Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Urusi imetekeleza uvamizi mkubwa dhidi ya Ukraine kutoka pande tatu kuu.
Ripoti zinasema wanajeshi wanasonga mbele kutoka kaskazini kuelekea Kyiv; kutoka mashariki kupitia Donetsk, Luhansk na Kharkiv; na kutoka Crimea kusini.
Katika chini ya saa 24, maeneo kadhaa yamepigwa, huku wanajeshi wa Urusi wakimiminika Ukraine.
Shambulio kutoka angani
Kuanzia takriban saa 03:00GMT, milipuko ilisikika katika miji mingi nchini kote, huku ulinzi wa anga wa Ukraine na miundombinu mingine ya kijeshi ikishambuliwa.
Wachambuzi wanasema kuwa mashambulizi kutoka angani yanalenga kusafisha njia kwa wanajeshi wa ardhini kuingia.
Miongoni mwa malengo yalikuwa maeneo ya Kyiv, Karkhiv, Odesa na Ivano-Frankivsk.
Shambulizi kutoka kaskazini
Kutoka kaskazini, wanajeshi wa Urusi wanaaminika kuvuka mpaka na kuingia Ukraine kwenye makutano ya njia tatu kati ya Ukraine, Urusi na Belarus, huko Senkivka.
Katika wiki za hivi karibuni, idadi kubwa ya wanajeshi wa Urusi wamekusanyika karibu na Novye Yurkovichi na Troebortno, likiwemo "jeshi zima la 41", kulingana na Michael Kofman wa Kituo cha Uchambuzi wa Majini chenye makao yake makuu nchini Marekani.
Nguzo za kivita, ikiwa ni pamoja na mizinga na mifumo mingi ya roketi za kurusha, zimehamia Chernihiv, kwenye njia ya moja kwa moja kuelekea Kyiv.
Pia kumekuwa na mapigano kwenye viunga vya mji mkuu, huku vikosi vya Ukraine vikijaribu kuteka tena kambi ya kikosi cha anga ya Antonov magharibi mwa mji huo.
Wanajeshi wa anga wa Urusi walichukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Gostomel, lakini rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliapa kwamba watazingirwa na kupigwa.
Shambulio la kombora pia lilipiga mji wa Brovary, mashariki mwa Kyiv.
Vikosi vya Urusi vimeripotiwa kukamata kinu cha zamani cha nyuklia huko Chernobyl.
Shambulio kutoka mashariki
Kutoka mashariki, kuna ripoti kwamba vifaru vya Kirusi vimewasili Kharkhiv, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ukraine. Sehemu za jiji zimepigwa makombora.
Usiku kucha, kulikuwa na milipuko mikubwa huko Donetsk, na milipuko kama hiyo ikitoka upande wa Belgorod kuvuka mpaka, ambapo harakati kubwa za askari ziliripotiwa Jumatano.
Kando, shirika la habari la Interfax la Urusi liliripoti madai kutoka kwa watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi kwamba walikuwa wameanzisha mashambulizi dhidi ya mji unaodhibitiwa na Ukraine wa Shchastia huko Luhansk.
Pia kulikuwa na mapigano makali karibu na Sumy, karibu na Kharkiv.
Inafikiriwa kuwa kuna watu 15,000 wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi huko Donetsk na Luhansk, ambao wanaweza kusaidia Urusi kusonga mbele. Ukraine inaamini takwimu ni kubwa zaidi.
Shambulio kutokea kusini
Kwa upande wa kusini, askari wamevuka kutoka Crimea hadi bara, kuelekea Kherson, wakichukua Chongar na Novo Alekseyevka.
Usiku kucha, milipuko ilisikika katika miji kote mkoa, ikiwa ni pamoja na Odesa, Mariupol, Melitpol na Kherson.
Maafisa wa Ukraine - walionukuliwa na shirika la habari la Reuters - walisema wanajeshi wa Urusi walikuwa wamefika katika bandari za Odesa na Mariupol.
Katika siku za hivi karibuni, Urusi ilikuwa imeweka meli za kutua zenye uwezo wa kupeleka vifaru vikuu vya vita, magari ya kivita na wafanyakazi, nje ya pwani ya Ukraine katika eneo kubwa la bahari Nyeusi na Bahari ya Azov.
Vikosi vya Ukraine vimejilimbikiza mashariki mwa Ukraine, kuelekea Donetsk na Luhansk.
Ben Barry, wa Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, asema kwamba Warusi wakisonga mbele kaskazini kutoka Crimea wanaweza kufaulu kuwakatilia mbali kutoka Kyiv, na kuwaweka kwenye upande wa mashariki wa Mto Dnieper.
Wanajeshi wa Urusi wakiwa mashariki mwao, huko Donetsk na Luhansk, kaskazini mwa Urusi, na kwenye ukingo wa magharibi wa Dnieper, wangezingirwa.