia ya Argentina... ili kuifanya Argentina kuwa kubwa tena."
Kabla ya chaguzi hizi chama chake kilikuwa na viti saba tu vya Seneti na
viti 37 katika bunge la chini.
Hiyo ilimaanisha mpango wake wa kubana matumizi na mageuzi ulikumbana na
vikwazo mbalimbali vya kisiasa.
Miswada yake ya kuongeza ufadhili kwa vyuo vikuu vya serikali, watu
wenye ulemavu na huduma ya afya ya watoto - yote ilibatilishwa na wabunge wa
upinzani.
Baada ya matokeo ya Jumapili, mamia ya wafuasi wake walikusanyika,
wakishangilia, nje ya hoteli moja mjini Buenos Aires ambako alikuwa akitazama
matokeo.
Chaguzi hizi zilikuwa mtihani wa kwanza kwa umaarufu wa Rais Milei tangu
aingie madarakani mwaka 2023, na kuahidi kupunguza matumizi ya serikali.
Tangu wakati huo amepunguza bajeti ya elimu, pensheni, afya,
miundombinu, na ruzuku, na kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi wa sekta ya
umma.
Waungaji mkono wake, ikiwa ni pamoja na Trump, wanampongeza kwa
kudhibiti mfumuko wa bei - kupunguza nakisi, na kurejesha imani ya wawekezaji.
Wakosoaji wake wanasema taitizo ni kwamba watu wengi wamepoteza
kazi, kushuka kwa uzalishaji, kuporomoka kwa huduma za umma, kuanguka kwa uwezo
wa watu wa kununua na hatari ya kuporomoka kwa uchumi.
Mfalme wa Uingereza kuhudhuria tukio rasmi la LGBT+
Chanzo cha picha, Rank Outsiders
Maelezo ya picha, Marufuku ya wapenzi wa jinsia moja katika jeshi ilibatilishwa baada ya kampeni ya muda mrefu kutoka kwa kundi la maveterani liitwalo Rank Outsiders.
Mfalme Charles III wa Uingereza, atazindua kumbukumbu ya sanamu la wapenzi wa jinsia moja, walio
na jinsia mbili na waliobadili jinsia wanaohudumu katika jeshi, katika shughuli yake ya kwanza rasmi ya
kuunga mkono jumuiya ya LGBT+.
Ilikuwa ni kinyume cha sheria kuwa mpenzi wa jinsia moja katika jeshi la
Uingereza hadi 2000, na wale ambao walikuwa wapenzi wa jinsia moja - au walioshukiwa
- walikabiliwa na uchunguzi, kufutwa kazi na katika baadhi ya kesi kufungwa.
Kumbukumbu hiyo, iliyopewa jina la "barua ya wazi," ni kwa
watu kutoka jumuiya ya LGBT+ ambao wanahudumu au walihudumu katika jeshi .
Sanamu ya shaba, liobuniwa na kikundi cha wasanii wa Norfolk Abraxas
Academy, itazinduliwa rasmi leo katika Makumbusho ya Taifa huko Staffordshire.
Mradi wa kumbukumbua unaoongozwa na Fighting With Pride, shirika la
usaidizi la wanajeshi wastaafu wa LGBT+ lililoanzishwa ili kupigania haki na
kuunga mkono wale walioathiriwa na marufuku ya jeshini.
Serikali ya Cameroninasema watu wanne wameuawa wakati wa maandamano ya Jumapili katika mji mkuu wa kiuchumi wa Douala, huku hofu ikiongezeka kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Katika taarifa, Gavana wa mkoa wa Littoral ambao ni kitovu cha uchumi, amesema waandamanaji walishambulia vituo vya polisi na polisi, kwa nia ya kuvichoma moto na vikosi vya usalama vilizuia majaribio haya.
"Katika mapambano hayo, kwa bahati mbaya watu wanne walipoteza maisha," amesema Gavana Samuel Dieudonné Diboua.
Pia amelaani maandamano hayo ambayo akiyaeleza kuwa ni "vurugu zilizopangwa" ambazo ni shambulio kubwa kwa utulivu wa umma na usalama wa taifa.
Zikiwa zimesalia saa 24 tu kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, mamia ya waandamanaji na wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary walijitokeza mitaani kote nchini na nje ya nchi kukemea kile wanachosema ni udanganyifu wa uchaguzi.
Tchiroma anadai ushindi katika uchaguzi huo, licha ya onyo kutoka kwa serikali.
