Rais Samia aagiza majengo yote Kariakoo kukaguliwa; waliofariki wafikia 13

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 1

Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuundwa kwa timu ya kukagua hali ya kimuundo ya majengo yote jijini Dar es Salaam na hasa katika eneo la Kariakoo lenye shughuli nyingi, kufuatia jengo la ghorofa nne kuporomoka mapema Jumamosi.

Rais alisema Jumapili kuwa hadi sasa watu 13 wameuawa, huku wengine 84 wakijeruhiwa.

Katika ujumbe wa video uliorekodiwa siku ya Jumapili, Rais Hassan, ambaye kwa sasa yuko nchini Brazil kwa Mkutano wa Viongozi wa G20 mjini Rio de Janeiro, aliuhakikishia umma kwamba shughuli ya uokoaji inayoendelea inaendelea vyema. Alieleza kuwa serikali iliweka kipaumbele katika kuokoa watu waliokwama chini ya vifusi, jambo ambalo lilisababisha kuchelewa kwa uchunguzi wa chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo.

TH

“Baada ya tukio hili la kusikitisha, namuagiza Waziri Mkuu aongoze timu ya wakaguzi wa majengo kuendelea na ukaguzi wa kina wa majengo yote ya eneo la Kariakoo, ili tuweze kupata tathmini ya kina ya hali yake ya kimuundo,” alisema Rais Hassan.

Aidha alitangaza kwamba polisi watakusanya taarifa kamili kutoka kwa mmiliki wa jengo lililoporomoka kuhusu ujenzi wake.

Matokeo ya uchunguzi yatatolewa hadharani, huku serikali ikijitolea kuchukua hatua zozote muhimu kulingana na matokeo.

Serikali pia imeahidi kulipia gharama za matibabu kwa majeruhi na kuhakikisha kuwa walioaga wanashughulikiwa kwa heshima inayostahili.

"Tunaendelea kupokea taarifa za uokoaji kutoka kwa Waziri Mkuu. Tunatoa pole kwa familia za walioathirika na tukio hili la kusikitisha," Rais Hassan alisema. "Serikali itaendelea kutoa maelezo hadi shughuli ya uokoaji itakapokamilika."

Kwa sasa, chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo bado kinachunguzwa, lakini Rais Hassan alisisitiza kuwa lengo kuu ni kuokoa maisha ya walionaswa.

"Kipaumbele chetu cha kwanza kilikuwa kuokoa wale walionaswa. Bado hatujabaini sababu za kiufundi za jengo hilo kuporomoka, kwani lengo letu limekuwa kuokoa maisha," aliongeza.

Shughuli ya uokoaji inaingia siku ya tatu leo .