Papa Leo XIV: 'Rafiki yangu Bob - Papa mpya'

Chanzo cha picha, Robert Karanja Ireri
Kwa Padri Robert Karanja Ireri, itachukua muda kuzoea kumwita rafiki yake Robert Prevost kwa jina lake jipya, Papa Leo XIV.
Hadi alipochaguliwa , kama wengi, alimjua tu papa mpya kama Bob Prevost.
"Alikuwa Big Bob na mimi ni Little Bob," Padri Karanja aliambia BBC. "Alikuwa mmoja wa washiriki wetu, kama baba kwetu, ndugu, rafiki, katika kusanyiko moja."
Padri Karanja ni kasisi wa kanda wa Shirika la Mtakatifu Augustino nchini Kenya.
"Bob mdogo" alikutana kwa mara ya kwanza na Papa Leo XIV katika kijiji chake cha Ishiara, Kenya, ambako kuna dayosisi ya mapadri wa shirika la Waagustino.
"Ilipendeza kusikia watu wakiniambia, 'Yeye ni kiongozi wa Waagustino duniani,' kwa sababu alionekana kuwa mtu mnyenyekevu na sikuzoea kuona viongozi wa namna hiyo," alisema.
"Naweza kusema yeye ni mtu mnyenyekevu sana, msikilizaji mzuri na rahisi kuelewana naye."
Wanaume hao wawili walikua marafiki na wanaendelea kuwasiliana hadi leo kupitia WhatsApp. Padre Karanja anamuelezea Papa kama "mzungumzaji mzuri sana."
"Niliendelea kuwasiliana naye. Mara ya mwisho nilipozungumza naye ilikuwa wakati wa salamu za Pasaka."
"Kwetu sisi Waagustino, uongozi ni mzigo. Nikiwa Muagustino, nilimuahidi maombi yangu."
Waagustino wanajulikana kwa maisha yao ya kijamii, kujitolea kwa maombi, na huduma kwa jamii katika masuala kama vile ya elimu na kazi ya parokia. Kuanzia 2001 hadi 2013, Papa Leo XIV alikuwa Mkuu wa Waagustino.
Mtakatifu Augustino alikuwa askofu wa Hippo, katika Algeria ya sasa, zaidi ya miaka 1,500 iliyopita.
Mara kwa mara katika Afrika

Chanzo cha picha, Robert Karanja Ireri
Kama sehemu ya kazi ya kimishonari ya Waagustino Papa Leo XIV alitembelea Afrika mara kadhaa, hivi karibuni zaidi nchini Kenya mwaka jana.
Padri Karanja ni mkuu wa Shule ya Kikatoliki ya Sacred Heartkatika Parokia ya Baba Dogo, viongani mwa jiji la Nirobi ambapo Papa Leo XIV alisaidia kujenga na kufungua shule ya chekechea mwaka wa 2011.
Pia alisaidia kutafuta fedha za kujenga Kanisa Katoliki la Sacred Heart na kliniki inayosaidia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Mnamo mwaka wa 2016, alitembelea Shirika la Agustino huko Abuja, Nigeria, wakati akihudumu kama askofu huko Peru.
Mnamo 2009, alizindua Chuo Kikuu cha Waagustino Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msukumo

Padre Karanja alimrudisha Papa Leo XIV katika parokia ya Baba Dogo mwezi Disemba mwaka jana kukutana na wanafunzi wa Shule ya Sacred Heart aliyosaidia kujenga.
Walishangaa kugundua kwamba tayari walikuwa wamekutana na kiongozi wao mpya wa kiroho.
Mwanafunzi mmoja, kwa jina Caleb alisema, "Mama yangu hakuamini. Nilimwambia alikuwa amesaidia kukuza shule yangu, na mama yangu alijivunia. Aliniambia nilikuwa na bahati ya kuwa katika shule hii."
Mwanafunzi mwenzake, Christopher, alitazama tangazo la kuchaguliwa kwa Papa mpya kwenye mtandao wa YouTube.
Anasema: "Tuliposikia habari hizo, tulifurahi sana kuona ni nani."
Padri Karanja alisema rafiki yake anakaribishwa tena Kenya.
"Akipata nafasi, tungependa arudi, na ninaamini hilo linawezakana, lakini tutampa muda wa kutulia."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