Marekani kuacha kulipia chakula cha msaada kwa raia wake
Chanzo cha picha, EPA
Msaada wa chakula unaowanufaisha Wamarekani zaidi ya milioni 40 hautatolewa
kuanzia Novemba kutokana na kusitishwa shughuli za serikali ya Marekani,
kulingana na Wizara ya Kilimo ya nchi hiyo.
Wizara hiyo imesema hakuna msaada, katika tovuti yake na kuwalaumu
wawakilishi wa Democratic katika Seneti kwa mkwamo huo.
Mpango wa Usaidizi wa Lishe (Snap) humnufaisha Mmarekani mmoja kati ya
wanane.
Mapema mwezi huu, utawala wa Trump ulikataa kutumia hazina ya dharura
ambayo ingeendeleza kutoa msaada huo, ikisema pesa hizo zinahitajika kwa
dharura zinazoweza kutokea kama vile majanga ya asili.
Democratic kimemlaani Rais Donald Trump kwa
kukataa kutumia hazina ya dharura.
"Pengine hili ni kosa la kikatili na kinyume cha sheria ambalo
utawala wa Trump unalifanya," wabunge katika Congress, Rosa DeLauro na
Angie Craig walisema katika taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa.
Pia walimkosoa Trump kwa kutoa msaada kwa Argentina na kujenga ukumbi
mpya wa White House wakati shughuli za serikali zimefungwa.
Kulingana na taasisi ya fikra tunduizi ya Budget and Policy Priorities (CBPP), hazina
ya dharura ingegharamia takriban 60% ya gharama hizo kwa mwezi mmoja.
Snap hufanya kazi kwa kuwapa watu kadi za benki wanazoweza kuzitumia
kununua bidhaa muhimu za nyumbani.
Familia ya watu wanne kwa wastani hupokea dola za kimarekani 715 (£540)
kwa mwezi, kulingana na CBPP, ambapo ni sawa na dola 6 (£4.50) kwa siku kwa kila mtu.
Majimbo ndio yanasimamia programu hii, huku ufadhili mwingi ukitoka kwa
serikali ya shirikisho.
Majimbo kadhaa yameahidi kutumia fedha zao wenyewe kufidia upungufu
wowote, hata hivyo serikali ya shirikisho imeonya kuwa fidia hiyo haitarejeshwa.
Baadhi ya majimbo, ikiwa ni pamoja na Massachusetts - ambapo watu milioni
moja wanatarajiwa kupoteza msaada huo - wamesema hawana pesa za kutosha kufidia
ukosefu wa fedha.
Kufungwa kwa shughuli za serikali ya Marekani kumeingia siku yake ya 26
Jumapili, na kuufanya kuwa ndio ufungaji wa pili kwa ukubwa katika historia.
Maandamano ya vurugu yatokea Cameroon kabla matokeo ya uchaguzi
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wafuasi wa mgombea wa upinzani Issa Tchiroma Bakary wameandamana katika miji kadhaa nchini Cameroon
Mamia ya waandamanaji wamepambana na vikosi vya usalama katika miji
kadhaa kote nchini Cameroon, saa chache kabla ya matokeo ya uchaguzi wa urais
uliokuwa na upinzani mkubwa kutangazwa.
Polisi waliwarushia vitoa machozi na maji ya kuwasha wafuasi wa mgombea
wa upinzani Issa Tchiroma Bakary katika ngome yake ya Garoua, mji ulioko
kaskazini mwa nchi hiyo.
Waandamanaji hao walikuwa wakilaani kile walichosema ni mpango wa
chama tawala, Cameroon People's Democratic Movement (CPDM), "kuiba
ushindi" kutoka kwa kiongozi wa upinzani.
Tchiroma Bakary amesisitiza kwamba ameshinda uchaguzi wa urais
uliofanyika tarehe 12 Oktoba, akipinga Rais aliye madarakani Paul Biya kwa miaka 43 kuendelea kushikilia madaraka.
Chama cha CPDM kimetupilia mbali madai hayo.
Maandamano hayo yanakuja baada ya Tchiroma Bakary kutoa wito kwa wafuasi
wake nchini humo na wale walio njea kuandamana kwa amani "kuikomboa
Cameroon."
Serikali imepiga marufuku mikusanyiko hadi Jumatatu, wakati baraza la
katiba la Cameroon litakapopanga kutangaza matokeo.
Huko Garoua, maandamano yalianza kwa amani lakini yakageuka ghasia
wakati vikosi vya usalama viliporusha vitoa machozi mitaani ili kuwatawanya
mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kumuunga mkono Tchiroma Bakary.
Mwandamanaji mmoja alionekana akiwa amebeba bango la kumtaka Rais wa
Marekani Donald Trump kuwasaidia.
