Maelfu ya wafanyakazi wa umma mashakani baada ya Marekani kufunga shughuli zake rasmi

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuwafuta kazi wafanyakazi ambao ''sio muhimu''

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Abdalla Seif Dzungu na Mariam Mjahid

  1. Kuwa na wakati mwema msomaji wetu. Nakutakia usiku mwema.

  2. Snapchat yaanza kutoza malipo kwa hifadhi ya picha na video za zamani

    logo ya mtandao wa Snapchat

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Snapchat imetangaza kuanzisha malipo kwa watumiaji wanaohifadhi picha na video za zamani kwenye kipengele cha Memories, hatua inayozua upinzani kutoka kwa watumiaji wengi ambao wamejengeka na kumbukumbu kubwa ya machapisho yao.

    Tangu kuanzishwa kwa kipengele hicho mwaka 2016, Snapchat imeruhusu watumiaji kuhifadhi maudhui yao yaliyowekwa awali kwa kutumia Memories.

    Hata hivyo, kwa sasa, watumiaji wanaohifadhi kumbukumbu zinazozidi gigabyte tano (5GB) watahitaji kulipa ili kuendelea kuzihifadhi.

    Kampuni mama ya Snapchat, Snap, ilikataa kutoa maelezo kuhusu kiwango cha malipo kwa watumiaji wa Uingereza, ikisema mabadiliko haya yatatekelezwa kama sehemu ya “utambulisho wa taratibu wa kimataifa.”

    Watumiaji wengi kwenye mitandao ya kijamii wameonyesha kukasirishwa na hatua hii, wakilalamikia kampuni hiyo kwa kutamani faida nyingi.

    “Hatuwezi kuepuka kubadilika” Snap imekiri kuwa “sio rahisi kamwe kutoka kwa huduma ya bure kwenda kwenye kulipia,” lakini imeongeza kuwa mabadiliko haya ni ya lazima ili kuendeleza ubora wa kipengele cha Memories.

    Katika chapisho rasmi la blogi, kampuni hiyo ilisema: “Mabadiliko haya yatatufanya tuendelee kuwekeza katika kuboresha Memories kwa ajili ya jamii yetu yote.”

    Snap inasema kuwa tangu kuanzishwa kwa kipengele hicho, zaidi ya trilioni moja ya kumbukumbu zimehifadhiwa na watumiaji, na hivyo kudhihirisha umaarufu wa huduma hiyo.

    Kipengele cha Memories kinawawezesha watumiaji kuhifadhi picha na video zilizoshirikiwa awali kwa muda wa masaa 24 au chini ya hapo, na baadaye kuziandika tena kama kumbukumbu au “throwback”.

    Watumiaji ambao hifadhi zao zitazidi 5GB sasa watahimizwa kubadilisha kwa mpango wa hifadhi wa 100GB, ambao utagharimu $1.99 (pauni 1.48) kwa mwezi.

    Kwa watumiaji wa usajili wa Snapchat+ na Snapchat Premium, viwango vya juu vya hifadhi vitapatikana kwa malipo ya ziada.

    Kampuni hiyo inasema kuwa itatoa hifadhi ya muda wa miezi 12 kwa watumiaji wanaozidi kikomo cha 5GB, na pia itaruhusu kupakua yaliyohifadhiwa kwenye kifaa cha mtumiaji.

    Pamoja na maelezo ya Snap, watumiaji kwenye mitandao ya kijamii wameonyesha hasira kuhusu kulazimika kulipa kwa ajili ya hifadhi, hasa kwa wale ambao wamekuwa wakitumia huduma ya bure kwa miaka mingi na sasa wanakutana na gharama kubwa.

    Wengine wanakosoa hatua hii, wakisema kuwa ni “haki” na “unyoaji” kutoka kwa kampuni, kwani inawalazimisha kuchagua kati ya kulipa au kupoteza kumbukumbu zao.

    Drew Benvie, mwasisi na mkurugenzi mtendaji wa Battenhall, kampuni ya ushauri wa mitandao ya kijamii, aliiambia BBC News: “Njia ya kulipa kwa hifadhi kwenye mitandao ya kijamii ni mabadiliko yasiyozuilika.”

