Virusi vya corona: Nchi sita Afrika kuanzisha uzalishaji wa chanjo ya mRNA

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Dorcas Wangira
- Nafasi, BBC Health
Nchi sita za Afrika ,Misri, Kenya, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia, zitakuwa za kwanza barani humo kuanzisha uzalishaji wa chanjo ya mRNA.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO ametoa tangazo hilo kuu katika mkutano wa Umoja wa Ulaya - Umoja wa Afrika mjini Brussels leo katika hafla iliyoandaliwa na Baraza la Ulaya, Ufaransa, Afrika Kusini. Nchi zote sita zilituma maombi ya kupata teknolojia inayohitajika kuzalisha chanjo ya mRNA katika wito uliotolewa na WHO Mnamo Aprili mwaka 2021.
Tangazo hili muhimu kwa Afrika linakuja huku bara hilo likiwa na shauku ya kuelekea katika utengenezaji wa chanjo zake. WHO kupitia kikundi cha wataalamu, ilichagua idadi ya wanufaika katika kanda zote sita za WHO kupokea teknolojia ya chanjo za mRNA. Mafunzo ya wapokeaji wa kwanza yataanza mwezi Machi mwaka huu.
Kituo cha uhamishaji wa teknolojia ya kimataifa cha mRNA kilianzishwa mwaka 2021 ili kusaidia watengenezaji katika nchi za kipato cha chini na cha kati kutengeneza chanjo zao wenyewe, kudhibiti, mafunzo na utafiti wa kitabibu.
Mpango huo unaungwa mkono na WHO, Shirika linaloungwa mkono la Umoja wa Mataifa la Medicins Patent Pool na mpango wa ACT-Accelerator/COVAX.
Kando na nchi sita zilizochaguliwa: Misri, Kenya, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia, Rwanda na Tanzania pia zimeonesha nia ya kuanzisha viwanda vyao vya kutengeneza chanjo.
Umoja wa Ulaya, hata hivyo, umeendelea kupuuza wito wa Afrika wa kuondoa haki miliki za chanjo ya COVID-19 kuchagua kuhamisha maarifa badala yake.Kufikia sasa, kulingana na CDC ya Afrika, ni 12.13% tu ya wakazi wa Afrika walio na chanjo kamili na chini ya 1% wamepokea dozi ya nyongeza.














