Mambo matano yaliyobadilisha sura ya Kanisa Katoliki chini ya Papa Francis

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 11

Wakati Muargentina Jorge Bergoglio alipochaguliwa kuwa mrithi wa Papa Benedict XVI mnamo Machi 13, 2013, taswira ya Kanisa Katoliki ilikuwa imetatizwa na mfululizo wa kashfa za ufisadi, unyanyasaji, na migogoro ya ndani.

Matarajio makubwa yalikuwa kwa Papa mpya.

Lakini kulikuwa na tatizo: Bergoglio alichaguliwa akiwa na umri wa miaka 76, mwaka mmoja zaidi ya umri ambao kwa kawaida maaskofu hujiuzulu. Wengi, akiwemo yeye mwenyewe, waliamini kuwa kipindi chake cha upapa kingekuwa kifupi.

Tangazo la kifo chake Jumatatu, Aprili 21, akiwa na umri wa miaka 88, lilihitimisha miaka 12 ya uongozi kutoka Vatican.

"Saa 1:35 leo asubuhi (kwa saa za hapa), Askofu wa Roma, Francisco, amerejea nyumbani kwa Baba. Alijitolea maisha yake yote kwa huduma ya Bwana na Kanisa lake," ilitangaza Vatican.

Unaweza pia kusoma

Licha ya umri wake, alifanya kazi bila kuchoka kueneza ujumbe wa Kanisa, akipokea viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii huko Vatican na kusafiri hadi zaidi ya nchi 60.

Kwa mtindo wake wa ubunifu, asili yake ya upole na unyenyekevu, pamoja na mipango yake ya mageuzi, jarida la Time lilimtaja kuwa "Mtu muhimu katika Mwaka" mnamo 2013.

Hata hivyo, wakati wa kipindi chake cha upapa alipokea pia ukosoaji mkali kutoka kwa makundi ya kihafidhina, ambao walipingana naye, na kutoka kwa makundi ya mageuzi zaidi, ambao hawakuridhika na mabadiliko yake.

Hapa tunakueleza mafanikio makubwa matano ya Papa Francisc; alichofanikiwa kubadilisha na ambayo hayakubadilika ndani ya Kanisa Katoliki.

1. Papa wa Kwanza Kutoka Amerika ya Kusini

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kama Muargentina halisi, Papa Francisco hakuwahi kuacha mapenzi yake kwa kandanda, na hasa kwa timu yake pendwa, San Lorenzo.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Papa Francisco alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kutoka nchi ya Amerika ya Kusini – na kwa hakika, wa kwanza kutoka bara lote la Amerika na nusu ya kusini ya dunia.

Hii ilikuwa hatua ya kihistoria na ishara ya wazi ya mabadiliko ya kieneo ndani ya Kanisa Katoliki.

Katika mwaka 1910, karibu theluthi mbili ya Wakatoliki wote duniani walikuwa barani Ulaya. Lakini kufikia 2022, takriban nusu (asilimia 48) ya Wakatoliki wako Amerika, huku asilimia 28 wakiwa Amerika ya Kusini, kwa mujibu wa Ofisi Kuu ya Takwimu za Kanisa.

Uteuzi wa Francisco uliakisi mabadiliko haya makubwa, ukileta sauti ya bara lililo na idadi kubwa ya waumini lakini lililokuwa limekuwa pembezoni kwa muda mrefu.

Asili yake kama Mlatino ilichangia mtindo wake wa uongozi wa karibu na wa kibinadamu—akiwa na tabasamu, unyenyekevu, na ucheshi uliomfanya awe mtu wa watu. Mtindo huu wa mawasiliano uliathiri si tu namna Kanisa linavyozungumza na dunia, bali pia nafasi yake katika siasa za kimataifa.

Kwa mfano, alikuwa mhusika muhimu katika upatanisho wa kihistoria kati ya Marekani na Cuba, uliosaidia kufufua uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo.

Mwaka 2015 alitembelea Cuba na kukutana na Fidel Castro – tukio la kihistoria lililoonyesha nafasi mpya ya Kanisa katika diplomasia ya kimataifa.

Na huo haukuwa mwisho wa safari zake Amerika ya Kusini.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wakati wa kipindi chake cha upapa, Papa Francisco alitembelea nchi kadhaa za Amerika ya Kusini.Picha hii alikuwa katika ziara Peru.

Ziara ya kwanza ya Papa Francisco nje ya Italia kama Kiongozi wa Kanisa Katoliki ilikuwa nchini Brazil, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Wakatoliki duniani. Hii ilikuwa mnamo Julai 2013, kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani (World Youth Day) – tukio lililoashiria mwanzo wa uhusiano wake wa karibu na Amerika ya Kusini kama Papa.

Baadaye, alitembelea pia Bolivia, Chile, Ecuador, Mexico, Paraguay, na Peru, akijitokeza kama mtetezi wa haki za jamii, wanyonge, na mazingira – hasa maeneo ya Amazon.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba hakuitembelea Argentina, nchi yake ya nyumbani, katika kipindi chote cha miaka 12 ya upapa wake. Hili lilizua maswali mengi na hata kukatisha tamaa baadhi ya wananchi, hasa wakati taifa hilo lilipokuwa likikumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi uliosababisha ongezeko kubwa la umasikini – hasa kwa watoto.

Kwa mujibu wa Gustavo Vera, rafiki wa karibu wa Bergoglio na mwanaharakati dhidi ya kazi za utumwa na usafirishaji haramu wa binadamu, Papa Francisco aliepuka kurejea nyumbani ili kutojikuta katikati ya mgawanyiko mkubwa wa kisiasa unaogawa taifa hilo. Hii ilikuwa njia ya kuzuia Kanisa kuonekana kama kinara wa upande wowote wa kisiasa.

Licha ya kutokuwepo nchini mwake, mtazamo wake kutoka Kusini mwa dunia ulileta mabadiliko makubwa ya kimfumo ndani ya Kanisa. Kama alivyosema Gerard O'Connell, mwandishi wa habari wa Vatican kutoka Ireland:

"Alileta utajiri mpya – njia tofauti ya kukabiliana na masuala ya kimaadili na ndani ya Kanisa zima. Na naamini yeye ndiye wa kwanza wa kizazi kipya kitakachotiririsha uvuvio mpya kutoka maeneo yenye idadi kubwa ya Wakatoliki."

2. Papa wa Kwanza wa Kijesuiti (Jesuit)

Papa Francisco alikuwa mwanachama wa kwanza wa Shirika la Yesu (Jesuit) kuongoza Kanisa Katoliki, na hili lilikuwa jambo la kihistoria. Wajesuiti ni waumini wa kiroho wenye msisitizo mkubwa juu ya elimu, utume wa kupatanisha, na haki za kijamii, na upendo wao kwa maskini na walioachwa nyuma umejidhihirisha katika maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, mtindo huu wa maisha ya kujitolea na kupigania haki za kijamii ulikuwa na shaka kubwa kutoka kwa baadhi ya makundi ya kihafidhina ndani ya Vatican, kwa sababu unaleta mtazamo wa mabadiliko kutoka kwa maadili ya jadi.

Kwa kuingia kwa Papa Francisco, mtindo wa maisha wa unyenyekevu ulionekana wazi, ukiwa kinyume na anasa ambazo zimekuwa sehemu ya mtindo wa upapa wa zamani.

Tangu siku ya kwanza, aliweka alama yake kwa kutumia maisha ya unyenyekevu, akionyesha wazi kuwa alijivunia asili yake ya Jesuiti.

Alikataa matumizi ya gari ya kifahari ya Kipapa na badala yake kushirikiana na makardinali wengine kwenye basi lililowachukua nyumbani. Hii ilikuwa ni ishara ya kuonyesha hali ya usawa, sio tu kwa viongozi wa Kanisa bali pia kwa waumini wa kawaida.

Chaguo la jina la "Francisco" pia lilikuwa na maana ya kiroho, likihusisha na Mtakatifu Francis wa Assisi, ambaye alijulikana kwa upendo wake kwa maskini, wanyama, na mazingira.

Hii ilikuwa ni ishara ya kuendeleza lengo la Papa Francisco la kuwa na "Kanisa maskini na kwa ajili ya maskini," na kuonyesha dhamira yake ya kimaadili.

Makazi ya Papa Francisco pia yalijitokeza kama mfano wa unyenyekevu. Alikataa kuishi katika kasri la Kipapa na badala yake alihamia katika makazi ya Santa Marta, eneo jirani, na kuishi katika nyumba ndogo ya mita 40 za mraba. Hii ilikuwa ni ishara nyingine ya upendeleo wa maisha ya kawaida na usawa kwa waumini wa kawaida.

Ziara yake ya kwanza rasmi kama Papa ilikuwa Lampedusa, kisiwa cha Italia kinachopokea wahamiaji wengi kutoka pwani ya Afrika kila mwaka. Hii ilikuwa ni ishara ya kukipongeza kwa jitihada za kupigania haki za wahamiaji na kuwa na utamaduni wa upatanisho na kuhudumia wanyonge.

Papa Francisko alianzisha miradi ya kutoa makazi, huduma za afya, na chakula kwa maskini wa Roma, na hata alionekana akitembea mitaani usiku, akigawa chakula kwa watu maskini. Huu ni mfano wa upendo wa kweli kwa maskini, na mabadiliko ya mtindo wa upapa ambao haujashuhudiwa hapo awali.

,,

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa Francisko alikubali na kuendeleza utamaduni wa kuosha miguu ya waumini ambao ulikuwa umeanzishwa na Papa Yohane Paulo II na kuendelea na Papa Benedict XVI.

Katika muktadha wa unyenyekevu na mageuzi, Papa Francisko alifanya juhudi kubwa ya kuleta uwazi katika hesabu za kifedha za Kanisa, jambo ambalo lilikuwa linakosekana kwa muda mrefu.

Hii ilikuwa ni hatua muhimu ili kurejesha imani ya waumini kwa Kanisa, ambalo limekuwa likikumbwa na tuhuma za utumiaji vibaya wa fedha katika historia yake.

Sambamba na hatua hii, pia alitaka kufanya hesabu za kihistoria za Kanisa kuwa wazi.

Kwa mfano, Februari 2014, alianzisha Sekretarieti ya Uchumi ili kusimamia fedha za Holy See. Mwezi mmoja tu mapema, kasisi mmoja wa cheo cha juu wa Italia alikuwa ameshtakiwa kwa ufujaji wa mamilioni kupitia Benki ya Vatican.

Lakini si kila kitu kilikuwa chanya kwa Wajesuti wakati wa upapa wa Francis.

Nchini Chile, nchi ambayo Wajesuti wamekuwa na ushawishi mkubwa kupitia taasisi zao za elimu, misingi, na wafuasi katika nyadhifa za juu za kisiasa, kutaniko hilo limekuwa kitovu cha kashfa nyingi katika miaka ya hivi karibuni, ambazo kimsingi zinahusishwa na unyanyasaji wa kijinsia.

Mazungumzo na dini nyingine

Papa Francisco alifungua Kanisa kwa dunia kwa njia ambazo hakuna Papa mwingine aliyewahi kufanya, kama alivyoandika Mathew Schmalz, profesa wa masomo ya dini katika cguo cha Holy Cross nchini Marekani.

Uongozi wake ulijikita katika maelewano kati ya dini tofauti, na juhudi zake ziliweka msingi mpya wa mazungumzo ya kidini kwa heshima na mshikamano.

Papa alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na viongozi wa dini nyingine, akiwemo wa Kiislamu na Kiyahudi, akilenga kuondoa hofu, chuki, na migawanyiko ya kidini.

Moja ya matukio muhimu kabisa yalikuwa ni kusaini Hati ya Udugu wa Kibinadamu na Imamu Mkuu wa Al-Azhar, Ahmed al-Tayeb, huko Abu Dhabi mnamo 2019. Hati hiyo ilihimiza amani, maelewano, na kuishi kwa pamoja kati ya watu wa dini tofauti, ikiwa ni hatua ya kihistoria katika uhusiano kati ya Uislamu na Ukristo.

Katika safari yake ya kihistoria nchini Iraq mwaka 2021, Papa Francisco alikutana na Ayatollah Ali Al Sistani, kiongozi mkuu wa Kishia.

Katika mkutano huo, Papa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na urafiki kati ya jumuiya za kidini, akisema kuwa kwa kukuza mazungumzo yenye kuheshimiana, dini zinaweza kuchangia amani na ustawi wa Iraq, eneo zima la Mashariki ya Kati, na dunia nzima.

Papa Francisco pia alikuwa msemaji wa wazi dhidi ya chuki na dhuluma zinazofanywa kwa misingi ya kidini. Baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa na watu wanaojinasibisha na Uislamu, aliweka wazi kuwa si sahihi kuuhusisha Uislamu wote na vurugu:

"Nikiongea kuhusu vurugu za Kiislamu, lazima pia nizungumzie vurugu za Kikatoliki," alisema, akisisitiza kuwa ukatili hauhusiani na dini bali na watu binafsi wenye misimamo mikali.

Vivyo hivyo, alipinga vikali mashambulizi dhidi ya Wayahudi, akiyaita "dhambi dhidi ya Mungu." Alikutana na viongozi wa jumuiya za Kiyahudi katika nchi nyingi duniani, akisisitiza maridhiano na kumbukumbu ya pamoja ya historia ya mateso na maumivu.

Kupitia juhudi hizi, Papa Francisco aliweka Kanisa katika mstari wa mbele wa mazungumzo ya amani duniani, akibadilisha mtazamo wa Kanisa kutoka kuwa taasisi iliyojifungia ndani hadi kuwa daraja la maelewano kati ya imani mbalimbali.

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Francis akiwa na Ahmed al-Tayeb mnamo 2022.

4. Alipendelea ujumuishaji

Kulingana na Francis, "Kanisa halifungi milango yake kwa mtu yeyote," na haipaswi kufanya "kuingilia kiroho" katika maisha ya kibinafsi, kwa sababu "Mungu, katika uumbaji, ametuweka huru."

Kwa maana hii, alikuwa Papa wa kwanza kuruhusu Wakatoliki waliotalikiana kupokea komunyo.

Na pengine msemo mashuhuri zaidi wa upapa wake ulikuwa: "Ikiwa mtu ni mpenzi wa jinsia moja, anamtafuta Bwana, na ana nia njema, mimi ni nani niwahukumu?"—akirejelea hasa makuhani waliokuwa wapenzi wa jinsia moja, lakini pia wanachama wote wa jumuiya ya LGBT kwa ujumla.

Francis hata alionyesha uwazi kuelekea vyama vya kiraia vya watu wa jinsia moja, akiwaidhinisha makasisi kuwabariki wapenzi wa jinsia moja na kuthibitisha kwamba wana haki ya kuunda familia.

Haya yote yaliwakilisha ahueni kubwa, ikizingatiwa kwamba mtangulizi wake, Papa Benedict XVI, aliamini kwamba ushoga ulikuwa na "uovu wa kimaadili wa asili."

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, "Ikiwa mtu ni mpenzi wa jinsia moja na anamtafuta Mungu na ana nia njema, mimi ni nani nimhukumu?" Francis alisema mwaka 2013.

Hata hivyo, Francis pia alishikilia kuwa ndoa za watu wa jinsia moja hazipaswi kuchukuliwa kuwa ndoa. Hilo, alisema, lingekuwa "jaribio la kuharibu mpango wa Mungu."

"Kanisa limegawanyika kwa miongo kadhaa kati ya mila, ya kihafidhina ambayo haitaki mabadiliko ya aina yoyote, na sekta ambayo inalia mageuzi, hasa katika jamii za mashinani," Vicens Lozano, mwandishi na mwanahabari ambaye ameangazia Vatican kwa zaidi ya miongo minne, anaeleza BBC Mundo.

"Papa alijaribu kutokuza migawanyiko hii, lakini alifanya mabadiliko muhimu: alikuwa Papa wa kwanza wa mazingira katika historia na wa kwanza kuwakaribisha watu wa jinsia moja," anabainisha Lozano, mwandishi wa "Vaticangate" na "Intrigues and Power in the Vatican."

Kuhusu masuala ya ngono, Francis alishikilia fundisho la Kikatoliki linaloruhusu tu matumizi ya njia asilia za uzazi wa mpango, kama vile useja na kujizuia.

Lakini aliunga mkono mjadala kuhusu suala hilo, akikiri kwamba kondomu ni njia madhubuti ya kuzuia virusi kama UKIMWI na Zika.

Hakuwa na msimamo kuhusu uavyaji mimba na useja wa kipadre.