"Tuko hapa kudai ushindi wetu. Tunafanya maandamano ya amani,
ambayo ni haki ya kiraia kwa Wacameruni wote - kwa kila mtu," muandamanaji
mwingine alisema.
Wafuasi pia waliingia mitaani katika mji wa kusini-magharibi wa Douala.
"Tunamtaka Tchiroma, tunamtaka Tchiroma," waandamanaji waliimba,
shirika la habari la Reuters linaripoti.
Tchiroma Bakary awali aliambia BBC kwamba hatakubali kuibiwa kura. Alisema timu yake imekusanya taarifa jumla kulingana na matokeo ya vituo
vya kupigia kura.
Katika taarifa yake ya video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii,
Tchiroma Bakary alisema ameshinda uchaguzi huo kwa takriban asilimia 55 ya kura.
Waziri huyo wa zamani wa serikali mwenye umri wa miaka 76 aliachana na Biya
mwenye umri wa miaka 92, ambaye anawania muhula mwingine baada ya miaka 43
madarakani.
CPDM imetupilia mbali madai ya ushindi wa Tchiroma Bakary na maafisa
kadhaa wameelezea kuwa ni kinyume cha sheria kwa sababu ni baraza la katiba
pekee ndilo linaloweza kutangaza matokeo rasmi.
Wafuasi wa upinzani wamedai kuwa uchaguzi wa Oktoba 12 ulikumbwa na
dosari, ikiwa ni pamoja na kujazwa kura katika maboksi.
Majaji katika baraza la katiba wametupilia mbali kesi nane, wakisema
hazina ushahidi wa kutosha au haina mamlaka ya kubatilisha matokeo.
Tchiroma Bakary alikataa kuwasilisha malalamiko katika baraza hilo,
ambalo majaji wake wameteuliwa na Biya, na kuchagua badala yake kujitangaza
kuwa "rais halali."
Mzaliwa wa Garoua, Tchiroma Bakary alikuwa mwanafunzi wa uhandishi nchini
Ufaransa kabla ya kurejea Cameron kufanya kazi katika kampuni ya kitaifa ya
reli.
1984, alitupwa jela, akishutumiwa kuhusika katika jaribio la kumwondoa
madarakani Rais Biya. Licha ya kukana shitaka hilo na hakuwahi kupatikana na
hatia, Tchiroma Bakary alikaa jela miaka sita.
Pia aliwahi kuwa waziri wa mawasiliano kuanzia 2009 hadi 2019.
Akiwa msemaji wa serikali, aliitetea serikali ya Biya wakati wa
machafuko kama vile uasi wa Boko Haram, na jeshi lilipotuhumiwa kuwaua raia.
Lakini mwezi Juni, miezi minne tu kabla ya uchaguzi mkuu, Tchiroma
Bakary alibadilika, akajiuzulu kutoka serikalini na kutangaza kuwa atachuana na
Biya kuwania urais.
Marekani na China zakubaliana mfumo wa kibiashara kabla ya mkutano wa Trump na Xi
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Donald Trump na mwenzake wa China Xi Jinping wanatarajiwa kufanya mazungumzo nchini Korea Kusini.
Marekani
na China zimekubaliana mfumo wa kibiashara ambao utajadiliwa wakati viongozi
wao watakapokutana baadaye wiki hii, waziri wa fedha wa Marekani amesema.
Scott
Bessent aliiambia CBS, mfumo huo wa makubaliano ni pamoja na "makubaliano ya
mwisho" kuhusu shughuli za TikTok Marekani na kulegeza kamba China juu
ya udhibiti wake wa rasilimali adimu.
Pia amesema
hatarajii ushuru wa 100% kwa bidhaa za China kama Rais wa Marekani Donald Trump
alivyotishia, wakati huo huo China itaanza tena ununuzi mkubwa wa soya kutoka
Marekani.
China na Marekani zinajaribu kuepusha kuongeza vita vya kibiashara kati ya mataifa
hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani.
Trump
na rais wa China Xi Jinping wanatarajiwa kufanya mazungumzo siku ya Alhamisi
nchini Korea Kusini
Bessent
alikutana na maafisa wakuu wa biashara wa China kando ya mkutano wa kilele wa
Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (Asean) nchini Malaysia, ambao
Trump pia anahudhuria kama sehemu ya ziara yake Asia.
Beijing
imesema kulikuwa na majadiliano mazuri.
Serikali
ya China imesema katika taarifa kwamba timu zote mbili za mazungumzo
"zilifikia makubaliano juu ya sintofahamu zao.
