Papa Leo XIV afungua ukurasa mpya wa Kanisa Katoliki


Kikundi cha watawa wakiwa wamevalia rangi ya kijivu wakionekana kufurahia kusikiliza hotuba ya kwanza ya Papa mpya katika uwanja wa St Peter’s mwezi Mei tarehe 8 2025.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watu waliojawa na furaha wakongamana katika uwanja wa St Peter's Square kushuhudia Papa mpya
    • Author, Laura Gozzi
    • Nafasi, BBC News
    • Akiripoti kutoka, Vatican City
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya huzuni ya kifo, huja furaha ya mwanzo mpya.

Jua la mwezi Mei lilikuwa bado linawaka, wakati mgurumo wa ghafla uliposikika katika mitaa iliyozunguka uwanja wa St Peter's.

Katika mitaa iliyozunguka uwanja huo, watu waliokuwa wakisubiri kwa hamu walishtuka, kisha wakichungulia simu zao.

Ghafula, wakaanza kukimbia wakielekea Vatican.

"Moshi mweupe! Wanasema moshi mweupe!" walishangilia kwa msisimko.

Walipowasili uwanjani, ukungu mweupe ulikuwa bado unafuka upande wa kushoto wa Jumba la Kitume- mahali ambapo makadinali 133 walikuwa wamefungiwa tangi siku iliyotangulia wakishiriki mchakato wa kumchagua mkuu mpya wa Kanisa Katoliki.

Jua la jioni lilipokuwa likimulika sanamu za mitume juu ya paa la Kanisa Kuu la St Peter's , mlio wa kengele ulisikika.

Vijana na wazee waliruka kwa furaha huku kundi la watawa likishikana kwa mbwembwe na kuonyesha mwanzo mpya kwa wanahabari waliokuwa wakinasa tukio hilo la kihistoria.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Haijatimia hata wiki tatu tangu Papa Francis alipowabiriki waumini kutoka roshani ile ile ya kanisa hilo kuu.

Alhamisi hii, kumbukumbu yake ilikuwa imetanda uwanjani; karibu kila mtu aliyeulizwa alimtaja Francis, akisisitiza umuhimu wa Papa Mpya kufuata nyayo zake.

" Tumeingia leo tu kutoka Marekani," alisema Amanda, raia wa Marekani, alipokuwa akizungumza na BBC.

" Hili ni jambo la kipekee ni kama baraka.Tulikuja kwa ajili ya mchakato huu, na sasa limetimia".

Hii ni miadi ya Kimungu!" alitania kwa furaha.

Wanawake wawili waliokuwa na umri wa miaka ishirini walieleza kuwa walijiskia kububujikwa na machozi.

" Ni wakati wa kihistoria, wa ajabu sana," mmoja wao alisema, akiongeza kuwa anatumai Papa mpya atakuwa "angalau bora kama mtangulizi wake".

Kauli hii iliungwa mkono na wengi waliokuwa wakisubiri tangazo rasmi la Papa mpya, kabla ya kutangazwa kwa Papa Leo wa XIV.

"Hatujali anatoka nchi gani, ilimradi afuate nyayo za Francis na kuendeleza umoja miongoni mwa Wakatoliki wote," alisema mama mmoja wa Kifaransa aliyekuwa akiwaongoza watoto wake watano kusogea mbele zaidi ya uwanja.

Kijana mdogo akiwa amevaa shati ya njani na suruali ya hudhurungi akiwa amesimama juu ya bega la babake.
Anapeperusha bendera ya Ufaransa katuka uwanja wa St Peters baada ya kutangazwa kwa Papa mpya.

Wakati Dominique Mamberti, dikoni mkuu, alipojitokeza kwenye roshani kutangaza hotuba maarufu ya Habemus Papam, uwanja ulikuwa umefurika.

Kimya kilitanda mara jina la Robert Francis Prevost lilipotajwa.