Mojawapo ya maeneo ambayo alikosolewa sana ni jinsi alivyoshughulikia suala kubwa alilokabiliana nalo wakati wa upapa wake: shutuma za unyanyasaji wa kingono na washiriki wa Kanisa.

Aliahidi "kutofanya juhudi zozote" kuwafikisha mapadre wenye dhuluma na maaskofu ambao walificha uhalifu wao mbele ya sheria. Hata hivyo, makundi ya walionusurika yalimshutumu kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuwahifadhi makasisi walioshutumiwa.

"Francis alipigana dhidi ya 'utamaduni wa kutokujali' ndani ya Kanisa, kama alivyoiita. Alifanya mengi: alipanga kundi zima la wachunguzi kufanya kazi huko Vatican juu ya suala la unyanyasaji wa kijinsia na kuwafukuza makasisi wengi kwa sababu hiyo," anasema Lozano.

Mwandishi huyo wa habari anaamini kwamba ukosoaji alioupata Papa ulitokana na matarajio yasiyo halisi ambayo wengi walikuwa nayo.

"Mtazamo wa watu ni kwamba hakuna kilichokuwa kikifanyika na kila kitu kilikuwa kikienda polepole... lakini ndivyo ilivyo Vatican," anasema.

...

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Papa alichagua wanawake katika nyadhifa za uongozi

Nafasi ya wanawake

Kuanzia Dini ya Kiyahudi iliyorekebishwa hadi matawi yenye maendeleo zaidi ya Uprotestanti, dini nyingine zimeruhusu wanawake kupanda kwenye madhabahu.

Hata hivyo, Francis alishikilia mila ya Kikatoliki na kupinga kuwekwa wakfu kwa wanawake kama makasisi, akisema ni "tatizo la kitheolojia."

Anne Tropeano, mmoja wa wanawake zaidi ya 200 waliotawazwa kote ulimwenguni katika uasi dhidi ya Vatican, aliiambia BBC mwaka wa 2022: "Kanisa linafundisha kwa matendo yake kwamba ni sawa kuwatenga wanawake. Wanawake wanajifunza hili, wavulana na wasichana wanajifunza hili, wanaume wanajifunza hili ... na kisha wote wanaenda ulimwenguni na kuishi kwa sheria hii."

Hata hivyo, kulingana na Schmalz, Papa "alifanya mabadiliko makubwa ambayo yalifungua majukumu kadhaa ya uongozi kwa wanawake."

"Francis alikuwa papa wa kwanza kumteua mwanamke kuongoza ofisi ya utawala katika Vatican. Pia kwa mara ya kwanza, wanawake walijumuishwa katika baraza la wanachama 70 linalochagua maaskofu na katika baraza la wanachama 15 linalosimamia fedha za Vatican. Alimteua mtawa wa Kiitaliano, Raffaella Petrini, kuwa rais wa Jiji la Vatican," alisema.

Aidha, mwezi Januari alimteua Simona Brambilla kuwa Mkuu wa Vatican, na kuwa wa kwanza katika historia.

"Kuwa na mwanamke mahali ambapo palikuwa na kardinali ni mapinduzi (...). Mahali ambapo makadinali wanatoka ni mapinduzi. Papa ambaye anazungumza kinyume na mfumo na kusema uchumi huu unaua ni mapinduzi," mwanatheolojia wa Argentina Emilce Cuda aliiambia BBC mwaka 2023, katika kipindi maalum kilichotajwa hapo juu kama kumbukumbu ya Papa Francis.

Kwa Schmalz, "upapa wa Francis umekuwa wa kihistoria": "Haukuongeza tu kujitolea kwa Kanisa Katoliki kwa maskini, lakini pia kupanua ambao wamejumuishwa katika kufanya maamuzi."

Lozano anakubali: "Francis alikuwa mwanamapinduzi kwa sababu alimpa papa hali tofauti, ambayo ilikoma kuwa utawala wa kifalme na kuwa kiongozi wa maadili na maadili wa karne ya 21, karne ambayo tunakosa sana aina hii ya viongozi duniani."

Na anaongeza: "Yeye ni Papa ambaye amesikiliza jamii za vijijini na kupanda mbegu kwa ajili ya mageuzi ya kina ya Kanisa katika siku zijazo."

Unaweza pia kusoma