Matukio matano makubwa ya kuvuja taarifa za kijasusi Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Siku ya jana, mhariri mkuu wa jarida la The Atlantic, huko Marekani alifichua kuwa alijua saa mbili kabla juu ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Wahouthi nchini Yemen, baada ya maafisa wa utawala wa Donald Trump kuchapisha taarifa hizo katika kundi la WhatsApp ambalo yeye aliingizwa kimakosa.
Jeffrey Goldberg, mhariri wa The Atlantic, aliingizwa kwenye kundi hilo lililojumuisha makamu wa rais wa Marekani JD Vance, Waziri wa ulinzi Pete Hegseth, mshauri wa usalama wa taifa Mike Waltz na mkurugenzi wa ujasusi wa taifa Tulsi Gabbard.
"Utawala huu unacheza na taarifa muhimu zaidi katika taifa letu, na inawafanya Wamarekani wote kutokuwa salama," aliandika Seneta Mark Warner wa Virginia, kwenye mtandao wa X ambaye ni mwanasiasa mwandamizi na kiongozi wa juu katika Kamati ya Ujasusi ya Seneti.
Lakini kuvuja kwa taarifa za kijasusi sio tukio la kwanza nchini Marekani. Makala hii itagusia matukio mengine matano ya kuvuja taarifa za kijasusi ambayo yaliacha athari kubwa katika siasa, usalama na diplomasia ya Marekani.
Nyaraka za 2023

Chanzo cha picha, Facebook
Aprili 2023, serikali ya Marekani ilimfungulia mashtaka Jack Teixeira (21), mfanyakazi wa kitengo cha kijasusi katika Jeshi la Anga la Marekani huko Massachusetts, kwa tuhuma za kuvujisha nyaraka za siri kwenye mtandao.
Mashirika makuu ya habari Bellingcat, New York Times na Washington Post yalipoti kuwa Bw Teixeira alichapisha nyaraka hizo nyeti katika kundi la mtandao wa kijamii wa Discord. Na hatimaye zilivuja kwenye mitandao yote ya kijamii.
Hati hizo zilikuwa zinatoa maelezo juu ya hali ya vita nchini Ukraine, pamoja na taarifa za kijasusi kwa washirika wa Marekani kama vile Korea Kusini na Israel.
Nyaraka za Pentagon

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1971, Daniel Ellsberg, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Jeshi la Marekani, akiwa katika Shirika la utafiti la RAND, alivujisha ripoti iliyoagizwa na jeshi la Marekani kuhusu Vita vya Vietnam. Vita hivyo vilikosolewa sana ndani na nje ya nchi, na ripoti hiyo ilifichua taarifa ambazo serikali ya Marekani ilikuwa imezificha kwa umma.
Gazeti la New York Times lilitumia hati hizo kufichua matukio mbalimbali yaliyofanywa na Marekani nchini Vietnam.
Awali Bw Ellsberg alishtakiwa kwa ujasusi, lakini jaji alitupilia mbali mashtaka hayo 1973. Ellsberg anachukuliwa kuwa mmoja wa wavujisha taarifa muhimu za serikali katika historia ya Marekani, na mtetezi wa uwazi wa serikali.
Nyaraka za NSA

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2013, Edward Snowden alivujisha taarifa za kijasusi kwa gazeti la Guardian na Washington Post, kuonyesha kuwa serikali ya Marekani ilikuwa ikikusanya data za simu za raia kinyume cha sheria.
Nyaraka hizo zilifichua kazi za ndani za Shirika la Usalama wa Taifa (NSA), mojawapo ya mashirika ya kijasusi ya Marekani. Pia nyaraka hizo zilifichua ukusanyaji wa siri wa taarifa za serikali zote ulimwenguni, zikiwemo washirika wa Marekani kama vile Uingereza, Australia na New Zealand.
Serikali ya Marekani ilimshtaki Bw Snowden kwa ujasusi na wizi wa mali ya serikali, lakini alipata hifadhi nchini Urusi, ambako sasa anaishi uhamishoni.
Chelsea Manning na Wikileaks

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2010, Chelsea Manning, ambaye wakati huo alikuwa mwanajeshi na mchambuzi wa masuala ya kijeshi katika Jeshi la Marekani, alivujisha maelfu ya nyaraka za siri kwa Wikileaks. Shirika hilo, lililokuwa likiongozwa na Julian Assange, lilijitolea kuchapisha nyaraka hizo.
Nyaraka zilizotolewa na Manning zilikuwa na maelezo kuhusu vita vya Iraq na Afghanistan, pamoja na taarifa za kidiplomasia. Wikileaks iliweka hadharani nyingi ya nyaraka hizo na mashirika makubwa ya vyombo vya habari yalichapisha taarifa hizo.
Mojawapo ya mambo yaliyofichuliwa ni video ya helikopta ya Apache ya Marekani ikiwaua raia 12, wakiwemo waandishi wawili wa habari wa Reuters, huko Baghdad mwaka 2007.
Manning alihukumiwa kifungo cha miaka 35 jela. Adhabu yake ilibadilishwa na Rais Barack Obama 2017, baada ya kuhudumu kwa miaka saba.
Manning aligombea kiti cha u-Seneti mwaka 2018 bila mafanikio.
Kesi ya Reality Winner

Chanzo cha picha, Bruce Glikas/WireImage
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka 2017, mwanajeshi wa zamani wa Jeshi la Anga na mfasiri katika Shirika la Usalama wa Taifa (NSA), Reality Winner, alikamatwa na kushtakiwa kwa kutoa ripoti ya siri kwa tovuti ya habari The Intercept.
Hati hiyo ilieleza kwa kina juhudi za Urusi kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016 kwa kutumia mbinu za uhalifu wa mtandao ili kupata maelezo binafsi ya maafisa wa uchaguzi wa mashinani.
Winner alivujisha hati hiyo bila kujulikana, lakini wachunguzi wa serikali waliweza kubaini asili ya ilipotoka hati hiyo baada ya The Intercept kuipeleka kwa NSA ili kuthibitisha ni yao.
Baada ya kukamatwa, Winner alikiambia kipindi cha televisheni cha Marekani cha 60 Minutes, kwamba alihisi analazimika kuwaambia ukweli Wamarekani kuhusu majaribio ya Urusi kuingilia uchaguzi wa 2016, ikizingatiwa kuwa Rais wa wakati huo Donald Trump alikanusha mara kwa mara jambo hilo.
Winner alipatikana na hatia ya kuvujisha nyaraka hizo kwa shirika la habari. Alikaa gerezani kwa miaka minne na aliachiliwa kwa uangalizi mwaka 2021.