    Aliongeza kuwa, katika ulimwengu ambapo tunachapisha kidogo lakini tunaokoa zaidi, mabadiliko haya ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayojitokeza kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.

    Soma pia:

  3. Mamlaka za Mitaa nchini Ethiopia zaripoti vifo vya watu 30 baada ya kanisa kuporomoka

    Mamlaka za mitaa nchini Ethiopia zimesema kuwa angalau watu 30 wamefariki dunia baada ya kanisa lililokuwa likijengwa kuanguka.

    Zaidi ya watu 50 walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha mbalimbali.

    Tukio hili lilitokea mapema Jumatano asubuhi katika mji wa Arerti, umbali wa takribani kilomita 70 mashariki mwa mji mkuu Addis Ababa, kaskazini mwa Ethiopia.

    Waumini walikuwa wamekusanyika kwenye kanisa hilo kwa maadhimisho ya kila mwaka ya Sherehe ya Mtakatifu Maria.

    Mtaalamu mmoja katika hospitali ya eneo hilo amesema kuwa miongoni mwa waathirika ni watoto na wazee.

    Hospitali hiyo inaendelea kutafuta msaada kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu ili kutoa huduma kwa majeruhi.

    Inakadiriwa kuwa wengine wengi bado wanazungukwa na kifusi, na mamlaka zina wasiwasi kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi.

    Soma pia;

  4. Maambukizi ya Covid yaongezeka kutokana na aina mpya: Nimbus na Stratus

    Baadhi ya fedha hizo zitatumiwa kwa umnunuzi wa vifaa vya kupima corona

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Baadhi ya fedha hizo zitatumiwa kwa ununuzi wa vifaa vya kupima corona

    Ikiwa unasumbuliwa na koo linalouma sana pamoja na homa, huenda umeambukizwa mojawapo ya aina mpya za virusi vya Covid-19 vinavyoenea kwa kasi msimu huu wa vuli.

    Kwa mujibu wa mamlaka za afya nchini Uingereza, aina mpya za virusi—XFG (inayojulikana pia kama Stratus) na NB.1.8.1 (ijulikanayo kama Nimbus) ndizo zinazoongoza kwa kusababisha maambukizi kwa sasa.

    Wataalamu wa afya wanasema kuwa, kwa sasa, hakuna ushahidi kwamba aina hizi mpya ni hatari zaidi au husababisha madhara makubwa zaidi kiafya kuliko aina zilizopita.

    Hata hivyo, mabadiliko ya kimaumbile yaliyojitokeza kwenye virusi hivi yanaweza kuongeza uwezekano wa kuambukiza kwa urahisi zaidi.

    Dalili zinazojitokeza

    Virusi hubadilika tabia zao kadri vinavyosambaa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

    Mabadiliko hayo, yanapofikia kiwango fulani, husababisha kuibuka kwa “aina mpya” au variants.

    Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa baadhi ya dalili zinazojitokeza sana katika maambukizi ya sasa ni pamoja na sauti ya kukwaruza na koo linalouma vikali kana kwamba limechomwa kwa wembe.

    Hata hivyo, Covid-19 bado inaweza kusababisha dalili nyingi kama vile:

    • Maumivu ya kichwa

    • Kikohozi

    • Pua kuziba au kutoa kamasi

    • Uchovu wa mwili

    Dalili hizi hufanana sana na zile za mafua ya kawaida au homa ya msimu, hivyo si rahisi kutambua tofauti bila kipimo rasmi.

    Tahadhari na Ushauri wa Kiafya

    Iwapo unahisi kuwa hujisikii vizuri na una dalili za Covid, ni vema kuepuka kukaribiana na watu walio katika hatari zaidi, kama wazee au watu wenye maradhi sugu.

    Kukaa nyumbani inapowezekana pia kunashauriwa ili kuzuia kusambaza maambukizi zaidi.

    Unapolazimika kutoka, vaa barakoa, osha mikono mara kwa mara, na tumia vitambaa safi (tishu) unapokohoa au kupiga chafya, kisha vitupe kwa usafi.

    Hatua hizi husaidia kupunguza kuenea kwa Covid na magonjwa mengine ya njia ya hewa.

