Vita vya Ukraine: Putin aapa kuendeleza uvamizi mpaka malengo yake ''makuu'' yatimie

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameapa kuendeleza mashambulizi Ukraine hadi malengo ''makuu'' ya nchi yake yatimie.

Amesema mazungumzo ya amani yamefikia kikomo na kusisitiza uvamizi huo - ambao uko katika wiki yake ya sita - unaendelea kama ilivyopangwa.

Afisa wa Ukraine, hata hivyo, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo yalikuwa magumu lakini yanaendelea.

Maoni ya Bw Putin yalikuwa ya kwanza kuhusu mzozo huo katika zaidi ya wiki moja.

Tofauti na siku za mwanzo za vita hivi karibuni ameweka hadhi ya chini.

Alikuwa akitembelea kituo cha anga za juu mashariki mwa Urusi akiwa na kiongozi wa Belarus Aleksandr Lukashenko, mmoja wa washirika wake wa karibu, kuadhimisha mwaka wa 61 wa Yuri Gagarin kuwa mtu wa kwanza angani.

Kiongozi huyo wa Urusi alidai kuwa hakuwa na la kufanya ila kuanzisha uvamizi huo kwa nia ya kuwalinda wazungumzaji wa Kirusi mashariki mwa Ukraine.

Kremlin inadai kuwa Ukraine imefanya mauaji ya halaiki dhidi ya wazungumzaji wa Kirusi mashariki mwa Ukraine, lakini hakuna ushahidi wa kuunga mkono hili,

"Kwa upande mmoja, tunasaidia na kuokoa watu, na kwa upande mwingine, tunachukua hatua za kuhakikisha usalama wa Urusi yenyewe," kiongozi huyo wa miaka 69 alisisitiza.

"Ni wazi kwamba hatukuwa na la kufanya. Ulikuwa uamuzi sahihi," alisema, akiongeza kuwa Urusi "itaendeleza uvamizi" bila "parapara".

Moscow imehamishia mwelekeo wake mashariki mwa Ukraine, na kuwahamisha wanajeshi kutoka kaskazini baada ya kukabiliwa na upinzani mkali katika wiki za mwanzo za kile ilichokiita "operesheni yake maalum".

Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 10 wamekimbia makazi yao tangu uvamizi huo uanze.

Msemaji wa rais wa Urusi Dmitry Peskov alikiri wiki iliyopita kwamba nchi hiyo imepata "hasara kubwa ya wanajeshi" tangu mzozo huo uanze.

Si Urusi wala Ukraine makadirio ya hasara ya Urusi yanaweza kuthibitishwa kwa kila upande - na wachambuzi wametahadharisha kuwa Urusi inaweza kuwa inapunguza kiwango chake cha madhara, wakati Ukraine inaweza kuongeza ili kuongeza ari. Viongozi wa nchi za Magharibi wanaamini kuwa kati ya wanajeshi 7,000 na 15,000 wa Urusi wameuawa.

Uchumi wa Urusi pia umetikiswa na vikwazo vikali vilivyowekwa na mataifa ya Magharibi.

Hata hivyo, siku ya Jumanne, Bw Putin alisema Urusi "haikudhamiria kutengwa", akisema kwamba "haiwezekani kutenga mtu yeyote katika ulimwengu wa kisasa - haswa nchi kubwa kama Urusi".

Bw Lukasjenko pia alipuuzilia mbali athari za vikwazo, na kumuuliza Bw Putin: "Kwa nini duniani tunapata wasiwasi sana kuhusu vikwazo hivi?"

Wiki iliyopita, serikali ya Uingereza ilitabiri kwamba Urusi inaelekea kwenye mdororo mkubwa zaidi wa uchumi tangu kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

Katika hatua nyingine:

• Urusi ilizidisha juhudi zake za kuchukua mji wa bandari wa kusini uliozingirwa wa Mariupol. Meya wa jiji hilo alisema takriban watu 21,000 walikufa huko, lakini maafisa wamelazimika kuacha kuhesabu miili kutokana na mapigano ya mitaani.

• Pia katika jiji hilo, serikali za Magharibi na mashirika ya kimataifa yalionesha wasiwasi wao kuhusu ripoti ambazo hazijathibitishwa za mawakala wa kemikali wanaotumiwa na Urusi huko.

• Idara ya usalama ya Ukraine ilisema imemkamata mwanasiasa anayeiunga mkono Urusi Viktor Medvedchuk. Alikuwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa tuhuma za uhaini lakini alikimbia siku chache baada ya Urusi kuanza uvamizi wake.

• Na Gavana wa Luhansk mashariki mwa Ukraine alisema takriban raia 400 wamezikwa katika mji wa Severodonetsk karibu na mstari wa mbele wa mapigano tangu kuanza kwa uvamizi huo.

Unaweza pia kusoma