Miili ya wanajeshi wa Urusi yatelekezwa na kuzagaa karibu na mji wa Kyiv

Mbwa wao walipoanza kuchimba kwa bidii mahali fulani msituni, wanakijiji wa Zavalivka waliwaita wenye mamlaka.

Kikosi cha wanajeshi wa Ukraine hivi karibuni walikuwa kwenye eneo la tukio wakiwa wamevalia suti nyeupe za kujikinga, wakifukua udongo wa juu kwa uangalifu.

Waliutoa mwili wa mtu (maiti). Kwa sare yake ilikuwa wazi kwamba alikuwa askari wa Urusi.

Wiki kadhaa baada ya kushindwa kuuteka mji mkuu wa Ukraine, Kyiv mabaki ya miili ya wanajeshi wa Urusi imeendela kugundulika katika mji huo na vijiji walivyopitia au kuvikalia karibu na mji mkuu, Kyiv. Lakini Ukraine inasema Urusi haionyeshi nia yake ya kuichukua miili hiyo.

Kutoka msituni, mwili huo ulitolewa na kuhifadhiwa kwenye jokofu la treni ndogo nje kidogo ya mji wa Kyiv ambayo sasa inafanya kazi kama chumba cha kuhifadhia maiti za wanajeshi wa Urusi.

Mifuko 137 mikubwa meupe ya plastiki ikiashiria kuwa na miili ya watu iliyowekwa namba badala ya majina ilionekana ndani ya mabehewa mawili siku tulipotembelea.

Wanajeshi wa Ukraine wanajaribu kuitambua miili hiyo:

"Angalau huyu ana nafasi ya kurejea nyumbani," msimamizi alitangaza, akionyesha matokeo, ikiwa ni pamoja na kipande cha fulana kilichochafuliwa kilichochapishwa na nembo ya Jeshi la Urusi.

Urusi ina kauli mbiu inayosema: "Hatutekelezi vyetu." Ni sehemu kubwa ya uhalali wa Rais Vladimir Putin wa kuivamia Ukraine, ambapo alidai kwamba wazungumzaji wa Kirusi walihitaji ulinzi.

Ahadi hiyo inaonekana haibebwi sana kwa wanajeshi wa Urusi wenyewe.

"Miili tuliyoipata inaonyesha kuwa inawachukulia watu kama takataka, kama chakula cha mizinga," Kanali Volodymyr Liamzin aliambia BBC.

"Hawahitaji askari wao. Wanawatupa hapa, wanaondoka - na kuacha miili."

Hakuna upande wowote kati ya Ukraine na Urusi ulio wazi kuhusu maiti zinazozagaa.

Tumezungumza na familia kadhaa za Kiukreni ambazo zinasema serikali yao imekuwa na msaada mdogo katika kurejesha mabaki ya miili ya wanajeshi wa Ukraine waliouawa kutoka kwenye uwanja wa vita.

Mwanamke mmoja, ambaye aliambiwa kuhusu kifo cha mumewe na wenzake, alisema alikuwa akijaribu kurejesha mwili wake kwa karibu miezi mitatu.

Lakini miili ya wanajeshi wa Urusi waliokufa inagunduliwa na kuokotwa hapa kila wakati.

Katika barabara ya kutoka Zavalivka huko Sytnyaky, mzee mmoja wa kijiji alituambia mwezi Machi angalau wanajeshi 10 wa Urusi waliuawa na miili yao kutekelezwa mwezi, pengine zaidi.

Safu yao ilivamiwa baada ya kupotea njia: wenyeji walikuwa wameondoa na kubadili alama za trafiki.

Vita vilikuwa vikali. Kile ambacho zamani kilikuwa mgahawa kando ya barabara mahali hapo sasa ni rundo la vifusi, ukuta kidogo na hifadhi kubwa ya maji.

Vipeperushi kwenye magofu vinatoa wito kwa askari wa Urusi kujisalimisha na kuokoa maisha yao, na kuokoa damu ya watoto wa Kiukreni.

Mzee wa kijiji anasema yeye na wengine walizika Warusi baada ya vita "kwa sababu za usafi". Anasema wengi walilipuliwa vipande vipande.

Hakuruhusiwa kutuonyesha makaburi: Lakini kwa hali ilnavyoonekana orodha yake ni ndefu.