Uchaguzi Kenya 2022: Changamoto zinazokabili Miungano ya kisiasa

Rais Uhuru kenyatta akihutubia mkutano wa kisiasa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Uhuru kenyatta akihutubia mkutano wa kisiasa
    • Author, Maimuna Mwidau
    • Nafasi, Mchambuzi

Miungano ya kisiasa ni baina ya vyama vya kisiasa vyenye itikadi ama sera pamoja na nia ya kufikia lengo fulani. Miungano hii inaundwa kabla ama baada ya uchaguzi kwa madhumuni ya kuleta ushindi na kuunda serikali nchini.

Miungano ya aina hii kabla ama baada ya uchaguzi inatokana na chama kimoja pekee kutoweza kupata ushindi wa moja kwa moja kulingana na matakwa ya katiba ya 2010 na sheria za uchaguzi nchini Kenya. Hivi karibuni nchini Kenya kumekuwa na harakati za vyama kuunda miungano kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe 9 Agosti 2022.

Utaratibu wa kuunda miuungano nchini Kenya unafuata sheria za vyama vya kisiasa ambazo zilibuniwa na kuweka taratibu za kusajili vyama vya kisiasa, pamoja na taratibu za kuunda miungano. Halikadhalika, mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa uraisi unaendelezwa kulingana na taratibu zilizowekwa na katiba ya Kenya 2010.

Licha ya kuwepo kwa mpangilio wa sheria wa kuongoza mchakato wa uchaguzi kwa misingi ya kidemokrasia, Kenya bado inakumbwa na changamoto za siasa za miungano. Changamoto hizi zimetokana kwanza na mikataba baina ya vyama ambavyo vimeamua kuunda muungano. Pili ni hesabu na ushawishi wa kikabila. Tatu ni udhaifu wa vyama na kukosekana kwa misingi bora ya sera. Nne na mwisho, ni mgawanyiko ndani ya serikali inayotawala.

Sheria

Kulingana na matakwa ya katiba ya Kenya 2010, kupata ushindi wa moja kwa moja wa Uraisi, inamlazimu mshindi aweze kupata asilimia 25% ya kura katika nusu ya kaunti 47, pamoja na asilimia 50 + 1 ya kura zote zitakazopigwa nchini. Sheria hii imeleta changamoto kubwa kwa vyama vya kisiasa na viongozi wao.

Changamoto hizi zinatokana na desturi ya vyama vya kisiasa kuwa na ufuasi wa kikabila na sio wa sera wala itikadi. Kwa hiyo, inalazimu kila chama kuhusisha viongozi wa kaunti hizo ambao wana ufuasi mkubwa wa maeneo yao ama ni viongozi wa chama cha kisiasa chenye ushawishi mkubwa katika hilo eneo ili kuafikia matakwa ya kikatiba.

Changamoto ya ziada ni kwamba, viongozi wanapokuwa katika mchakato wa kuafikia matakwa ya kisheria, wao pia huwa wanajadiliana kuhusu muungano wao, na matarajio yao endapo huo muungano utaunda serikali.

Raila Odinga

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Raila Odinga

Mfano bora ni yale maeneo yenye kura nyingi zaidi. Wao huwa wanafanya majadiliano vipi wataunga mkono muungano na matarajio yao. Matarajio huwa ni namna watakavyo weza kuchaguliwa katika baraza la mawaziri, nafasi za mabalozi na mashirika mbali mbali serikalini.

Majadiliano hayo yanafika kilele pale mikataba baina ya vyama inapotiwa saini ili kuhakikisha kwamba yale makubaliano yatatekelezwa endapo muungano utaunda serikali.

Hesabu ya kikabila

Ijapokuwa vyama vimesajiliwa kisheria kama vyama vya kitaifa, vyama vingi vina ufuasi mkubwa kwa misingi ya kikabila. Hii inachangiwa zaidi na sehemu anayotoka kiongozi wa chama hicho. Kwa hivyo imedhihirika wakati wa uchaguzi kwamba baadhi ya maeneo yanachagua chama ambacho kiongozi ametoka kwao nyumbani.

Hesabu za kikabila pia imewalazimu wanasiasa katika miungano kutafuta ufuasi kutoka maeneo yao kwa njia ya kikabila bila kuzingatia sera . Mfano mzuri ni ule wa miungano mikubwa miwili ilioweza kupata naibu wa mgombea uraisi kutoka sehemu moja tu ya Kenya ambako kunajulikana kuna idadi kubwa ya kura kuliko sehemu yoyote nchini. Ni kwasababu kama hizi, ambapo vyama vimelazimishwa kuunda miuungano ili kuweza kufikia yale matakwa ya katiba, sheria za uchaguzi na mwishowe ushindi mkubwa.

William Ruto

Chanzo cha picha, Getty Images

Mfumo dhaifu wa vyama

Mifumo dhaifu ya vyama imechangia pakubwa katika hizi changamoto za siasa za miungano. Kama ilivyoelezwa awali, vyama vingi vimebuniwa sio kwa itikadi maalumu ila kwa ushawishi wa maeneo ya anayotoka kiongozi. La ziada ni kwamba vyama vingi vimekosa msingi bora wa sera ambazo zingevutia ufuasi mkubwa wa muungano wenye mwelekeo wa sera za jamii. Kwasababu hizo za ushawishi wa maeneo na kukosa kuwa na sera maalumu, vyama vingi vidogo vimekosa ufuasi na uwezo wa kuendeleza sera zao nchi nzima.

Pamoja na hayo, imechangia pakubwa upungufu wa uongozi wa kisiasa na demokrasia katika vyama vya kisiasa. Pia, kukosa ufuasi mkubwa na kusajili idadi kubwa ya wanachama nchi nzima, vyama vimekuwa vinategemea kupewa usaidizi na vyama vikubwa ndani ya miungano ili kuendeleza mipango yao midogo. Hili limekuwa mzigo mzito na tatizo kubwa la kudumisha umoja wa muungano.

Mikataba

Kulingana na sheria za vyama vya kisiasa, kila chama ambacho kimeamua kujiunga na muungano, kinapaswa kufuata taratibu za kujiunga na muungano kwa kuandikiana mikataba ya makubaliano. Baada ya kuweka sahihi, mikataba inapelekwa kwa msajili wa vyama vya kisiasa.

Hii mikataba baina ya vyama vya muungano inaeleza yale makubaliano yatakayotekelezwa endapo muungano utashinda uchaguzi na kuunda serikali. Makubaliano hayo ni kama ugawaji wa fedha za vyama, nafasi za vyeo serikalini na mengineo mengi.

Changamoto kubwa imekuwa katika uwazi wa makubaliano ya hii mikataba kwa vyama vidogo kulemewa na vyama vyenye ufuasi mkubwa nchini. Hili pia limeleta changamoto ambayo imeonekana kuhama kwa vyama kadhaa kutoka muungano mmoja na kujiunga na muungano mwengine ulio na uwazi zaidi.

Pamoja na hayo, kutokuaminiana baina ya viongozi wa vyama kumechipuka. Tetesi zimejitokeza kuhusu taratibu za mchakato wa mchujo wa vyama ili apatikane mgombea mmoja kutoka kwenye muungano. Swali kubwa lilikuwa ni je muungano utawasilisha kwa tume ya uchaguzi wagombea kadhaa kutoka kila chama ama mgombea mmoja wa muungano kwa kila nafasi zote za uchaguzi?.

Swali hili limeweza kutatuliwa na muungano mwingine kwa mfumo wa kugawa sehemu za nchi kwa vyama kulingana na maeneo yao ya kikabila na kutoa masharti ya idadi ya kura kila chama kinatakiwa kuleta kwa muungano ili chama kipate fursa ya kuwepo kwenye kuunda serikali endapo ushindi utapatikana.

Wafuasi wa mgombea wa urais nchini Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wafuasi wa mgombea wa urais nchini Kenya

Miungano ya vyama vya kisiasa imejitokeza kwa nguvu wakati huu nchi ya Kenya inapojiandaa kufanya uchaguzi mwezi Agosti 9, 2022. Vyama vya kisiasa vimekuwa katika harakati za kuweka mikataba ya muungano huku wengine wakiamua kuhama muungano na kujiunga na mwengine.

Kumekuwa na ushawishi mkubwa wa kikabila ili vyama kupata idadi kubwa ya ufuasi kutoka maeneo yenye idadi kubwa ya kura na sio itikadi au sera za maendeleo. Hizi ndio baadhi ya changamoto za kuchagua uongozi nchini Kenya.

Waathiriwa wa baadaye ni Wakenya ambao wataishia na wafalme wa kisiasa na waakilishi wao waliochaguliwa afisini kwa nguvu na ushawishi wao wa kikabila na sio kwa sababu ya sera zitakazo Jenga Taifa la Kenya.