    Kwa koo linalouma, unywaji wa maji ya kutosha na kijiko cha asali kunaweza kupunguza maumivu, kwa mujibu wa ushauri wa Huduma ya Afya ya Taifa (NHS) ya Uingereza.

    Kwa mujibu wa Chuo cha Madaktari wa Familia nchini Uingereza (Royal College of General Practitioners), kiwango cha maambukizi ya Covid-19 kimeongezeka nchini kote, hasa miongoni mwa watoto wadogo na watu wazee.

    Aidha, idadi ya wagonjwa wa Covid wanaolazwa hospitalini inaendelea kuongezeka, hali inayozusha hofu ya athari kubwa zaidi wakati wa msimu wa baridi.

    Watu wenye umri wa miaka 75 na zaidi wanastahili kupata chanjo ya bure ya Covid kupitia NHS.

    Kwa mujibu wa Shirika la Usalama wa Afya Uingereza (UKHSA), chanjo hizi bado zinatoa ulinzi mzuri hata dhidi ya aina mpya za virusi.

    UKHSA inahimiza watu kupata pia chanjo dhidi ya mafua na virusi vingine vya baridi kama RSV (respiratory syncytial virus), ambavyo navyo huenea zaidi wakati wa majira ya baridi.

    “Ni kawaida kwa virusi kubadilika. Kadri tunavyokusanya takwimu zaidi kuhusu aina hizi mpya, ndivyo tutakavyoweza kuelewa vyema jinsi vinavyoshirikiana na kinga ya mwili, na kuchukua hatua sahihi kulinda walio hatarini zaidi,” imeeleza UKHSA.

    “Jambo muhimu zaidi ni kwa wale waliostahili kupokea chanjo, kuhakikisha wanafanya hivyo mara tu inapopatikana.” Dkt. Alex Allen, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza UKHSA, amesema: “Kwa sasa, hakuna ushahidi kwamba aina hizi mpya husababisha maradhi makali zaidi, wala chanjo zinazotumika sasa kuwa na ufanisi mdogo dhidi yao.”

    Pia unaweza kusoma;

  5. Umoja wa Mataifa: Zaidi ya wapiganaji 7,000 wameajiriwa na M23

    G

    Chanzo cha picha, AND

    Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bi. Bintou Keita, ameeleza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kundi la waasi la AFC/M23 limewaajiri zaidi ya wapiganaji wapya 7,000 tangu kuchukua udhibiti wa jiji la Goma.

    Akihutubia kikao maalum cha Baraza hilo, Bi. Keita alisema kuwa kwa kipindi cha miezi saba iliyopita, wapiganaji hao wamepatiwa mafunzo ya kijeshi katika kambi za kundi hilo, huku M23 ikiendelea kujitanua na kuimarisha udhibiti wake katika maeneo iliyoiteka.

    “Katika kipindi cha miezi minane iliyopita, AFC/M23 imeendeleza upanuzi na umarishaji wa nafasi zake, bila kuzingatia masharti na maazimio yaliyowekwa na Baraza hili katika azimio la Februari mwaka huu,” alisema Keita.

    Azimio hilo lilizitaka pande zote zinazohusika kusitisha mapigano mara moja na bila masharti.

    Aidha, lililitaka kundi la AFC/M23 kusitisha mashambulizi, kujiondoa kutoka Goma, Bukavu na maeneo mengine waliyochukua kwa mabavu, na kuacha kuanzisha taasisi mbadala zinazokiuka mamlaka halali ya serikali ya DRC.

    Bi. Keita pia alifichua kuwa tangu mwezi Juni, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO) umeshuhudia ongezeko kubwa la raia wanaokimbilia maeneo yanayodhibitiwa na M23 kutafuta hifadhi.

    Aliongeza kuwa mwezi wa Julai ulikuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia tangu kundi hilo lianzishe mashambulizi yake mwishoni mwa Novemba 2021.

    Licha ya kuelekeza lawama kwa M23, Bi. Keita alibainisha kuwa si kundi hilo pekee linalochochea mzozo wa mashariki mwa DRC.

    Alilitaja kundi la ADF pamoja na CRP na CODECO kuwa pia vinahusika na kuendeleza ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

    Hata hivyo, hakuzungumzia kwa kina kundi la FDLR linalopambana na serikali ya Rwanda kundi ambalo Rwanda imekuwa ikiishutumu serikali ya DRC kwa kushirikiana nalo.

    Serikali ya DRC, kwa upande wake, inakanusha madai hayo na badala yake inaituhumu Rwanda kwa kutumia kisingizio hicho kuhujumu uhuru na mamlaka ya DRC, taifa ambalo limekuwa kwenye hali ya vita kwa karibu miongo mitatu sasa.

    Tangu kuibuka upya kwa mapigano mwishoni mwa mwaka 2021, juhudi za kidiplomasia kurejesha amani zimeendelea kugonga mwamba.

    Bi. Keita alikumbusha kwamba mashirika na mataifa ya kikanda na kimataifa, yakiwemo Marekani, Qatar, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), yameahidi kushirikiana katika mchakato wa amani kupitia njia ya mazungumzo.

    “Wakati huo huo, amani bado iko mbali kana kwamba ni mwezi,” alisema Keita kwa masikitiko.

    Katika hotuba yake, alieleza kwa kina mapungufu katika utekelezaji wa maazimio na mikakati ya kurejesha amani nchini humo, akisisitiza kuwa bila hatua za haraka na thabiti, raia wa Kongo wataendelea kubeba mzigo wa mateso.

    “Tusipofunga mianya hii, mamilioni ya Wakongo wataendelea kulipa gharama ya migogoro isiyokwisha,” alihitimisha.

    Haya yanajiri, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne kutangaza kuwa ameongoza na kusuluhisha mgogoro kati ya DR Congo na Rwanda.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Mbunge wa Afrika Kusini Julius Malema apatikana na hatia ya kufyatua risasi hadharani

    Kiongozi wa Economic Freedom Fighters (EFF) Julius Malema hivi majuzi alitiwa hatiani kwa matamshi ya chuki

    Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa Economic Freedom Fighters (EFF) Julius Malema hivi majuzi alitiwa hatiani kwa matamshi ya chuki

    Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini Julius Malema amepatikana na hatia ya kufyatua risasi hadharani miaka saba iliyopita - kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka 15 gerezani.

    Mnamo 2018, video iliibuka ikimuonyesha kiongozi huyo wa Economic Freedom Fighters (EFF) akifyatua risasi kadhaa hewani wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka mitano ya chama chake zilizofanyika katika jimbo la Eastern Cape nchini humo.

    Alishtakiwa pamoja na mlinzi wake wa zamani Adriaan Snyman, ambaye aliachiliwa huru.

    Malema alipatikana na hatia ya kutoa matamshi ya chuki chini ya miezi miwili iliyopita na mara nyingi huwasuta wazungu wachache katika nchi ambayo, miaka 31 baada ya ubaguzi wa rangi kumalizika, mivutano juu ya suala hilo inaendelea kujitokeza.

    Soma pia:

  7. Viongozi wa Ulaya wakutana baada ya droni za Urusi kuvamia anga lao

    fd

    Chanzo cha picha, Reuters

    Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakusanyika jijini Copenhagen Jumatano ili kuimarisha ulinzi wa Ulaya baada ya msururu wa uvamizi wa Urusi katika anga ya Umoja wa Ulaya.

    Ni siku chache baada ya ndege zisizo na rubani kuvuruga usafiri katika viwanja vya ndege vya Denmark.

    Uvamizi wa droni za Urusi umeongezeka kwa nchi zilizo upande wa mashariki wa EU kama vile Poland na Estonia.

    Nchi kumi wanachama tayari zimeunga mkono mipango ya kuzifuatilia na kuziharibu ndege zisizo na rubani za Urusi.

    Denmark imeimarisha usalama kabla ya mkutano huo, ikipiga marufuku safari zote za ndege zisizo na rubani hadi Ijumaa na kuweka vizuizi vikali barabarani huko Copenhagen.

  8. Waandamanaji warejea mitaani Madagascar licha ya kuvunjwa kwa serikali

    c

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vikosi vya usalama vimefyatua vitoa machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji vijana katika mji mkuu wa Madagascar ambao waliingia tena mitaani siku ya Jumanne licha ya uamuzi wa rais wa kuitikia matakwa yao ya kuivunja serikali.