Wale waliomjua huenda walimtambua mapema kama mmoja wa wagombea kadinali mzaliwa wa Chicago mwenye umri wa miaka 69, ambaye aliwahi kuwa mmishonari nchini Peru kabla ya kufanywa askofu.

Hata hivyo, wengi waliokuwa uwanjani walionekana kuchanganyikiwa mwanzoni, hasa kwa kuwa mitandao ya simu haikufanya kazi.

Hivyo, sura ya kwanza waliyoipata ya Papa Leo wa XIV ilitegemea kabisa namna alivyojitambulisha alipojitokeza kwenye roshani yenye mapambo mazito.

Alionekana kuguswa kihisia, akiwa amevalia mavazi ya kipapa ya rangi nyeupe na nyekundu.

Akizungumza kwa Kiitaliano kilichojaa ujasiri, japo kwa lafudhi ndogo, alisoma hotuba ndefu kuliko ile fupi aliyowahi kutoa Papa Francis mwaka 2013.

"Ningependa salamu hii ya amani iwafikie nyote mioyo yenu, familia zenu, na watu wa ulimwengu mzima. Amani iwe nanyi," alianza kusema kwa sauti ya utulivu.

Maneno yake yalikatizwa mara kwa mara na makofi ya shangwe, hasa alipotaja neno "amani," ambalo alilitamka mara tisa. Alimtaja pia Francis kwa heshima kubwa.

Sehemu ya hotuba aliyotoa kwa Kihispania, akimkumbuka kwa hisia muda aliotumia Peru, ilishangiliwa na makundi ya Waamerika Kusini waliokuwepo uwanjani.

Alisisitiza umuhimu wa umoja wa Kanisa, na mwishoni akaomba kila mtu aungane naye katika sala. Alipoanza kusoma Ave Maria, milio ya sauti za pamoja ilisikika uwanjani, watu wakisali kwa lugha mbalimbali kulingana na imani zao.


Wanandoa Juan na Carla kutoka Barcelona wakikumbatiana katika uwanja wa St Peter’s kushuhudia uchaguzi wa Papa mpya.
Maelezo ya picha, Carla na Juan wanasema ni zaira yao ya kwanza katika eneo la Vatikani.

Muda mfupi baadaye, watu walianza kutoka uwanjani polepole.

Wanandoa wachanga walikumbatiana kwa furaha, nyuso zao zikimulika.

"Bado nahisi msisimko," alisema Carla kutoka Barcelona.

"Nguvu ya tukio hili inaridhisha, ni ya kushangaza. Hii ni mara yetu ya kwanza kufika hapa," alisema Juan kutoka Ecuador.

Alipoulizwa matumaini yake kwa Papa mpya, alisema: "Natumaini Roho Mtakatifu atamwongoza, ili sisi sote tuweze kuunganishwa."

Gemma, mkazi wa Roma, alisema hakuwahi kusikia jina la Robert Prevost hadi alipoliona kwenye mtandao wa Instagram asubuhi hiyo.

"Watu walionekana hawajakubali haraka," aliongeza rafiki yake Marco.

"Kama angekuwa Muitaliano, watu wangepokea kwa furaha zaidi." "Lakini bado ilikuwa jioni ya kipekee, tukio la kuvutia," alisema Gemma.

"Hii ilikuwa tukio la kwanza la uchaguzi wa Papa kuhudhuria mara yangu ya kwanza.

Na Papa huyu mpya ana miaka 69 tu, kwa hiyo nani ajuaye ni lini kutakuwa mwingine?"

Uwanja ulianza kutulia.

Migahawa iliyo karibu na Vatikani ilijaa mahujaji, makasisi, na watalii. Wapenzi walipiga picha za mwisho mbele ya basilika.

Ndani ya Jumba la Kitume, ambalo sasa lilikuwa limefunguliwa tena, Robert Prevost alisalia kwa muda wa sala ya faragha.

Kisha, kwa mara ya kwanza, akaingia tena ndani ya Kanisa la Sistine kama Papa Leo wa XIV, Papa wa 267 wa Kanisa Katoliki.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid