Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ukraine na Urusi: Putin anapotoshwa na washauri waoga-Marekani
Rais wa Urusi Vladimir Putin anapotoshwa na washauri ambao wanaogopa sana kumwambia jinsi vita vya Ukraine vinavyoendelea vibaya, Ikulu ya Marekani inasema.
Wakati huo huo idara ya kijasusi ya Uingereza inasema kuwa wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine wamekatishwa tamaa, hawana vifaa na wanakataa kutekeleza maagizo.
Bw.Putin pia haambiwi kuhusu athari kamili ya vikwazo kwa uchumi wa Urusi, Ikulu ya Marekani ilisema.
Kremlin bado haijatoa maoni juu ya tathmini hizo.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Kate Bedingfield alisema Marekani ilikuwa na habari kwamba Bw Putin "alihisi kupotoshwa na jeshi la Urusi" na hii imesababisha "mvutano unaoendelea kati ya Putin na uongozi wake wa kijeshi".
"Vita vya Putin vimekuwa kosa la kimkakati ambalo limeiacha Urusi kuwa dhaifu kwa muda mrefu na kuzidi kutengwa katika ulimwengu," alisema.
Msemaji wa Pentagon John Kirby amesema kuwa Putin ambaye hana taarifa za kweli anaweza kusababisha juhudi" katika kumaliza mzozo kupitia mazungumzo ya amani kutozaa matunda.
"Nyingine ni kwamba, hujui kiongozi wa namna hiyo atapokeaje habari mbaya," alisema.
Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Vikosi vya Ukraine vimeanza majaribio ya kutwaa tena baadhi ya maeneo yanayoshikiliwa na Urusi, ambayo siku ya Jumanne ilisema itapunguza operesheni zake za kijeshi katika mji wa Kyiv na mji wa kaskazini wa Chernihiv.
Mkuu wa Shirika la kijasusi la GCHQ linaloshughulikia masuala ya mtandao Uingereza, Jeremy Fleming alisema hatua hiyo inaongeza dalili kuwa Urusi "imeichukulia vibaya hali hiyo" na kulazimika "kwa kiasi kikubwa kutafakari upya".
Bw. Fleming alisema wanajeshi wa Urusi waliharibu vifaa vyao na kuangusha ndege zao wenyewe kimakosa.
Alionya pia China kutojiweka karibu sana na Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, akisema kuwa ushirikiano huo hautayasaidia maslahi ya muda mrefu ya Beijing.
Kwa upande mwingine, maafisa wa Marekani na Ukraine wanasema Urusi inaendelea kuviondoa vikosi vyake karibu na Kyiv, pengine ni sehemu ya juhudi zake za kuelekeza nguvu zake katika maeneo ya mashariki.
Katika hatua nyingine:
Rais Volodymyr Zelensky alitilia shaka madai ya Urusi kuwa inapunguza kasi, akisema ilishawahi kutokea huko nyuma katika eneo la mashariki la Donbas na kuzuka "mashambulizi mapya".
"Hatuamini mtu yeyote. Hakuna hata neno moja zuri," alisema.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilipendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa siku moja huko Mariupol iliyozingirwa siku ya Alhamisi ili kuwaruhusu watu kuondoka.
Haya yalijiri baada ya Bw Putin kusema Mariupol italazimika kujisalimisha ili kukomesha mashambulizi hayo.
Afisa wa ulinzi wa Marekani alisema baadhi ya wanajeshi wa Urusi walikuwa wakiondoka eneo la Chernobyl - kilipokuwa kinu cha zamani cha nyuklia ambacho kilihusika katika ajali mbaya zaidi ya nyuklia duniani mwaka 1986 - na kuelekea katika nchi jirani ya Belarus. "
"Tunadhani kwamba wanaondoka, lakini siwezi kukwambia kuwa wameondoka wote," afisa huyo alisema.
Waukraine milioni nne wameikimbia nchi yao na robo ya watu wote nchini humo wameyakimbia makazi yao.