Yevgeny Prigozhin: Je, mkuu wa Wagner alikuwa ni 'maiti inayotembea?'

Chanzo cha picha, Reuters
Tangu alipoongoza uasi dhidi ya Moscow mwishoni mwa Juni Yevgeny Prigozhin alielezewa na walinzi wa Urusi kama ''maiti inayotembea''.
Akizungumzia muda wa kuishi wa kiongozi huyo wa mamluki, Mkurugenzi wa CIA William Burns hata alisema: "Kama ningekuwa Prigozhin nisingemfuta mwonjaji wangu wa chakula"
Iwapo itathibitishwa kuwa ndege iliyokuwa imembeba Yevgeny Prigozhin ilishambuliwa kimakusudi kama hatua yaKremlin kulipiza kisasi, basi kitendo hiki kitaingia katika historia ya Urusi kama "operesheni maalum ya kijeshi".
Prigozhin, mfungwa wa zamani, mpishi na mfanyabiashara aliyegeuka kuwa mamluki, alikuwa na watu wengi wanaomsifu miongoni mwa safu za jeshi lake la mamluki la Wagner na zaidi. Wengi watakuwa wameshuhudia mapokezi yake mazuri kutoka kwa umma huko Rostov-on-Don wakati alifika huko miezi miwili iliyopita katika hatua ya uasi wake wa siku moja.
Lakini pia alikuwa na maadui wengi huko Moscow, haswa katika ngazi ya juu ya jeshi la Urusi ambalo mara kwa mara aliwakosoa viongozi wake hadharani.
Jambo ambalo pengine limegeuka kuwa kosa lake kuu ni kuvuka mpaka wa Rais Putin wakati alipoongoza maasi hayo huko Moscow mnamo 23 Juni.
Ingawa hakumtaja Putin moja kwa moja wakati huo, Prigozhin aliikasirisha Kremlin kwa kukosoa hadharani sababu rasmi zilizotolewa na Urusi kuvamia Ukraine mnamo Februari 2022.
Aliwaambia Warusi walikuwa wamedanganywa na kwamba wana wao wanakufa katika vita vya Ukraine kutokana na uongozi mbovu.
Huu ulikuwa uzushi na ujumbe wa video wa Putin siku hiyo ulikuwa mkali sana. Alitaja hatua ya Prigozhin huko Moscow kuwa usaliti na kuchomwa kisu mgongoni

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Vladimir Putin hawasamehe wasaliti wala wale wanaompa changamoto.
Afisa wa zamani wa ujasusi wa Urusi aliyegeuka kuwa mwasi, Alexander Litvinenko, alikufa kifo cha polepole na cha uchungu katika hospitali ya London mnamo 2006 baada ya kuwekewa sumu ya mionzi ya Polonium-210.
Uchunguzi uliofuata ulihitimisha kwamba wauaji wake walitumia dutu hatari kutoka Urusi na kwamba inaweza tu kuwa imetolewa kutoka kwa maabara ya serikali ya Urusi. Moscow ilikanusha kuhusika lakini ilikataa kuwasalimisha washukiwa wawili kwa ajili ya kesi.
Mrusi mwingine ni Sergei Skripal, afisa wa zamani wa KGB ambaye pia aliasi tena nchini Uingereza. Mnamo mwaka wa 2018 yeye na binti yake Yulia waliponea kifo chupuchupu wakati maafisa wa ujasusi wa kijeshi wa GRU wa Urusi walidaiwa kumwekea sumu neva ya Novichok kwenye mpini wa mlango wa nyumba yake huko Salisbury.
Chupa ya manukato iliyotupwa iliyokuwa na dawa ya kuua ilipatikana baadaye na mkazi wa eneo la Wiltshire, Dawn Sturgess, ambaye alikufa baada ya kupaka kwenye mikono yake.

Chanzo cha picha, EPA
Ndani ya Urusi kuna orodha ndefu ya watu, ikiwa ni pamoja na wakosoaji na wafanyabiashara, ambao wamekutana na kifo cha ghafla, katika baadhi ya matukio "kuanguka nje ya madirisha kutoka ghorofa ya juu".
Mpinzani mkubwa wa Rais Putin, Alexei Navalny, sasa anateseka katika gerezani kwa kile kinachosemekana kuwa tuhuma za ulaghai zilizochochewa kisiasa.
Yeye pia alinusurika kuuawa kwa sumu ya Novichok baada ya kukaribia kufa ndani ya ndege akiwa safarini kutoka Siberia mnamo 2020.
Lakini kisa cha Prigozhin kilikuwa tofauti sana, ambayo inafanya kifo chake kuwa na utata zaidi kwa Warusi. Mhusika huyu alikuwa na ni mtu ambaye alikuwa muhimu sana kwa Kremlin na kuchukuliwa na baadhi ya Warusi kama shujaa wa kitaifa.
Kundi lake la mamluki -Wagner, kilichoanzishwa mnamo 2014, kiliundwa kutoka kwa msingi mgumu wa watendaji wa zamani wa Speznaz (Vikosi Maalum) vya Urusi na askari wengine.
Limekuwa likiendesha shughuli zake mashariki mwa Ukraine ambapo lilifanikiwa kutimua jeshi la Ukraine kutoka mjini Bakhmut, na kupata sifa ya kushangaza ambayo haipewi jeshi la kawaida la Urusi linalodaiwa kuongozwa vibaya.
Wagner iliimarisha safu yake wakati Prigozhin alipotembelea jela za Urusi ili kuajiri maelfu ya wafungwa wakiwemo wabakaji na wauaji. Hatua hii ilitumiwa kwa ufanisi kama lishe ya mizinga mashariki mwa Ukraine ambapo makamanda waliwaamuru wasonge mbele katika majaribio ya mara kwa mara ya kukabili ngome ya adui.

Chanzo cha picha, Reuters
Wagner pia wamekuwa wakifanya kazi nchini Syria kwa miaka mingi lakini ni barani Afrika ambapo wamepata mafanikio ya kimkakati kwa Kremlin. Huko wameunda mtindo wa biashara wenye ufanisi wa kikatili ambao unaonekana kupendwa na tawala zisizo za kidemokrasia.
Kwa kutoa aina mbalimbali za "huduma za usalama", kutoka ulinzi wa watu mashuhuri hadi kushawishi uchaguzi, kuwanyamazisha wakosoaji, wamepokea haki za madini na upatikanaji wa dhahabu na madini mengine ya thamani katika mataifa kadhaa ya Afrika. Pesa zinarudi Moscow na kila mtu anatajirika - isipokuwa watu wa nchi hizo.
Wapiganaji wa Wagner wameshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia nchini Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Hata hivyo wamefanikiwa kupindua majeshi ya Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi katika eneo kubwa la bara la Afrika. Ni wiki hii tu Prigozhin ilijitokeza kwenye chaneli ya Telegram katika video inayodhaniwa kuwa ilirekodiwa katika kituo kimoja nchini Mali, ikiahidi kupanua shughuli za Wagner barani Afrika na "uhuru" kwa watu wake.
Licha ya hayo yote, kuna baadhi ya watu waliorudi Moscow, haswa katika ujasusi wa kijeshi, ambao walimwona kama dhima, kanuni huru na tishio dhidi utawala wa Putin na mfumo unaomzunguka.















