Je, ulimwengu unapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu virusi vipya HMPV?

Chanzo cha picha, EPA
Kuongezeka kwa magonjwa ya mfumo wa kupumua ikiwemo virusi vya Human Metapneumovirus (HMPV) kaskazini mwa China kumezua wasiwasi mkubwa.
Haya yanajiri miaka mitano baada ya kuibuka kwa virusi vya Covid-19 nchini China, ambavyo vilisababisha janga la kimataifa na vifo milioni saba.
Mafisa wakuu wa afya wa China wamesema kuwa idadi ya maambukizi, hasa kwa watoto chini ya umri wa miaka 14, inaongezeka, lakini wamekana madai kwamba hospitali nchini humo zimejaa kutokana na virusi hivyo.
Maambikizi ya virusi hivi pia vimeripotiwa nchini India.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, ugonjwa wa HMPV ni virusi vipya?

Kwa mujibu wa kituo cha kukabiliana na kudhibiti magonjwa (CDC) nchini Marekani, virusi hivi viligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001, ingawa wataalamu wanasema kuwa huenda virusi hivi vimekuwepo kwa miongo mingi kabla ya hapo.
Kwa kawaida, dalili za HMPV ni sawa na zile za mafua au homa.
Zinaweza kujumuisha kikohozi, homa, kuziba kwa pua, na upumuaji wa shida.
Kwa wengine, inaweza kuwa hali mbaya zaidi.
CDC inasema kuwa virusi hivi vinaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa kupumua hewa, kama vile kikoromeo na kichomi, kwa watu wa rika zote, lakini mara nyingi huonekana zaidi kwa watoto wadogo, watu wazee na wale wenye mifumo ya kinga dhaifu.
Kipindi cha kuambukizwa virusi hivi ni kati ya siku tatu hadi sita, na muda wa kuumwa unaweza kutofautiana kulingana na uzito wa hali, lakini kawaida ni sawa na magonjwa mengine ya mfumo wa kupumua yanayosababishwa na virusi.
CDC inasema kuwa virusi vya HMPV vinaonekana kuwa vimekuwa na ufanisi zaidi mwishoni mwa msimu wa baridi na mapema katika msimu wa joto katika maeneo yenye mabadiliko ya hali ya hewa.
Je unaambukizwa vipi?
HMPV kwa kawaida husambazwa kutoka kwa mtu aliyeambukizwa kwenda kwa wengine kupitia kukohoa na kupiga chafya.
Vinaweza pia kusambazwa kupitia mgusano wa karibu, kama vile kugusa au kushikana mikono, au kugusa vitu au maeneo vilivyo na virusi na kisha kugusa mdomo, pua au macho.
Virusi hivi husambaa zaidi katika miezi ya msimu wa baridi ambapo watu hukaa ndani ya majumba.
Kwanini watoto na wazee wamo hatarini kuambukizwa?
Mtu anaweza kuambukizwa na ugonjwa wa HMPV mara kadhaa.
Wataalamu wanasema kuwa wakati wa kwanza mtu anapokumbwa na virusi hivi, ndiyo huwa mbaya zaidi.
Baadaye, kinga hupatikana na uwepo mwingine wa HMPV unaweza kuwa mwepesi, mradi tu mfumo wa kinga bado upo imara na haujadhurika na magonjwa mengine kama vile UKIMWI au saratani.
Hii inaelezea kwa nini watoto wadogo walio chini ya miaka mitano na wazee wa miaka 65 na zaidi, ambao wana mifumo dhaifu ya kinga au matatizo ya kupumua, wanakuwa katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa mzito wa HMPV.
Hata hivyo, kwa kuwa HMPV inadhaniwa kuwa imedumu kwa miongo mingi, wataalamu wanakubali kuwa kumekuwepo na kiwango kikubwa cha kinga kilichojengeka duniani kote kutokana na virusi hivi.
Ni kipi kinaendelea China?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Picha na video za watu waliovaa barakoa hospitalini nchini China zimeenezwa kwenye mitandao ya kijamii, hali ambayo imeongeza dhana kwamba hospitali hizo zimejaa.
Baadhi ya taarifa za ndani zililinganisha hali hii na mlipuko wa awali wa Covid.
Kiongozi wa Idara ya Magonjwa ya Kuambukiza katika CDC ya China, Kan Biao, alisema kuwa nchi hiyo inatarajiwa kukumbwa na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ya kupumua katika msimu wa baridi na joto.
Alisema kuwa idadi ya visa vya HMPV kwa watu chini ya umri wa miaka 14 inaonyesha "mwelekeo wa kuongezeka."
Lakini aliongeza kusema kuwa jumla ya visa vya magonjwa ya kupumua mwaka 2024 inatarajiwa kuwa ndogo ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Profesa Tulio de Oliveira, mkurugenzi mwanzilishi wa kituo cha kubuni na kudhibiti majanga, alisema kuwa HMPV ni mojawapo ya virusi vinavyosababisha wimbi la magonjwa ya msimu wa baridi nchini China – vinginevyo ni virusi vinavyoathiri mfumo wa kupumua (RSV), Covid na homa ya mafua.
Alieleza kuwa baadhi ya shinikizo katika hospitali za China lilikuwa linatarajiwa kutokana na msimu huu na mzunguko wa virusi hivi vinne.
China ilitangaza Ijumaa kuwa inajaribu mfumo wa ufuatiliaji kwakichomi kisicho cha wazi, huku visa vya magonjwa ya kupumua vikitazamiwa kuongezeka katika msimu wa baridi.
Hii inatofautiana na kiwango cha maandalizi cha miaka mitano iliyopita wakati Covid-19 ilipoibuka.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi












