'Mama yangu bado amenaswa kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka'

Haijajulikana idadi ya waliokwama kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka
Maelezo ya picha, Haijajulikana idadi ya waliokwama kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka
    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC News
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanaume mmoja kutoka Tanzania, Dar es Salaam, ameiambia BBC kwamba anasubiri kusikia habari za mama yake, ambaye bado amekwama chini ya kifusi siku mbili baada ya jengo kuanguka.

Shughuli za uokoaji zinaendelea na kufikia sasa watu 86 wameokolewa wakiwa hai huku 16 wakifariki, alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Emmanuel Mallya aliambia idhaa ya BBC kwamba mama yake alikuwa akifanya kazi katika jengo hilo wakati lilipoporomoka asubuhi ya Jumamosi.

“Alinipigia simu na baadaye akaniambia alikuwa akihudumia wateja. Masaa mawili baadaye, nilijulishwa kwamba jengo lilikuwa limeanguka,” alisema.

"Waokoaji wamenihakikishia kuwa wanazungumza naye kwani amekwama na wengine hapo chini”

“Nina Imani atapatikana akiwa hai kwasababu nimeona juhudi zinazoendelea na mengine tunaachia Mungu."

Mallya ni miongoni mwa familia ambazo zinasubiri kupata taarifa kuhusu wapendwa wao waliokwama kwenye kifusi cha jengo lililodondoka katika soko la Kariakoo.Hata hivyo ,bado idadi ya waliokwama kwenye vifusi haijulikani .

Waokoaji wamekuwa wakiwasambazia maji,na mitungi ya oksigeni kwa wale waliokwama ili wajisaidie wakisubiri kuokolewa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Waziri mkuu Kassim Majaliwa ametoa hakikisho kuwa baada ya kila mtu kuokolewa kwa jengo hilo uchunguzi wa kina utaanza kubaini chanzo cha jengo hilo kudondoka.Wakati huo huo maafisa wa ujasusi wanaendelea kufuatilia mmiliki wa jengo hilo ili kusaidia katika uchunguzi wa mkasa ulioua watu kadhaa.

Majaliwa aliongea hayo akiwa katika uwanja wa Mnazi mmoja ambapo waliofikwa na msiba walikusanyika kuwapa mkono wa buriani wapendwa wao waliofariki na kuchukua miili yao kwa maziko.

Vile vile,kati ya wale waliokolewa kwenye kifusi cha jengo hilo wakiwa hai watano wanaendelea kupokea matibabu ya dharura katika hospitali zilizoko karibu na eneo la mkasa.

"shughuli za uokoaji ni endelevu hadi pale tutaokoa mtu wa mwisho," Majaliwa amesema.

Baada ya jengo hilo kuporomoka saa tatu asubuhi majira ya Afrika mashariki Jumamosi asubuhi,waokoaji waliofika kwa mkasa walianza shughuli za uokoaji kwa kutumia nyundo wengine wakitumia mikono kuondoa mawe yaliyofunika wenzao,haya ni kulingana na ripoti ya chombo cha habari cha AFP.

Tinga tinga na mashine za uokoaji zililetwa baadaye ili kusaidia kuokoa hali.Jengo hilo liliporomoka kabla ya shughuli za biashara kunoga zinazovutia wateja wengi.

Haya yakijiri,timu ya watu 19 imebuniwa ili kukagua ufaafu wa majengo katika jiji la Dar es salaam.Kikosi hicho kitachunguza na kuwasilisha ripoti kuhusu vibali vinavyotolewa kabla ya ujenzi na iwapo majengo yamekidhi viwango hitajika na kupendekeza mikakati salama ili kuepuka ajali kama hizo siku za usoni.

Soma zaidi:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Yusuf Jumah