Chanjo ya Covid-19: Kwa nini mataifa mengi hayajatimiza lengo kuhusu chanjo?

Mwuguzi akitoa chanjo Kampala

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, WHO ilitaka 10% ya watu wawe wamechanjwa kufikia mwisho wa Septemba
    • Author, Na Peter Mwai
    • Nafasi, BBC Reality Check

Mataifa zaidi ya 50 kote duniani hayajafanikiwa kutimiza lengo lililowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) la kuchanja 10% ya raia wake kufikia mwisho wa Septemba.

Mengi ya mataifa haya yanapatikana Afrika, ambapo kwa jumla ni 4.4% ya watu ambao wamechanjwa kikamilifu.

Kiwango hiki ni cha chini mno ukilinganisha na maeneo mengine duniani.

Uingereza, 66% wamechanjwa na katika Umoja wa Ulaya ni 62%, na Marekani ni karibu 55%.

Mataifa gani hayajatimiza lengo la 10%?

Mengi - ingawa si yote - ya mataifa ambayo yemeshindwa kufanya hivyo ni ya kipato cha chini na yametatizika kupata chanjo zenyewe na pia mifumo yao ya afya ni dhaifu.

Baadhi yamekumbwa na migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile Yemen, Syria, Iraq, Afghanistan na Myanmar, na mengine kama Haiti yameathiriwa na majanga ya kiasili. Matatizo haya yanaifanya vigumu kupata na kutoa chanjo kwa raia.

Lakini yapo mataifa kama vile Taiwan, ambalo si taifa maskini vile, lakini ilitatizika kupata chanjo na haikutaka kupata chanjo kutoka China. Kiwango chao ni chini ya 10%.

Pia, Vietnam, ambayo imekuwa na moja ya viwango vya chini zaidi vya maambukizi ya corona duniani, pia ilichelewa kuzindua mpango wa utoaji chanjo, na bado hawajatimiza asilimia 10.

Magari na pikipiki barabarani Hanoi, Vietnam

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chini ya watu 10% Vietnam wamechanjwa

Barani Afrika, mengi ya mataifa hayajatimiza lengo hilo, na ni mataifa 15 pekee ambayo yamefanikiwa kufanya hivyo.

Mengi ni mataifa madogo na ya visiwa kama vile Ushelisheli, Comoro, Mauritius, Cape Verde na Sao Tome & Principe.

Kuna pia mataifa madogo ya bara kama vile Rwanda na Guinea ya Ikweta.

Mataifa mengine ni makubwa na yaliyoendelea kama vile Morocco na Afrika Kusini.

Mchoro wa kuonyesha utoaji wa chanjo

"Mengi ya mataifa haya [ambayo yamechanja kwa kiwango cha juu] ni mataifa ya kipato cha wastani cha juu au kipato cha juu na yalinunua chanjo moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa chanjo," anasema mkuu wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti.

Mataifa mengine makubwa na yenye idadi kubwa ya watu yamebaki nyuma. Misri imechanja takriban 5% ya raia wake pekee, nazo Ethiopia na Nigeria hazijapitisha 3%.

Mataifa mawili barani Afrika - Burundi na Eritrea - bado hayajaanza kutoa chanjo, ingawa Burundi imeeleza nia ya kupokea chanjo kutoka kwa Covax.

Mbona Afrika ikabaki nyuma?

Mataifa ya Afrika yalitegemea ununuzi wa chanjo moja kwa moja, kupokea chanjo kama msaada na pia kupokea chanjo kutoka kwa mfumo wa utoaji chanjo wa Covax unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Mapema mwaka huu, mataifa yalitatizika kupata chanjo kupitia Covax, lakini hali ilianza kuimarika Julai na Agosti.

Mataifa tajiri yalianza kutoa msaada wa chanjo wa Covax - au moja kwa moja kwa mataifa - katika mkutano wa mataifa makuu kiuchumi duniani ya G7 nchini Uingereza mwezi Juni.

Hata hivyo, ni kiwango kidogo cha chanjo zilizoahidiwa ambazo zimetolewa kufikia sasa.

