Fahamu uwezo mkubwa wa Papa kote duniani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa Francis na Barack Obama, Rais wa wakati huo wa Marekani, walipotembelea Washington mwaka 2015.
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Vatican, zaidi ya watu bilioni 1.4 duniani ni Wakatoliki. Hii inawakilisha takriban 17% ya idadi ya watu kote duniani.

Kwa hivyo haishangazi kwamba Papa Francis, ambaye alifariki Aprili 21 na ambaye mazishi yake yalifanyika Jumamosi, Aprili 26, alivutia umati mkubwa wa watu wakati wa safari yake ya 2024 huko Asia, na karibu nusu ya wakazi wa Timor-Leste walihudhuria Misa nchini humo.

Mwaka uliotangulia, zaidi ya watu milioni moja walistahimili jua kali kuhudhuria misa katika uwanja wa ndege wa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, wakati wa ziara yake katika nchi mbili za Afrika.

Uwezo wa kuleta pamoja watu wengi—na ibada hiyo—ni ishara moja tu ya ushawishi wa kudumu wa Papa na Kanisa Katoliki duniani.

Papa anaongoza sio tu waumini wa Kikatoliki, bali pia Jimbo la Vatican City na baraza lake linaloongoza, Holy See. Holy See inachukuliwa kuwa chombo huru chini ya sheria za kimataifa.

Hii inamaanisha, anashiriki rasmi katika masuala ya kimataifa na kudumisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na nchi 184 na Umoja wa Ulaya.

Nafasi ya Papa kama mkuu wa nchi na serikali, pamoja na kiongozi wa kiroho wa waumini zaidi ya bilioni moja, inamfanya kuwa mmoja wa viongozi wa kidini wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakatoliki waliovalia mavazi ya kitamaduni ya Kijava wakijiandaa kwa maandamano ya Misa ya Krismasi.

Holy See ina hadhi ya uangalizi wa kudumu katika Umoja wa Mataifa, ambapo imehakikishiwa kiti katika moja ya meza za maamuzi zenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ingawa Holy See hana haki ya kupiga kura, anaweza kushiriki katika mikutano na kushawishi mijadala.

Mwaka wa 2015, kwa mfano, kabla ya kusainiwa kwa Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris, Papa Francis alikosoa kile alichokiita "kutojali kwa kiburi" kwa wale wanaoweka masilahi ya kifedha juu ya juhudi za kuokoa sayari.

Muundo na muda wa uingiliaji kati huu ulionekana kuwa wa manufaa hasa kwa nchi za Kusini mwa Ulimwengu.

Mapema mwaka wa 2024, Holy See ilizuia mijadala kuhusu haki za wanawake katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, kufuatia mkwamo wa masuala ya jinsia na ujinsia.

Makubaliano ya ajenda yalijumuisha msaada wa kifedha kwa wanawake katika mstari wa mbele wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Vatikani, pamoja na Saudi Arabia, Urusi, Iran, na Misri, walielezea wasiwasi wao kwamba maandishi hayo yanaweza kujumuisha wanawake waliobadili jinsia na kutaka marejeleo ya wanawake wasagaji kuondolewa.

Licha ya ukosoaji huo mkali, kipindi hicho kiliangazia uwezo wa Kanisa kuathiri makubaliano ambayo yanaathiri moja kwa moja maisha ya mamilioni ya watu.

Makubaliano ya mwaka 2014 ya kurekebisha uhusiano kati ya Marekani na Cuba ni mfano mwingine wa mafanikio ya diplomasia ya upapa. Marais wa wakati huo Barack Obama na Raúl Castro walimshukuru hadharani Papa Francis kwa kufanikisha mchakato huo.

Francis aliandika barua kwa wote wawili na kufanya mkutano wa siri huko Vatican ili kuwezesha ukaribu-ingawa Marekani ilikataa sehemu za makubaliano chini ya Donald Trump.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa Francisko katika "gari lake la papa" katikati ya umati wa Wakatoliki huko Timor Mashariki baada ya kuadhimisha Misa nchini humo wakati wa ziara yake mwaka 2024.

Lakini ni mchango wa Kanisa katika demokrasia katika miongo ya hivi karibuni unaowakilisha mafanikio yake makubwa zaidi, kulingana na Profesa Daved Hollenbach wa Kituo cha Berkley cha Dini, Amani na Masuala ya Dunia nchini Marekani.