    Rais Andry Rajoelina alikwenda kwenye runinga ya serikali mwishoni mwa Jumatatu na kusema anataka kufanya mazungumzo na vijana wanaoshinikiza kupata maji na kukomesha kukatwa kwa umeme, na kuahidi hatua za kusaidia biashara zilizoathiriwa na uporaji.

    Wengine walikwenda mbali zaidi, wakipeperusha mabango yenye ujumbe kama vile "Tunahitaji maji, tunahitaji umeme, Rajoelina aondoke."

    Waandamanaji pia waliandamana katika mji wa Fenoarivo, mji mdogo ulio kilomita 20 (maili 12) magharibi mwa mji mkuu.

    Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, mikutano ya hadhara iliripotiwa huko Mahajanga, kilomita 510 (maili 315) kaskazini-magharibi mwa Antananarivo, na huko Diego Suarez, kilomita 950 kaskazini mwa mji mkuu, 2424.

    Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 22 wameuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika maandamano yaliyoanza wiki iliyopita na sasa yako katika siku ya nne.

    Wizara ya mambo ya nje imekataa takwimu za majeruhi za Umoja wa Mataifa, ikisema taarifa hiyo haikutoka kwa mamlaka husika na ilitokana na uvumi au habari potofu.

    Maandamano ya siku nne yamekuwa makubwa zaidi katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, na ni changamoto kubwa zaidi ambayo Rajoelina amekabiliana nayo tangu kuchaguliwa kwake tena 2023.

    Rajoelina aliingia madarakani kwa mara ya kwanza katika mapinduzi ya 2009. Alijiuzulu 2014 lakini akawa rais tena baada ya kushinda uchaguzi wa 2018, na kupata muhula wa tatu katika uchaguzi wa Desemba 2023 ambao wapinzani wake walisema uligubikwa na makosa.

    Wametumia mbinu za mitandaoni kuandaa maandamano kama waandamanaji walivyofanya nchini Kenya na Nepal.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Maandamano ya vijana Morocco yaingia siku ya nne na kugeuka kuwa ghasia

    vc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Vikosi vya usalama vikijiandaa kuzuia maandamano ya kudai mageuzi katika elimu na afya yasifanyike, Septemba 29, 2025.

    Maandamano yaliyoongozwa na vijana kudai elimu bora na huduma za afya nchini Morocco yaliongezeka na kuwa makabiliano makali na vikosi vya usalama Jumanne jioni, ikiwa ni siku ya nne mfululizo ya maandamano katika miji kadhaa.

    Maandamano hayo yalipangwa mtandaoni na kikundi cha vijana, kinachojiita "GenZ 212," kwa kutumia majukwaa ikiwa ni pamoja na TikTok, Instagram na programu ya michezo ya kubahatisha ya Discord.

    Katika miji ya kusini ya Tiznit, Inzegane, na Ait Amira, pamoja na mji wa mashariki wa Oujda, na Temara karibu na mji mkuu Rabat, mamia ya waandamanaji vijana walirusha mawe kwa vikosi vya usalama vilivyojaribu kutawanya mikusanyiko hiyo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani na akaunti za mashahidi.

    Huko Ait Amira, kilomita 560 (maili 350) kusini mwa Rabat, waandamanaji walipindua na kuharibu magari kadhaa ya polisi na kuchoma benki moja.

    Huko Inzegane, video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha waandamanaji waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakichoma moto benki, huku wengine wakikabiliana na polisi.

    Kusini zaidi huko Tiznit, waandamanaji waliwarushia mawe maafisa wa polisi walipokuwa wakijaribu kuvunja mkutano huo, walioshuhudia waliambia Reuters.

    Waandamanaji waliimba kauli mbiu, zikiwemo "Wananchi wanataka kukomesha ufisadi," walisema.

    Huko Oujda, muandamanaji alipata majeraha mabaya baada ya kugongwa na gari la vikosi vya usalama, shirika la habari la serikali MAP liliripoti.

    Huko Rabat, polisi walikamata makumi ya vijana walipojaribu kuanzisha maandamano katika kitongoji chenye watu wengi.

