Kwanini ugonjwa huu unaoweza kuzuiwa unawauwa maelfu ya watu?

Na Kennedy Gondwe
BBC News, Lusaka
Nilipokutana na Andrew Kazadi baada ya mpwa wake mwenye umri wa miaka 26 kufariki kutokana na ugonjwa kipindupindu katika kituo cha matibabu katika mji mkuu wa Zambia Lusaka, alionekana kuwa na majonzi makubwa.
"Tumeambiwa tutafute jeneza tulilete wamuweke ndani lakini tukichelewesha, watamzika kwa namna hiyo," alisema Kazadi, katika matamshi yanayokumbusha baadhi ya masharti ya vizuizi yaliyowekwa na serikali wakati wa janga la virusi vya corona.
Ugonjwa wa kipindupindu unaosababishwa na maambukizi ya bakteria wanaosababishwa na maji au chakula kichafu , umesababisha maafa makubwa sana nchini Zambia, na zaidi ya vwatu 15,000 wamekumbwa na ugonjwa huu huku karibu vifo 600 vikirekodiwa, hasa katika eneo la mji mkuu Lusaka, tangu mwanzo wa msimu wa mvua ulioanza mnamo mwezi wa Oktoba.
Na wakati mawingu yakikusanyika juu ya anga kabla ya mvua nyingine kunyesha , Bwana Kazadi anasema: "Tunapaswa kuharakisha kupata jeneza."
Nilikutana naye nje ya uwanja wa Mashujajaa (heroes Stadium) wenye viti 60,000, ambao umegeuzwa kuwa kituo cha matibabu na madaktari 800 wanaohudumia wagonjwa kutoka nchi nzima.
Sauti za ving'ora vya kuomboleza vya ambulensi vinasikika mara kwa mara. Wagonjwa huletwa au kupelekwa kwa mazishi baada ya kuugua ugonjwa huo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa Bwana Kazadi, kuiona maiti isiyo na uhai ya Charles, mtoto wa dada yake, lilikuja kama jambo la mshtuko.
Charles alipatwa na ugonjwa wa kuhara na alikuwa anatapika. Alipelekwa kliniki, ambapo familia iliambiwa alikuwa na kipindupindu.
Kisha akahamishiwa uwanjani – uwanja ambao kwa kawaida ni uwanja wa mechi za mpira wa miguu - ambapo alifariki siku nane baadaye.
"Matarajio yetu yalikuwa kwamba atakuwa sawa. Kwa kweli tunaomboleza kama familia," alisema Kazadi, akieleza kuwa mpwa wake ameacha mtoto mwenye umri wa miaka mitatu.
Lakini katika ishara ya imani ya kina ya familia, aliongeza: "Mtu anapokuwa mgonjwa, tunaweka kila kitu mikononi mwa Mungu - mtu huyo anaweza kufa au kuishi. Kwa changamoto zote tulizopitia, tunapaswa kumshukuru Mungu."
Kwa kuzingatia kanuni za serikali za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, maiti ya Charles ilifungwa kwenye mfuko wa kuhifadhi mwili, kabla ya kuwekwa kwenye jeneza na wanaume waliokuwa wamevaa vifaa vya kujikinga.
Familia haikuruhusiwa kuugusa mwili ili kuwalinda kutokana na hatari ya maambukizi. Ni ndugu watano tu walioruhusiwa kuhudhuria mazishi ya Charles.
Miongozo ya serikali ni sawa na ile ya Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo inashauri kwamba familia zinapaswa kushughulikia mwili kidogo iwezekanavyo, na mazishi yanapaswa kufanyika ndani ya saa 24.
"Maambukizi ya utumbo [kama kipindupindu] yanaweza kuambukizwa kwa urahisi kutoka kwa kinyesi kuvuja kutoka kwa miili ya wafu," WHO inasema.

Chanzo cha picha, Andrew Kazadi
Lakusikitisha, baadhi ya familia za Lusaka zinapitia kiwewe tofauti na kile cha familia ya Kazadi.
Hawajui hatima ya wapendwa wao, kwani wahudumu wa afya waliozidiwa nguvu wameshindwa kuwaeleza kuhusu hali yao - au kama hata wako hai.
Miongoni mwao ni Eunice Chongo, ambaye aliniambia kuwa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 34, Boniface, aliletwa na gari la wagonjwa uwanjani wiki moja iliyopita, lakini hajasikia taarifa yoyote kumhusu tangu wakati huo.
"Ninachotaka ni kwa serikali kuniambia ukweli kuhusu mahali alipo mwanangu," Bi Chongo alisema huku akionekana kuhuzunika.

