Muda bora wa mazoezi hutofautiana kwa wanaume na wanawake, unasema utafiti wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Mazoezi ni mazuri kwako wakati wowote unapoyafanya, lakini muda wa siku ili kufikia matokeo bora unaweza kuwa tofauti kwa wanawake na wanaume, kulingana na utafiti wa Marekani.
Uligundua kuwa wanawake walichoma mafuta mengi mwilini wakati wa mazoezi ya asubuhi, wakati jioni ilihesabiwa zaidi kwa wanaume.
Mengi ya kile kinachojulikana juu ya mada hii ni msingi wa tafiti juu ya wanaume, watafiti wanasema.
Tofauti za homoni, katika saa za kibaiolojia na mizunguko ya kuamka kati ya jinsia zote, zinaweza kuwa na jukumu.
Utafiti huo wa wanaume 30 na wanawake 26 - wote wakiwa hai na wenye afya nzuri, na kati ya umri wa miaka 25 na 55 - ulidumu kwa wiki 12 na kufuatilia athari za programu ya usawa wa mwili, ambayo ilijumuisha kujinyoosha, kukimbia mbio, upinzani na mafunzo ya uvumilivu.
Kundi moja lilifanya mazoezi kwa saa moja kabla ya saa mbili na nusu asubuhi huku kundi lingine likifuata shughuli zile zile jioni, kati ya 18:00 na 20:00 usiku.
Washiriki wote walifuata mpango maalum wa chakula.
Watafiti walijaribu shinikizo la damu na mafuta ya mwili ya kila mtu katika kipindi cha utafiti, pamoja na kubadilika kwao, nguvu na mazoezi makali ya viungo mwanzoni na mwisho.
Wale wote walioshiriki katika utafiti waliboresha afya na utendakazi wao kwa ujumla katika jaribio la wiki 12, bila kujali walifanya mazoezi lini.
''Wakati mzuri zaidi wa kufanya mazoezi ni wakati mzuri zaidi unaoweza kufanya hivyo na kufaa katika ratiba yako,'' anasema Dk Paul Arcerio, mwandishi mkuu wa utafiti na profesa wa sayansi ya afya na fiziolojia ya binadamu katika Chuo cha Skidmore, jimbo la New York.
Lakini anapendekeza kuna ''kitu kingine kinachoendelea'' ambacho kinaweza kumaanisha wakati mzuri wa siku wa kufanya mazoezi ni tofauti kwa wanawake na wanaume.
Mazoezi ya mapema au jua likishaanza kutua?
Kulingana na matokeo, wanawake wanaopenda kupunguza mafuta karibu na katikati yao na kupunguza shinikizo la damu wanapaswa kulenga kufanya mazoezi asubuhi, Dk Arcerio anasema.
Hii ni muhimu kwa sababu mafuta ya tumbo - au tumbo - huzunguka viungo vya ndani vya mwili, ikiwa ni pamoja na ini, na inaweza kuwa hatari.
Hata hivyo, anasema wanawake wanaojaribu kuboresha uimara wa misuli katika sehemu zao za juu za mwili pamoja na hisia zao kwa ujumla na ulaji wa chakula, wanapaswa kufanya mazoezi ya jioni.
Wanaume katika jaribio hilo hawakuwa makini sana na muda wa siku wa kufanya mazoezi, hivyo kuboresha nguvu zao katika mazoezi asubuhi na jioni.
Lakini mazoezi ya jioni yalionekana kuwa ''ni bora kwa wanaume wanaopenda kuboresha afya ya moyo na kimetaboliki, pamoja na ustawi wa kihisia,'' anasema Dk Arcerio.
Kuboresha afya ya kimetaboliki kunamaanisha kupunguza hatari ya hali kama vile unene wa kupitiliza, kisukari cha aina ya 2, ugonjwa wa moyo na kiharusi.
Haijulikani kwa nini hasa majibu ya wanaume na wanawake kwa muda wa mazoezi yalikuwa tofauti sana, na watafiti wanasema utafiti zaidi unahitajika ili kujua zaidi.
Wanasema wanawake wanaweza kuchoma mafuta mengi zaidi asubuhi kwa sababu wana uwezekano mkubwa wa kuwa na mafuta mengi ya tumbo.
Midundo ya ndani ya mwili inaweza pia kuwa sababu.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Frontiers in Physiology, ulifuatilia watu walio na uzani mzuri kiafya, lakini watafiti wanasema mpango huo unaweza pia kuwafanyia kazi watu walio na uzito mkubwa au wanene kupita kiasi.
''Wana fursa zaidi ya kufaidika,'' anasema Dk Arcerio.