    Chama cha Haki za Kibinadamu cha Morocco (AMDH) kinasema vijana 37 wako nje kwa dhamana, wakisubiri uchunguzi.

    Hakim Saikuk, mkuu wa AMDH huko Rabat, alilaani kukamatwa kwa watu hao kuwa ni kinyume cha katiba.

    Serikali ilitoa taarifa siku ya Jumanne ikieleza nia ya kufanya mazungumzo na vijana "ndani ya taasisi na maeneo ya umma ili kupata suluhu za kweli".

    Pia ilisifu kile ilichokiita "mwitikio wa vyombo vya usalama kulingana na taratibu husika za kisheria".

    Wizara ya mambo ya ndani haikupatikana mara moja kuzungumzia matukio hayo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mbappe afikisha mabao 60 Ligi ya Mabingwa, aweka historia

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kylian Mbappe (katikati)

    Kylian Mbappe alifunga amefunga magoli matatu katika mechi moja na kufikisha mabao 60 kwenye Ligi ya Mabingwa wakati Real Madrid ilipoichabanga Kairat Almaty nchini Kazakhstan.

    Nahodha huyo wa Ufaransa alipiga mkwaju wa penalti dakika ya 25 baada ya kipa Sherkhan Kalmurza kumchezea rafu Franco Mastantuono.

    Aliongeza mabao bao la pili dakika ya 52 alipouunganisha mpira wa Thibaut Courtois na kuuzamisha nyafuni. Dakika ya 73 Mbape akaweka nyavuni goli la tatu.

    Wachezaji wengine waliofunga ni E. Camavinga (83') katika Brahim Díaz (90'+3)

    Ulikuwa ushindi wa 5:0 ulikuwa muhimu sana kwa kikosi cha Xabi Alonso baada ya kufungwa 5-2 na wapinzani wao wa jiji la Atletico Madrid kwenye La Liga Jumamosi.

    Mabao hayo ya Mbappe kwenye Ligi ya Mabingwa – yanamaanisha amempiku mshambuliaji wa zamani wa Bayern Munich Thomas Muller na kuwa mfungaji bora wa sita katika historia ya mashindano hayo.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watu 38 wahofiwa kukwama katika jengo lililoporomoka

    c

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waokoaji huko Java Mashariki, Indonesia wanakimbizana na muda ili kuwapata watu 38 wanaoaminika kuwa wamenasa kwenye vifusi vya jengo la shule ambalo lilianguka siku ya Jumatatu

    Wanafunzi watatu wamefariki na wengine 99 walipelekwa hospitalini, baadhi yao wakiwa na majeraha mabaya, maafisa wanasema, na kuongeza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

    Wengi wa wale ambao wamenaswa ni wavulana ambao walikuwa wamekusanyika kwa maombi wakati jengo hilo lilipoanguka.

    Jengo hilo la ghorofa mbili lilikuwa na msingi usio imara na halikuweza kuhimili uzito wa ujenzi wa ziada wa ghorofa mbili zaidi, maafisa wanasema.

    Waokoaji wanajaribu kuwafikia manusura walionaswa chini ya kifusi - ambao baadhi yao bado wanaitikia - wakati familia zinasubiri kwa wasiwasi habari za wapendwa wao.

    Maafisa wanasema kuna maeneo ambayo bado wanawasiliana na manusura - na wamewapa oksijeni, chakula na maji.

    Operesheni ya uokoaji ilisitishwa kwa muda Jumanne, baada ya mamlaka kuonya juu ya jengo hilo kuanguka zaidi.

    Wanafunzi walikuwa wamekusanyika kwa maombi katika Shule ya Bweni ya Kiislamu ya Al Khoziny, katika mji wa Java Mashariki wa Sidoarjo, wakati jengo hilo lilipoporomoka.

    Mamlaka inasema shule hiyo haikuwa na vibali vya kupanua jengo lake.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Watu 69 wafariki katika tetemeko kubwa la ardhi Ufilipino

    c

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban watu 60 wamefariki katika tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.9 katika kipimo cha Richter katikati mwa Ufilipino, wanasema maafisa wa usimamizi wa majanga.

    Mji wa Bogo na miji mingine iliyoathiriwa wametangaza 'hali ya maafa' huku wakitathmini uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo.

    Tetemeko la ardhi lilitokea kwenye ufuo wa Cebu City siku ya Jumanne na kusababisha kukatika kwa umeme na kuharibu majengo.

    Taasisi ya Ufilipino ya Volcanology na Seismology haijatoa tahadhari ya kutokea kwa tsunami.

    Wakaazi katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko wameiambia BBC kuwa walilala nje mitaani jana usiku.

    Askofu mkuu wa Cebu amewaambia waumini kukaa mbali na makanisa. Wito huu ni muhimu kwani Cebu kilikuwa mojawapo ya visiwa vya kwanza vya Ufilipino kutawaliwa na Uhispania katika miaka ya 1500, na kina makanisa mengi ya zamani.

    Mji wa Cebu, ilioko katika eneo la Visayas, ina wakazi karibu milioni moja.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Rais wa zamani wa Congo ahukumiwa kifo kwa uhalifu wa kivita

    cx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Joseph Kabila alirejea DR Congo mwezi Mei baada ya kuishi uhamishoni

    Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila amehukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani kwa uhalifu wa kivita na uhaini.

    Mashtaka hayo yanamshutumu Kabila kuunga mkono kundi la M23, kundi la waasi ambalo limesababisha uharibifu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

    Kabila alitiwa hatiani siku ya Ijumaa na mahakama ya kijeshi kwa uhaini, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.

    Alikana mashtaka, lakini hakufika mahakamani kujitetea. Pia aliikataa kesi hiyo na kusema mahakama inatumiwa kama "chombo cha ukandamizaji". Kwa sasa hajulikani alipo.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 54 aliiongoza DR Congo kwa miaka 18, baada ya kumrithi babake Laurent, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 2001.

    Kabila alikabidhi madaraka kwa Rais Félix Tshisekedi mwaka 2019, lakini baadaye walitofautiana na akaenda uhamishoni mwaka 2023.

    Mwezi Aprili mwaka huu, rais huyo wa zamani alisema anataka kusaidia kutafuta suluhu ya mgogoro katika eneo la mashariki na aliwasili katika mji unaoshikiliwa na M23 wa Goma mwezi uliofuata.

    Rais Tshisekedi alimshutumu Kabila kwa nyuma ya M23 na maseneta walimwondolea kinga yake ya kisheria, na hilo kufungua njia ya kufunguliwa mashitaka.

    Mapema mwaka huu M23 ilitwaa udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ikiwa ni pamoja na Goma, jiji la Bukavu na viwanja viwili vya ndege.

    Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa za Magharibi zimeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono M23, na kutuma maelfu ya wanajeshi wake nchini DR Congo.

    Lakini Kigali inakanusha mashtaka hayo.

    Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali yalifanyika mwezi Julai, lakini umwagaji damu umeendelea.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Serikali ya Marekani yafunga shughuli zake rasmi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maseneta wa Marekani wameshindwa kupitisha mswada wa dakika za mwisho wa kuzuia kufungwa kwa shughuli za serikali, ambao ungehakikisha kuendelea kwa ufadhili wake.

    Hii ni mara ya kwanza tangu 2018. Ingawa wafanyakazi muhimu wa serikali wataendelea na majukumu yao kama kawaida, lakini wale wanaoonekana sio muhimu watalazimika kwenda likizo bila malipo.

    Huduma zitakazo athirika zaidi ni pamoja na mpango wa usaidizi wa chakula, shule za chekechea zinazofadhiliwa na serikali, utoaji wa mikopo ya wanafunzi, ukaguzi wa chakula na shughuli katika mbuga za kitaifa.

    Rais Trump ametishia kupunguza bajeti ikiwa kufungwa huko kutatokea, na ametupa lawama zake kwa Wanachama wa Democratics.

    Kufungwa huku kutawaacha maelfu ya wafanyakazi kwenye likizo bila malipo na kusimamishwa kwa programu na huduma nyingi za serikali.

    Hili limekuja saa chache baada ya Seneti inayodhibitiwa na Republican kushindwa kupitisha mswada wa matumizi ya serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Natumai hujambo