Chanjo za Covax uwanja wa ndege Goma nchini DR Congo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chanjo za Covax zikipakiwa kwenye gari DR Congo

Ahadi zaidi zilitolewa katika mkutano mkuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwezi huu, ambapo Marekani iliahidi kutoa chanjo zaidi 500 milioni za Pfizer.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni kuhusu chanjo za G7 na EU ulionyesha kati ya zaidi ya chanjo bilioni moja zilizokuwa zimeahidiwa, ni 15% pekee zilizokuwa zimetolewa.

WHO ilikuwa awali imekadiria kwamba Afrika ilihitaji takriban chanjo 270 milioni ili kufikisha lengo la kutoa chanjo kwa watu asilimia 10 kufikia mwisho wa mwezi huu.

Kufikia 30 Septemba, bara hili lilikuwa limepokea jumla ya 200 milioni, na hii ina maana kwamba kuna upungufu wa chanjo 70 milioni.

Nini chanzo cha uhaba wa chanjo?

Tatizo kubwa lililoukumba mpango wa Covax - ambao mataifa mengi ya Afrika yalitegemea - ulikuwa ni kutegemea sana chanjo kutoka kwa kampuni ya Serum Institute ya India (SII), kampuni kubwa zaidi ya utengenezaji chanjo duniani.

India ilisitisha uuzaji nje wa chanjo Aprili baada ya kukumbwa na ongezeko kubwa la visa vya corona humo, na watengenezaji wengine wa chanjo walitatizika kuongeza uzalishaji katika kipindi kifupi.

Mataifa tajiri yalikuwa pia yametia saini mikataba ya kununua chanjo zilipokuwa zikiandaliwa mapema kuanzia Julai 2020.

Watengenezaji wa chanjo walilazimika kutimiza mikataba hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wengine.

Hili liliifanya vigumu kwa mpango wa Covax, mpango wa Umoja wa Afrika na hata mataifa binafsi kupata chanjo.

Mapema mwezi huu, Covax ilitoa taarifa na kusema ingepunguza makadirio yake ya chanjo ambazo ilitarajia kupata mwaka huu.

Ilitaja marufuku za uuzaji nje wa chanjo, uwezo wa uzalishaji na kukawia kwa utoaji idhini kwa baadhi ya chanjo kama baadhi ya sababu.

India imetangaza kwamba itarejelea uuzaji nje wa chanjo kuanzia Oktoba, ingawa hawajataja tarehe halisi. India inatarajia kuangazia uuzaji wa chanjo kwa mataifa mengine Asia na kwa Covax ingawa idadi ya chanjo zitakazopatikana pia haijulikani.

"Tunazihimiza nchi, ambazo zinatoa msaada wa chanjo, kutoa chanjo hizo kwa wakati zikiwa hazijakaribia muda wake wa kuisha kutumika," anasema Ayoade Alakija kutoka Muungano wa Utoaji Chanjo wa Umoja wa Afrika.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown, pia ameomba kuchukuliwa kwa hatua za dharura kuhakikisha mamilioni ya chanjo ambazo mataifa yamejiwekea hazitupwi baada ya kupitisha muda wake wa kutumika.

Afrika inahitaji chanjo kiasi gani?

WHO inalenga kuchanja 40% ya watu duniani kufikia mwisho wa 2021.

Lakini Covax tayari imepunguza kiasi cha chanjo ambazo inatarajia kutoa kwa Afrika kufikia wakati huo kutoka 620 milioni hadi takriban 470 milioni.

Hizo zitatosha kuchanja 17% ya watu Afrika, na ina maana kuwa chanjo 500 milioni zinahitajika ili Afrika itimize lengo la 40% kufikia mwisho wa Desemba.

"Kwa viwango na kasi ya sasa, bara hili litaweza tu kutimiza lengo la 40% mwishoni mwa Machi 2022," Matshidiso Moeti kutoka WHO anasema.

Mwuguzi akipewa chanjo Afrika Kusini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwuguzi akipewa chanjo Afrika Kusini

Barani Afrika upo pia wasiwasi wa watu ambao wahataki kuchanjwa.

Ni vigumu kukadiria hili litaathiri kwa kiasi gani mipango ya utoaji chanjo. Lakini utafiti wa hivi majuzi Afrika Kusini ulionyesha viwango vya watu kutokubali chanjo vimekuwa vikishuka kwa jumla miongoni mwa rais, lakini kiwango hicho kilipanda miongoni mwa vijana wa miaka 18-25.

Utafiti zaidi na Becky Dale na Kumar Malhotra

Banner
Reality Check branding