Virusi vya corona: Kuna uhusiano wowote baina ya chanjo na hedhi?

Sodo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya wanawake wamelalamika kuhusu mabadiliko ya mizunguko yao ya hedhi

Kumekuwa na na malalamiko kwa baadhi ya wanawake duniani ambao wamepokea chanjo ya corona kuwa mifumo yao ya hedhi imevurugika.

Malalamiko hayo yanatoka sehemu mbalimbali duniani, kuanzia Marekani mpaka Kenya, Afika Kusini mpaka Uingereza.

Kila mtu katika malalamiko hayo ana upande wake, kuna wale wanaosema kuwa mara baada ya kupokea chanjo mzunguko wao wa hedhi umekuwa ni mrefu kuliko kawaida, wengine wanadai damu ya hedhi imekuwa ikiwatoka kwa wingi kuliko awali na wengine wamelalamikia maumivu makali ambayo hawakuwa wakiyapata awali.

Si wote wanaolalamika. Baadhi ya wanawake wameripoti kuwa mizunguko yao imekuwa mifupi na wengine kudai damu ya hedhi wanayopata baada ya chanjo si nzito sana kama ilivyokuwa awali.

Kuna kundi la mwisho ambao wao wanaripoti kutokuziona kabisa siku zao baada ya kuchanjwa.

Tafiti zinasemaje?

Namna bora zaidi ya kujibu maswali ya kitaalamu kama athari za dawa na chanjo kwa binadamu huwa ni kupitia utafiti wa kina.

Mpaka sasa hakuna utafiti wa kina uliofanyika juu ya jambo hilo kwa hivyo hakuna majibu ya moja kwa moja ya kitafiti.

Lakini suala la mabadiliko ya hedhi limeripotiwa pia kwa wanawake ambao wamekutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Jarida la Health la nchini Marekani linaripoti katika moja ya makala zake mwezi huu kuwa utafiti mdogo uliofanyika Januari mwaka huu na kuhusisha wanawake 233 ambao wapo katika umri wa uzazi na waliokutwa na corona ulibainisha uwepo wa mabadiliko ya hedhi. Wanawake 177 kati yao ambao rekodi zao za hedhi zipo walitoa majibu yafuatayo; asilimia 25 walipata mabadiliko ya wingi wa damu, asilimia 20 wakipata hedhi ya kiwango kidogo kuliko awali na asilimia 19 wakipata mzunguko mrefu kuliko awali.

Je, chanjo nazo zinaweza kuwa na athari kama hizo, bado haifahamiki kwa hakika mpaka sasa.

Wataalamu wanasemaje

AstraZenica ni moja wapo ya chanjo dhidi ya virusi vya corona

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, AstraZenica ni moja wapo ya chanjo dhidi ya virusi vya corona

Licha ya kutokuwa na utafiti, wataalamu wengi wa afya wanaamini kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa chanjo na mabadiliko ya hedhi.

Baadhi ya wataalamu pia wanaamini msongo wa mawazo unaweza pia kuchangia mabadiliko yasiyo ya kawaida ya hedhi na si chanjo.

"Mzunguko wa hedhi unaweza kubalika kutokana na msongo wa mawazo, kukosa usingizi, mazoezi na hata baadhi ya dawa. Hivyo si jambo la kushangaza baadhi ya wanawake kusema mizunguko yao imebadilika baada ya kupata chanjo," Dkt Gloria A. Bachmann, kutoka Shule Kuu ya Tiba ya Rutgers Robert Wood Johnson ya mjini New Jersey ameliambia jarida la Health.

"Nina wasiwasi kuwa watu waovu waliounda uongo huu waliona baadhi ya ripoti za watu kusema wanaona mabadiliko kwenye hedhi zao na kuamua kufanya jambo hilo kuwa sehemu ya kampeni yao ya mtandaoni dhidi ya chanjo," ananukuliwa Dkt Jen Gunter, bingwa wa magonjwa ya wanawake na gazeti la The Guardian la Uingereza.

"Haiwezekani, chanjo ya corona haiwezi kuchochea mabadiliko ya mfumo wa hedhi. Sababu hii ni chanjo na si uchawi," anasisitiza Dkt Gunter.

Unaweza pia kusoma:

Wataalamu wawili kutoka Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani wamechapisha makala yao katika gazeti la The New York Times wakisema hakuna ushahidi kuwa chanjo zinabadili mfumo wa hedhi.

Alice Lu-Culligan na Dkt Randi Hutter Epstein wanasema: "Hata kama kuna uhusiano wa moja kwa moja, mabadiliko ya mara moja ya hedhi si jambo la kushtusha."