Serikali imeanzisha kituo cha kupiga simu, ikiwataka watu kama Bi Chongo kuripoti familia iliyopotea ili waweze kusaidia kuwafuatilia.
Zambia imekumbwa na milipuko ya kipindupindu mara 30 tangu mwaka 1977, huku shirika la misaada la WaterAid likisema kuwa lmlipuko wa hivi karibuni ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2017.
Hii ni licha ya ukweli kwamba serikali iliahidi mwaka 2019 kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi wa WaterAid nchini Zambia Yankho Mataya amesema serikali haitatimiza lengo lake "bila ya kuongeza uwekezaji na kuboresha uratibu wa kushughulikia chanzo cha tatizo hilo,ambacho ni ukosefu wa maji safi na usafi wa mazingira".
Utafiti uliochapishwa mwaka 2019 ulionyesha kuwa idadi kubwa ya Wazambia - 40% - walikuwa wakiishi bila maji safi ya kutosha, huku asilimia 85 wakiwa hawana usimamizi sahihi wa uhufadhi wa taka ngumu.

Mratibu wa Kitengo cha Usimamizi na Kukabiliana na Maafa nchini Zambia, Gabriel Pollen, anasema takwimu bado zinakusanywa ili kutathmini ni hatua gani zimepigwa tangu mwaka 2019 ili kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.
"Idadi hiyo inatisha sana, na tunaona hapa kuzorota kwa upande wa jamii katika suala la usafi," alisema.
Maeneo ya mlipuko wa kipindupindu mjini Lusaka ni vitongoji duni, vinavyojulikana kama misombo, ambapo watu wanaishi katika makazi duni.
Mara nyingi vyoo vya shimo hujengwa karibu sana na maeneo ambako kuna visima vya maji ya kunywa.
Wakati mvua inaponyesha, kiwango cha maji huongezeka, pamoja na hatari ya taka za binadamu kuchafua maji - na mifereji mibovu husababisha maji haya kufurika majumbani.
Ili kupambana na ugonjwa huo, hatua kadhaa zimechukuliwa na serikali, ikiwa ni pamoja na marufuku ya kuchimba visima virefu, na uuzaji wa chakula katika hali isiyo ya usafi.
Katika hotuba yake mapema mwezi huu, Rais Hakainde Hichilema aliahidi pia kuboresha makazi yasiyo rasmi, na kuzuia ujenzi wa makazi duni mapya.
Baadhi ya vijana wamekuwa "wakizunguka na kutofanya chochote" katika miji na mitaa badala ya kuhamia vijijini kulima, rais alisema.
"Kuna maeneo mengi sana ya vijijini. Kuna maji safi. Tunaweza kujenga nyumba nzuri katika vijiji, ambavyo havijachafuliwa," aliongeza.

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati huenda serikali ikaona kuwa kuzuia msongamano wa watu katika miji kama suluhisho la muda mrefu, kipaumbele chake sasa ni kuzuia kupoteza maisha zaidi kupitia kampeni ya chanjo.
Ilipokea dozi milioni 1.6 mapema mwezi huu, na hadi sasa imesimamia idadi kubwa ya utoaji wa chanjo hizo, hasa katika mi wa Lusaka.
"Majibu yamekuwa ya kushangaza. Tuna wasiwasi tu kama tutaweza kutoa kutoa huduma ya chanjo katika maeneo yote yenye maambukizi na dozi tulizonazo," Waziri wa Afya Sylvia Masebo alisema, katika mkutano wa hadhara.
Bi Masebo hakutoa maelezo zaidi, lakini baadhi wanaamini kwamba chanjo huwachafua kiroho.
Ujumbe kwao ulikuwa: "Tafadhali tusivurugwe na imani kama hizo. Sote tunajua kwamba dini ya kweli inalenga kulinda afya ya waumini."
Bi Masebo pia alibaini kusita kupokea chanjo chanjo miongoni mwa kundi jingine - vijana.
Tena, hakuingia kwa undani, lakini alionekana akimaanisha ukweli kwamba baadhi yao wanaamini hawahitaji kuchanja kwani wana mfumo imara wa kinga.
Wanaume wengine wamekuwa wakinywa pombe zaidi, kwani wanaamini inaua bakteria ambayo husababisha kipindupindu.
Katika kile kilichoonekana kuwa ujumbe ulioelekezwa kwao, Bi Masebo alisema watu wanapaswa kutumia pesa zao kwa klorini - ambayo huua bakteria ndani ya maji - badala ya bia.
Lakini Bi Masebo atalazimika kurudia ujumbe huo zaidi, kabla ya kubadili imani za vijana ambao wanazidi kuzuru kumbi za bia za Lusaka.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi












