Wagner: Mali yasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Mali inasema imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine, baada ya afisa wa kijeshi kusema kuwa Kyiv ilihusika katika mapigano makali karibu na mpaka wa Algeria mwezi uliopita.
Makumi ya wanajeshi na mamluki wa Mali kutoka kundi la Wagner la Urusi waliuawa katika mapigano ya siku kadhaa na waasi wa Tuareg wanaotaka kujitenga na wapiganaji wanaohusishwa na al-Qaeda.
Andriy Yusov, msemaji wa idara ya ujasusi ya jeshi la Ukraine, alisema wiki iliyopita kwamba waasi walipewa "taarifa muhimu" ili kutekeleza mashambulizi hayo.
Afisa wa ngazi ya juu wa Mali, Kanali Abdoulaye Maiga, amesema serikali yake ilishtushwa kusikia madai hayo na kuishutumu Ukraine kwa kukiuka mamlaka ya Mali.
Matamshi ya Yusov "yalieleza kuhusika kwa Ukraine katika shambulio la kuogofya, la kisaliti na la kinyama la makundi ya kigaidi yenye silaha" ambalo lilisababisha vifo vya wanajeshi wa Mali, ilisema taarifa ya Kanali Maiga.
Mali imeamua kuvunja uhusiano "ikiwa ni hatua ya haraka", alisema.
Wiki iliyopita, jeshi la Mali lilikiri kuwa limepata hasara "kubwa" wakati wa mapigano ya siku kadhaa ambayo yalizuka tarehe 25 Julai.
Mapigano hayo yametokea katika jangwa karibu na Tinzaouaten, mji wa kaskazini-mashariki kwenye mpaka na Algeria.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ripoti zinasema kuwa wanajeshi hao wa Mali na Urusi walishambuliwa na waasi wa Tuareg na wapiganaji wa kundi tanzu la al-Qaeda, Jamaat Nusrat al-Islam wal-Muslimin wakati wakisubiri kuongezwa nguvu, baada ya kuondoka Tinzaouaten.
Si wanajeshi wa Mali wala Wagner, ambao tangu wakati huo wamejiunga na kundi linaloitwa Africa Corps, ambao wametoa takwimu kamili, lakini makadirio ya vifo vya wapiganaji wa Wagner ni kati ya 20 hadi 80.
Hasara ya kikosi cha mamluki cha Urusi inakisiwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Mali tangu ilipoanza kuisaidia serikali ya kijeshi kupambana na waasi miaka miwili iliyopita.
Wagner imekiri kwamba mmoja wa makamanda wake aliuawa na helikopta ya Urusi iliangushwa katika "mapigano makali", akisema walikuwa wameshambuliwa na wapiganaji wapatao 1,000.
Waasi wanaotaka kujitenga wakiongozwa na Tuareg walidai siku ya Alhamisi kuwa waliwaua mamluki 84 wa Wagner na wanajeshi 47 wa Mali.
Zaidi ya muongo mmoja uliopita, serikali kuu ya Mali ilipoteza udhibiti wa sehemu kubwa ya kaskazini baada ya uasi wa Tuareg, ambao ulichochewa na mahitaji ya serikali tofauti.
Usalama wa nchi hiyo ulitatizwa zaidi na kuhusika kwa wanamgambo wa Kiislamu katika mzozo huo.
Wakati wa kunyakua mamlaka katika mapinduzi ya 2020 na 2021, jeshi lilieleza kutokuwa na uwezo wa serikali kukabiliana na machafuko haya.
Wanajeshi hao wapya walisitisha muungano wa muda mrefu wa Mali na mkoloni wa zamani Ufaransa na kuipendelea Urusi, kwa nia ya kuzima machafuko hayo.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












