Virusi vya corona: Kwanini baadhi ya watu hupata corona kati ya dozi ya kwanza na ya pili ya chanjo

Inachukua takriban siku 14 kwa miili yetu kupata antobodies baada ya kupata chanjo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Inachukua takriban siku 14 kwa miili yetu kupata antobodies baada ya kupata chanjo

Muuguzi Maria Angélica Sobrinho, 53, alikuwa wa kwanza kupata chanjo dhidi ya virusi vya corona katika mji wa Bahia nchini Brazil. Siku chache baadaye, akaanza kuonesha dalili za corona na alipopimwa akapatikana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Sobrinho hakupitia hali hii peke yake. Katika nchi kadhaa duniani, kumeripotiwa visa vya wagonjwa ambao katikati ya siku 21 tangu alipopata chanjo ya kwanza na dozi ya pili, wamepata maambukizi ya virusi vya corona.

Wakati mwingine wanaosambaza taarifa za uongo na dhana potofu katika mitandao ya kijamii wametumia fursa kama hizi na kutangaza kwamba chanjo zinaweza hata kuua.

Hivyobasi, kabla ya kuanza kusambaza taarifa kama hizi ili zianze kukutia hofu, ni muhimu sana kuwa makini na kuelewa kile kinachoendelea.

Sasa je inawezekanaje mtu kupata maambukizi ya ugonjwa wa corona kati ya dozi ya kwanza na ya pili ya chanjo ya corona?

Kinga ambayo bado haijakamilika

Chanjo kadhaa tayari chanjo ambazo zimeanza kutolewa katika nchi mbalimbali zinahiaji mtu kupata dozi mbili kuhakikisha kuwa ana kinga kamili kama vile chanjo ya Pfizer, Oxford / AstraZeneca, Coronavac, Moderna, au Sputnik V.

Kipindi kati ya dozi ya kwanza na nyingine kinatofautiana kulingana na mtengenezaji wa chanjo. Kwa mfano, kampuni ya Pfizer inapendekeza kuwe na siku 21 kati ya chanjo ya kwanza na ya pili huku Chuo kikuu cha Oxford kikipendekeza muda wa miezi mitatu.

Chanjo nyingi zinazotolewa uhitaji dozi mbili ili kupata kinga inayohitajika

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chanjo nyingi zinazotolewa uhitaji dozi mbili ili kupata kinga inayohitajika

"Hakuna chanjo ambayo inaweza kutoa kinga kabla ya siku 14 kupita tangu kuanzia siku ambayo mtu amepata dozi ya kwanza," amesema Dkt. Isabella Ballalai, makamu rais wa chama kinachosimamia chanjo nchini Brazil.

Licha ya teknolojia, chanjo mara nyingi huwa na dutu za antijeni ambazo huwasiliana na mfumo wa kinga na kutengeneza kinga ya mwili inayoweza kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza siku za usoni.

Mchakato huu huchukua muda kukamilika: chembe za kinga zinahitajika kutambua antijeni "kuwasiliana" nazo, na kutengeneza matokeo chanya. Kawaida mchakato huu huchukua wiki mbili.

Hivyobasi, ni muhimu mgonjwa aliyepata dozi ya kwanza ya chanjo kujilinda kwa kuvaa barakoa, kutokaribiana na kunawa mikono mara kwa mara pamoja na hatua zinginezo.

"Kupata chanjo haimaanishi kwamba umepata uhuru wa kuishi maisha kama 'kawaida'. Tunachokifahamu kufikia sasa, chanjo ni kinga dhidi ya athari mbaya za ugonjwa wa corona, lakini kupata chanjo kunaweza kumaanisha kuendelea kueneza virusi kwa wengine," aliongeza Ballalai.

Pia suala la kuwa chanjo itapunguza kusambaa kwa virusi vya corona linachunguzwa na lipo katika hatua za awali.

Hivyobasi, mradi virusi hivyo vinaendelea kusambaa kwa kiwango cha juu na idadi ya waliopata chanjo ni ndogo inapendekezwa kufuatwa kwa sheria zilizowekwa kikamilifu.

Licha ya kupatiwa chanjo , ni muhimu kuendelea kufuata masharti yaliotolewa na serikali

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Licha ya kupatiwa chanjo , ni muhimu kuendelea kufuata masharti yaliotolewa na serikali

Visivyowezekana Kisayansi

Uvumi mwingine uliokuwa unasambaa hivi karibuni uliangazia uwezekano wa chanjo yenyewe kusababisha ugonjwa wa corona.

Lakini Ballalai anasema hili haliwezekani kabisa.

Hii ni dhana potofu ambayo hujitokeza kila mwaka wakati wa kampeni za chanjo dhidi ya virusi.

Mtu akidungwa chanjo

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mtu akidungwa chanjo

"Mtu anayepata chanjo akipata mafua siku chache baada ya kupata chanjo anaanza kuamini kuwa chanjo ndio imesababisha," amesema Ballalai.

Pia, suala linakuwa katika muda uliopo hadi chanjo ianze kutoa kinga. Mradi mfumo wa kinga hautasita kutengeneza kinga, hatari ya kupata maambukizi iko juu.

Chanjo ya corona inatokana na virusi visivyo na nguvu na haviwezi kusababisha ugonjwa mwilini

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chanjo ya corona inatokana na virusi visivyo na nguvu na haviwezi kusababisha ugonjwa mwilini

Mapendekezo

Ni muhimu kujua ni nadra sana chanjo kuwa na athari hasi lakini inaweza kutokea.

"Mtu anaweza kuwa na joto, akawa na wasiwasi au maumivu kidogo," Ballalai ameelezea.

Ikiwa utahisi kwamba hauko sawa siku kadhaa baada ya kupata chanjo, au ukaendelea kuhisi vibaya, ni muhimu kumuona daktari kwa ushauri zaidi.

Inawezekana pengine unavyohisi ni athari za kawaida za chanjo lakini pia kuna dalili za ugonjwa wa Covid-19 na itakuwa vyema kama utaondoa hofu hiyo kwanza.

Kukiwa na zaidi ya dozi milioni 200 za chanjo ya virusi vya corona kote duniani, hadi kufikia sasa hakujakuwa na taarifa za kutia hofu kuhusu chanjo dhidi ya virusi vya corona.