Baraza kuu la Pili la Vatikan katika miaka ya 1960, ambapo Kanisa lilipitia kwa kina mafundisho na miongozo yake, liliashiria kujitolea kutetea haki za binadamu na uhuru wa kidini, ambao Hollenbach anauita "hatua muhimu mbele."

Profesa huyo anataja kazi ya mwanasayansi wa siasa Samuel Huntington, kulingana na "wakati wa papa wa Yohane Paulo II, hadi mwanzo wa papa wa Francis, robo tatu ya nchi ambazo zilihamia kutoka kwa mamlaka hadi demokrasia zilikuwa na ushawishi mkubwa wa Kikatoliki."

"Yote yalianza na mabadiliko ya Uhispania na Ureno mbali na serikali za Franco na Salazar, na kisha kuenea hadi Amerika ya Kusini.

Kisha ilifikia nchi kama Ufilipino na Korea Kusini, ambapo pia kuna uwepo mkubwa wa Wakatoliki," Hollenbach anaelezea, akimfafanua Huntington.

Kulingana na yeye, hatua za Papa John Paul II zilisaidia kufungua njia ya demokrasia katika nchi yake ya asili ya Poland na "hatimaye ilichangia kuanguka kwa Umoja wa Kisovyeti na kuenea kwa demokrasia katika sehemu mbalimbali za himaya yake ya zamani."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sherehe za kufunga Mtaguso wa Pili wa Vatikani huko Roma mnamo 1965

Miba ya kisiasa

Hata hivyo, Vatikan haifanikiwi siku zote kuwashawishi viongozi wa ulimwengu.

Wakati Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance – yeye mwenyewe Mkatoliki – alipotumia hoja za kitheolojia kuhalalisha sera ya serikali ya uhamiaji, Papa aliandika barua butu akitukumbusha kwamba Yesu pia alikuwa mkimbizi.

"Mfalme wa mpaka" wa Marekani Tom Homan, pia Mkatoliki, alijibu: "Papa anapaswa kurekebisha Kanisa Katoliki."

Mnamo 2020, Rais wa wakati huo wa Brazil Jair Bolsonaro pia alimshambulia papa baada ya kutetea ulinzi wa Amazon. "Papa anaweza kuwa wa Argentina, lakini Mungu ni wa Brazil," Bolsonaro alisema.

Ushawishi wa kijamii wa Kanisa umepungua huko Uropa, huku wengi wakisema kwamba misimamo yake ya kihafidhina kuhusu haki za LGBT+, upangaji mimba, na uavyaji mimba haiendani na karne ya 21. Kukataa kwa Fransisko kuwaruhusu wanawake kushika nyadhifa fulani za uongozi, kama vile makuhani na mashemasi, ni ishara nyingine ya hili.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa John Paul II anakutana na Rais wa Soviet Mikhail Gorbachev huko Vatican mnamo 1990

Katika Amerika ya Kusini, ingawa Kanisa Katoliki bado lina nguvu kubwa, mvutano wake ulikuwa mkubwa zaidi. Kanisa lilikuwa na jukumu muhimu katika kutunga sheria zinazozuia utoaji mimba katika eneo hilo, lakini katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, nchi kama vile Uruguay, Mexico, Argentina, na Colombia zimepanua ufikiaji wa utaratibu huo, kwenda kinyume na mafundisho ya Kikatoliki.

Ukuaji wa Ukristo wa kiinjilisti pia unatishia ushirika wa kanisa na mamlaka ya kisiasa.

Nchini Brazili, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Wakatoliki duniani, wachambuzi fulani wanatabiri kwamba baada ya miaka mitano tu, Ukatoliki utakoma kuwa dini iliyo ya wengi zaidi.

Zaidi ya hayo, ufichuzi unaoendelea wa unyanyasaji wa kijinsia wa makasisi—na jukumu la Kanisa katika kuufunika—umeharibu sifa yake kote duniani.

Licha ya hayo, mkuu wa Kanisa Katoliki anaendelea kuwa na ushawishi ambao viongozi wengine wachache duniani wanao. Hii ni kwa sababu papa ndiye mkuu wa tawi kubwa la Ukristo na mkuu wa serikali.

Kuanzia kubusu miguu ya wababe wa vita nchini Sudan Kusini hadi kuwafariji wahamiaji katika kambi za wakimbizi nchini Ugiriki, hatua za papa—na jukumu la Kanisa Katoliki—zinaendelea kuunda mijadala ya kimataifa.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi