Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Urusi imeshutumiwa kwa kutumia silaha haramu na hatari hatua inayochukuliwa kama ukatili na unyama dhidi ya raia nchini Ukraine tangu ilipoivamia nchi hiyo jirani.
Matumizi ya silaha za thermobaric na mabomu ya 'cluster' yamelaaniwa sana na yatakuwa sehemu ya uchunguzi wa uhalifu wa kivita dhidi ya Urusi.
Kwa upande mwingine wa vita, Ukraine imetegemea washirika wake kuipatia makombora hatari ya Stinger na Javelin ili kupunguza mwendo wa vikosi vya Urusi.
Fahamu silaha zinazotumiwa na pande zote mbili katika vita hivyo na hatari ya silaha hizo huku mapigano yakichacha baada ya Urusi kuanza kulenga miji ya magharibi mwa Ukraine inayopakana na nchi jirani kama Poland ambazo zinategema ulinzi wa muungano wa kujihami wa NATO iwapo zitaonekana kutishiwa na mashambulizi ua Urusi.
Unaweza kusoma pia:
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Makombora ya Stinger ni nini?
Makombora ya Stinger, pia yanajulikana kama FIM-92, huruhusu watu walio ardhini kuangusha ndege zinazoruka chini kama vile helikopta au ndege za kawaida
Silaha hizi za ardhini hadi angani ni nyepesi, ni rahisi kusafirisha na zinaweza kurushwa na mtu mmoja tu.
Makombora ya stinger hufuata joto ambalo ndege hutoa na haihitaji kurekebishwa mara baada ya kurushwa, na kuwapa watu walio chini wakati wa kuondoka.
Nani anayo?
Nchi ambazo zimeipatia Ukraine makombora ya Stinger ni pamoja na Ujerumani, Marekani, Uholanzi, Lithuania na Latvia.
Wapi yamekuwa yakitumika Ukraine?
Makombora ya Stinger yametajwa kuwa silaha muhimu katika kusaidia Ukraine kukabiliana na uvamizi wa majeshi ya Urusi.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya na nchi za NATO "kuacha kusukuma silaha" kwenda Ukraine, ikitaja wasiwasi kwamba makombora ya Stinger yanaweza kuishia mikononi mwa "magaidi" na kuwa tishio kwa mashirika ya ndege.
Makombora ya Javelin ni nini?
Makombora Javelin pia yanajulikana kama FGM-148, yameundwa kuharibu mizinga.
Yanaweza kubebeka kwa urahisi , ni mepesi na yanaweza kuzinduliwa na mtu mmoja kutoka kwa bega.
Makombora ya Javelin yameundwa kugonga tanki kutoka juu ambapo silaha zake ni nyembamba zaidi.
Yana umbali wa hadi kilomita 4.5 na pia yanaweza kutumika katika mashambulizi ya magari mengine, majengo au ndege za chini zinazoruka.
Nani anayo?
Marekani na Estonia zimeipatia Ukraine makombora ya Javelin
Uingereza na Luxemburg pia zimeipatia Ukraine aina nyingine ya kombora la kukinga mizinga, NLAW ((Next Generation Light Antitank Weapon).).
Wapi yamekuwa yakitumika Ukraine?
Kama makombora ya Stinger, makombora ya Javelin yamekuwa sehemu muhimu ya safu ya ushambuliaji ya Ukraine dhidi ya vikosi vya Urusi.
Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwa na magari 280 ya kivita yaliyoharibiwa na Javelin nchini Ukraine, kati ya 300 yaliyopigwa risasi.
Tayari picha za mizinga na malori ya Urusi yamekwama kwenye matope, na kuwafanya kuwa katika hatari ya kushambuliwa na kuwalazimisha wanajeshi kuviacha vifaa hivyo.
Hali ya matope inatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika wiki zijazo.
Silaha za thermobaric ni nini?
Silaha za thermobaric pia hujulikana kama mabomu ya utupu kwa sababu hunyonya hewa kutoka kwa mapafu ya wahasiriwa wao.
Silaha ya thermobaric hulipuka katika hatua mbili.
Katika hatua ya kwanza, bomu hulipuka, na kuharibu mazingira yake kwa nguvu zinazoweza kusababisha kifo.
Kisha huachilia wingu la kemikali zenye sumu angani ambazo zinaweza kuenea kwenye majengo au makazi ya karibu.
Sekunde chache baadaye, bomu hilo hulipuka kwa mara ya pili ambapo huwasha kemikali, na kusababisha wimbi kubwa la mshtuko.
Wimbi hili la mshtuko lina uwezo wa kuvuta miili ya binadamu.
Pia huchoma oksijeni hewani, na kutengeneza 'utupu' unaoweza kupasua mapafu ya watu walio karibu.
Sheria ya kimataifa inakataza matumizi ya silaha za thermobaric dhidi ya raia, lakini sio kinyume cha sheria kutumia dhidi ya malengo ya kijeshi.
Silaha za thermobaric huja kwa ukubwa tofauti, kutoka kwa mabomu ya roketi yaliyoundwa kwa mapigano ya karibu hadi matoleo makubwa ambayo yanaweza kutumwa kutoka kwa ndege.
Nani anayo?
Marekani, Urusi, China na India ni miongoni mwa nchi zenye silaha thermobaric.
Silaha za thermobaric zilitengenezwa wakati wa Vita vya pili vya dunia na kutumika kwanza na vikosi vya Amerika katika Vita vya Vietnam.
Vikosi vya Urusi vilipeleka silaha za thermobaric katika mzozo wa Chechnya mnamo 1999.
Marekani ilizitumia mara mbili nchini Afghanistan: kwanza mwaka 2001 dhidi ya wapiganaji wa al Qaeda na Taliban waliokuwa wamejificha kwenye mapango, na tena mwaka wa 2017 dhidi ya wapiganaji wa Islamic State.
Serikali za Urusi na Syria zilishutumiwa kwa kutumia silaha za thermobaric dhidi ya waasi huko Aleppo mnamo 2016.
Wapi zimekuwa zikitumiwa Ukraine?
Maafisa wa Uingereza wanasema Wizara ya Ulinzi ya Urusi imethibitisha matumizi ya silaha za thermobaric nchini Ukraine.
Ujumbe mmoja wa Twitter mnamo Machi 10, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema Urusi imethibitisha matumizi ya mfumo wa silaha wa TOS-1A nchini Ukraine.
"TOS-1A hutumia roketi za thermobaric, kuunda athari za moto na mlipuko."
Haijulikani hadharani ni wapi au lini Urusi ilitumia mfumo wa silaha wa TOS-1A nchini Ukraine.
Mabomu ya cluster nini?
Mabomu ya cluster ni makombora ambayo hulipuka angani ili kutoa mabomu madogo kwenye eneo kubwa.
Makombora yanaweza kurushwa kutoka ardhini na mifumo mikubwa ya lori au kudondoshwa kutoka kwa ndege.
Kombora hilo linapokaribia shabaha yake, sehemu ya mbele hulipuka, na kuachia mabomu madogo kiholela kwenye eneo linalofikia ukubwa wa uwanja wa mpira.
Mabomu hayo ambayo yana ukubwa sawa na kopo la kinywaji baridi yameundwa ili kulipuka.
Hata hivyo, mara nyingi mabomu hayo hayategemeki na mengi yanashindwa kulipuka, jambo linaloweza kuwa hatari kwa watu wazima na watoto ambao watayapata baadaye.
Sehemu ya mkia ya kombora hailipuki lakini uchafu unaweza kusababisha uharibifu unapoanguka chini.
Nani anayo?
Mabomu ya makundi ama Cluster yamepigwa marufuku na zaidi ya nchi 100, ikiwa ni pamoja na Australia, chini ya Mkataba wa Mabomu ya makundi.
Urusi, Ukraine, Marekani na China hazijajiunga na mkataba huo.
Mabomu ya makundi yametumika katika migogoro mingi ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na Syria, Lebanon, Yemen, Iraq, Afghanistan, na wakati wa vita vya Balkan.
Wapi wamekuwa kutumika katika Ukraine?
Washirika wa NATO na Ukraine wameishutumu Urusi kwa kutumia mabomu hayo katika mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo.
Matukio hayo ni pamoja na shambulio karibu na hospitali katika mji wa Vuhledar siku ya kwanza ya uvamizi huo, Februari 24. Raia kadhaa waliuawa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mabomu ya makundi yaliwaua watu watatu, akiwemo mtoto, wakati shule ya chekechea katika mji wa Okhtyrka iliposhambuliwa Februari 25.
Mabomu hayo pia yaliripotiwa kutumika katika shambulio lililoua raia katika makazi ya watu wa Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, mnamo Februari 28.
Uchunguzi wa uhalifu wa kivita umeanzishwa kuhusu utumiaji wa mabomu hayo.