Wawili wakamatwa kwa wizi katika jumba la makumbusho Ufaransa
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Maafisa wa polisi wa Ufaransa wanachunguza wizi katika Jumba la Makumbusho la Louvre, jijini Paris, Oktoba 19, 2025.
Washukiwa wawili wamekamatwa kwa wizi wa vito vya thamani katika
jumba la makumbusho la Louvre jijini Paris, Ufaransa, vyombo vya habari vya nchi
hiyo vinasema.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema mmoja wa watu hao ametiwa
mbaroni alipokuwa akijiandaa kupanda ndege katika uwanja wa ndege wa Charles de
Gaulle.
Vito vyenye thamani ya dola za kimarekani milioni 102, viliibiwa katika jumba
la makumbusho linalotembelewa zaidi duniani Jumapili iliyopita, wakati wezi
wanne waliokuwa na zana za kisasa walipovamia jengo hilo mchana kweupe.
Waziri wa sheria wa Ufaransa amekiri kuwa itifaki za usalama "zilishindwa,"
na kuiacha nchi hiyo katika "picha mbaya."
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Paris imesema, watu hao walikamatwa
Jumamosi jioni, bila kutaja ni watu wangapi wametiwa mbaroni.
Mmoja wa washukiwa alikuwa akijiandaa kusafiri kuelekea Algeria, vyanzo kutoka
polisi vimeviambia vyombo vya habari vya Ufaransa, huku ikifahamika kuwa
mwengine alikuwa akienda Mali.
Polisi wanaweza kuwazuilia na kuwahoji kwa hadi saa 96.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ufaransa siku ya Jumapili,
DNA iliyopatikana katika eneo la wizi ilipelekea kutambuliwa kwa mmoja wa
washukiwa.
Genge hilo liliacha vitu kadhaa, ikiwa ni pamoja na glavu na koti.
Pia iliripotiwa hapo awali kwamba walidondosha taji ambalo lilikuwa la
Empress Eugenie, mke wa Napoleon III.
Mwendesha mashtaka wa Paris alikosoa "kufichuliwa mapema" kwa
habari zinazohusiana na kesi hiyo, akiongeza kuwa zinazuia juhudi za kurejeshwa
kwa vito hivyo na kuwapata wezi.
Inasemekana wezi hao walifika saa 09:30 (08:30 GMT), muda mfupi baada ya
jumba la makumbusho kufunguliwa.
Washukiwa walifika na ngazi ya umeme iliyokuwa kwenye gari na kuikunjua
hadi kulifikia dirisha la roshani katika ghorofa ya kwanza ya Gallery ya Apollo.
Wawili kati ya wezi hao waliingia kwa kukata dirishani wakiwa na mashine
za kisasa.
Kisha waliwatishia walinzi, ambao walitoka nje ya jengo hilo, na kukata vioo
vya masanduku mawili yaliyohifadhi vito.
Ripoti ya awali imefichua kuwa chumba kimoja kati ya vitatu katika eneo
la jumba la makumbusho lililovamiwa hakikuwa na kamera za CCTV, kulingana na
vyombo vya habari vya Ufaransa.
Polisi wa Ufaransa wanasema wezi hao walikuwa ndani ya jumba kwa dakika nne
na kutoroka kwa pikipiki mbili zilizokuwa zikingoja nje saa 09:38.
Wataalamu wameelezea wasiwasi wao kwamba vito hivyo tayari huenda vimevunjwa
vunjwa na kuwa vipande vipande.
Dhahabu na fedha zinaweza kuyeyushwa na kukatwa na kuwa vijiwe vidogo
ambapo haitawezekana kujua kuwa viliibiwa katika wizi huo, afisa wa upelelezi wa
Uholanzi Arthur Brand aliambia BBC.
Hatua za usalama tangu wakati huo zimeimarishwa karibu na taasisi za
kitamaduni za Ufaransa.
Kampuni ya Louvre imehamisha baadhi ya vito vyake vya thamani hadi Benki
ya Ufaransa kufuatia wizi huo. Sasa vitahifadhiwa katika chumba salama zaidi
cha Benki, mita 26 (85ft) chini ya ghorofa katika makao makuu ya benki katikati
mwa Paris.
Misri na Msalaba Mwekundu zaungana kutafuta miili ya mateka Gaza
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Maelezo ya picha, Matrekta ya Misri yanavuka kuingia Ukanda wa Gaza
Timu kutoka Misri na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC)
zimeruhusiwa kutafuta miili ya marehemu waliotekwa nyara wakati wa mashambulizi
ya Oktoba 7, Israel imethibitisha.
