Kombe, goli na hakuna kikomo - enzi ya Mbappe wa Madrid imeanza

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Steven Sutcliffe
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kylian Mbappe anasema hakuna kikomo kwa kile ambacho yeye na Real Madrid wanaweza kukifanikisha pamoja, baada ya kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza dhidi ya Atalanta na kuisaidia klabu hiyo kushinda mara ya sita Uefa Super Cup.
Nahodha huyo wa Ufaransa alikamilisha uhamisho uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na kujiunga na Real msimu huu wa joto baada ya kunyakua mataji katika klabu ya Paris St-Germain.
Na licha ya kuanza mazoezi tena wiki moja iliyopita, ilimchukua mfungaji bora wa PSG chini ya dakika 70 kufunga goli lake la kwanza ndani ya msimu mpya, na kuhakikisha mwanzo wa ushindi na zawadi zaidi kwa waajiri wake wapya.
"Ulikuwa usiku mzuri - nimekuwa nikingojea wakati huu kwa muda mrefu," amesema Mbappe kwa Kihispania fasaha. “Kucheza na shati hili, na beji hii, kwa mashabiki hawa, ni zawadi kwangu."
Huku Vinicius Junior, Jude Bellingham, Rodrygo na Endrick pia wakiwa chini ya meneja Carlo Ancelotti, kuongezwa kwa Mbappe - ambaye bila shaka ndiye mchezaji na mshambuliaji bora duniani - kumeimarisha mabingwa wa sasa wa Uropa na Uhispania.
"Tuko Real Madrid, hatuna kikomo. Ikiwa naweza kufunga bao 50, basi 50, lakini jambo muhimu zaidi ni kushinda na kuboresha timu, kwa sababu tutashinda kama timu," aliongeza Mbappe.
Kiungo wa kati wa Uingereza Bellingham, ambaye alicheza vizuri katika ushindi wa Real dhidi ya timu ya Serie A anasema kuhusu Mbappe, "Ni mchezaji wa kipekee, mwenye kipaji.”
"Hodari sana. Ni fundi sana. Mchezaji mwenzangu ambaye ni mzuri sana. Anafanya kazi kwa ajili ya timu, kama vijana wengine. Pongezi kwake, na anastahili pongezi usiku wa leo."
Akizungumza na TNT Sports, Ancelotti alisema: "Mbappe alicheza vizuri sana. Ameizoea timu vizuri. Alishirikiana vyema na Vinícius Jr na Bellingham.
"Kwa kweli, tuna timu bora, lakini lazima tucheze kwa pamoja na tumefanya hivyo usiku wa leo."
Wameongeza mchezaji bora
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wachambuzi wa TNT wakimtazama Mbappe wamemsifu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye alipokea shangwe alipotolewa mwishoni mwa mchezo.
"Mbappe kupata bao lake ndicho ambacho mashabiki wote wa Real Madrid walikitaka," alisema beki wa zamani wa Uingereza na Manchester United, Rio Ferdinand.
"Wameongeza mchezaji bora wa dunia kwenye timu hii. Kwa sababu wana vijana wengi. Wanaongeza wachezaji wenye njaa ya magoli. Mbappe amedhihirisha uwezo wake – lakini haijalishi ni mzuri kiasi gani, bado hajafanya uzuri wake wote hapa. Kuna mengi ya kufanywa na wachezaji hawa."
Huku Mbappe akibadili upande wa kushoto baada ya mapumziko na Vinicius Jr akizunguka katikati zaidi, iliruhusu Bellingham kusonga mbele na kudhibiti mchezo kwa Real dhidi ya Atalanta.
"Bellingham alikuwa wa kipekee kabisa katika nafasi ya namba nane. Uchezaji wake ulikuwa mzuri," aliongeza Ferdinand.
"Timu pinzani zitalazimika kuwakabili Mbappe na Vinicius Jr, jambo ambalo linampa Bellingham nafasi nzuri zaidi."
Kiungo wa kati wa zamani wa England na Bayern Munich, Owen Hargreaves anasema: "Wakiwa na Jude na Vinicius Jr, Real Madrid ilicheza vyema zaidi katika kipindi cha pili.
"Ancelotti ndiye meneja bora, meneja wa wachezaji, kwa kumuongeza Mbappe na Endrick Felipe Moreira de Sousa ambaye atakuwa mchezaji mchanga na mzuri. Kundi hili la wachezaji ni la kipekee kabisa."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