Serikali ya Israel imesema timu hizo zimeruhusiwa kutafuta zaidi ya eneo la "mstari wa njano,” amablo linadhibitiwa na Jeshi la Ulinzi la
Israel (IDF) huko Gaza.
Wakati huo huo, siku ya Jumapili, vyombo vya habari vya Israel
viliripoti kwamba wanachama wa Hamas pia wameruhusiwa kuingia katika eneo
linalodhibitiwa na IDF la Gaza kusaidia msako huo, pamoja na timu za ICRC.
Hamas imekabidhi miili ya mateka 15 kati ya 28 wa Israel chini ya awamu
ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Marekani.
Kundi hilo limesema sasa linashirikiana na mamlaka za Misri.
Donald Trump ameitaka Hamas kurejesha miili "haraka, au nchi
nyingine zinazohusika katika mpango huu wa amani zitachukua hatua."
Msemaji wa Israel alisema timu ya Misri imeruhusiwa kufanya kazi na ICRC
kutafuta miili hiyo, na itatumia matreka ya kuchimba na magari makubwa kutafuta
miili zaidi ya "mstari wa njano."
Mstari wa " njano" unaashiria mpaka wa kaskazini,
kusini na mashariki mwa Gaza, eneo ambalo Israeli ilijiondoa, kama sehemu ya
hatua ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Baada ya zaidi ya miaka miwili ya mashambulizi makali ya Israel, Umoja
wa Mataifa unakadiria kuwa 84% ya eneo la Gaza ni kifusi.
Hamas inasema inajitahidi kadiri iwezavyo kupata miili ya mateka, lakini
inakabiliwa na ugumu wa kuipata chini ya vifusi vya majengo yaliyolipuliwa na
jeshi la Israel huko Gaza.
'Trump anataka kuipindua serikali’ – Afisa wa Venezuela
Rais wa Marekani Donald Trump anataka kuigeuza Venezuela kuwa
"koloni" la Marekani, Mwanasheria Mkuu wa Venezuela ameiambia BBC.
Tarek William Saab alisema siku ya Jumapili kwamba wito wa mabadiliko ya
utawala nchini Venezuela ni mbinu ya kutaka kunyakua maliasili za nchi yake,
ikiwa ni pamoja na akiba ya dhahabu, mafuta na shaba.
Mshirika huyo wa karibu wa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro, Saab anasema
"hakuna shaka" Marekani inajaribu kuipindua serikali ya Venezuela,
akiongeza kuwa ni jaribio la hivi punde katika msururu mrefu wa majaribio kama
hayo "yaliyofeli".
Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayamtambui Maduro kama kiongozi
halali wa Venezuela, baada ya uchaguzi uliopita wa 2024 kukosolewa na wengi
kuwa haukuwa huru na wa haki.
Trump pia amerudia mara kwa mara uwezekano wa kile alichokiita "operesheni
za ardhini" nchini Venezuela, na alisema wiki iliyopita kwamba Marekani
"inaangalia uwezekano wa operesehani za ardhini" baada ya kupata udhibiti
wa eneo la bahari."
Takriban watu 43 wameuawa katika mashamulizi dhidi ya boti zinazodaiwa
kuwa za dawa za kulevya katika pwani ya Amerika Kusini, baada ya utawala wa
Trump kuanzisha mashambulizi mapema Septemba kama sehemu ya vita vinavyodaiwa
kuwalenga walanguzi wa dawa za kulevya.
Wabunge wa Congress nchini Marekani kutoka pande zote mbili za vyama vya siasa, wameibua wasiwasi juu ya uhalali wa mashambulizi hayo na mamlaka ya
rais kutoa amri yafanyike.
Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham aliwaambia waandishi wa
habari Jumapili kwamba mashambulizi ya ardhini ni jambo linaloweza kutokea",
na Trump alimwambia kuwa anapanga kuwafahamisha wabunge wa Congress
kuhusu operesheni za baadaye za kijeshi atakaporejea kutoka Asia.
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuvamiwa kwa ardhi ya Venezuela, Saab ameiambia
BBC "haipaswi kutokea, lakini tumejitayarisha."
Aliongeza kuwa Venezuela "bado iko tayari kuanza tena
mazungumzo" na Marekani, licha ya mashambulizi "haramu" dhidi ya
ulanguzi wa dawa za kulevya.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Marekani imekuwa ikiendelea
kujenga kikosi cha meli za kivita, ndege za kivita, wanajeshi wa majini, ndege
za kijasusi, na ndege zisizo na rubani katika visiwa vya Caribbean, kama sehemu
ya kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya na "magaidi wa
mihadarati."