Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Makaburi ya pamoja Ukraine: Miji iliyoshambuliwa inachimba maeneo ya muda ya maziko
Mashambulio ya mabomu ya Urusi katika baadhi ya maeneo nchini Ukraine ni makali kiasi kwamba miji na majiji yanalazimika kuzika makumi ya wahanga ambao ni raia katika makaburi ya halaiki.
Hakuna mahali ambapo ukweli huu mbaya wa vita unaonekana zaidi kuliko huko Mariupol, jiji kuu la bandari lililoharibiwa na makombora ya mara kwa mara, ambapo maeneo kadhaa ya mazishi yamechimbwa kwa haraka katika wiki mbili zilizopita.
"Hatuwezi kuwazika [wahasiriwa] katika makaburi ya kibinafsi, kwa vile wale wako nje ya jiji na eneo hilo linadhibitiwa na wanajeshi wa Urusi," naibu meya wa Mariupol Serhiy Orlov aliambia BBC kwa njia ya simu.
Maeneo hayo yanajumuisha kaburi la jiji lililostaafu ambalo sasa limefunguliwa tena, Bw Orlov alisema.
Onyo: Makala hii ina picha ambazo wengine wanaweza kuzipata zikiwakera
Siku ya Jumapili, baraza la jiji lilisema idadi ya vifo vya raia imeongezeka zaidi ya 2,100. Mashambulizi makubwa ya makombora ya Urusi yamezuia uhamishaji wowote wa watu wengi kutoka Mariupol, licha ya juhudi za kufungua njia salama ya kutoka.
Bw Orlov hakuweza kutoa jumla ya raia waliokufa waliozikwa kwenye makaburi ya halaiki, lakini alisema miili 67 ilikuwa katika eneo moja. "Wengine hatuwezi kuwatambua lakini wengine walikuwa na nyaraka."
Unaweza kusoma pia:
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Maelfu ya wakaazi wamejificha kwenye pishi na katika visa vingine, alisema, watu wanazika wanafamilia kwa faragha kwenye ua au bustani.
Wasafishaji wa barabara za jiji hilo walioathirika na timu za kutengeneza barabara walikuwa wakikusanya miili mitaani, alisema, huku huduma za manispaa zikiporomoka. "Baadhi ya watu waliuawa wakati wa makusanyo hayo. Tumekuwa hatuna umeme, au joto, usafi wa mazingira, maji, chakula kwa siku 11," alisema.
Maili mia nne kaskazini magharibi, kwenye ukingo wa mji mkuu wa Kyiv, kaburi la halaiki lilichimbwa karibu na kanisa katika mji wa Bucha, mbunge wa eneo hilo Mykhailyna Skoryk-Shkarivska alisema. Ina miili zaidi ya 60.
Video ya mazishi hayo iliwekwa kwenye Facebook na daktari anayefanya kazi katika eneo la karibu la Irpin, Andriy Levkivsky. Madaktari walizika wahasiriwa, ambao walikuwa wameletwa katika hospitali ya Irpin.
Bi Skoryk-Shkarivska aliambia BBC kwamba "ibada ya kitamaduni" ilifanywa hospitalini kabla ya mazishi. Sio wote walikuwa wametambuliwa na "hakuna anayejua jamaa waliko," alisema.
"Sasa tunajadiliana na watu waliojitolea jinsi ya kuunda mfumo wa kidijitali kutambua watu na kufuatilia jamaa waliopotea," alisema.
Wanajeshi wa Urusi waliteka hospitali hiyo siku ya Jumamosi na kuwaambia madaktari waondoke, alisema, akizungumza kwa simu kutoka magharibi mwa Ukraine. Bucha na nusu ya Irpin sasa ziko mikononi mwa Urusi, alisema.
Kurudi kwa makaburi ya watu wengi ni mshtuko kwa Waukraine. Wengi wana kumbukumbu za uchungu wa kifamilia wakati wa Vita vya pili vya dunia wakati Wayahudi na washiriki wa Soviet waliuawa na Wanazi, na Holodomor - njaa iliyoanzishwa nchini Ukraine na ukamataji wa nafaka na mifugo wa Soviet katika miaka ya 1930.
"Mjomba wangu ana umri wa miaka 92 na hata alilinganisha na utoto wake katika vita," alisema Bi Skoryk-Shkarivska, ambaye alisisitiza "ni muhimu kwetu kuzika jamaa kwa njia ya jadi, njia ya Kikristo, kwa kusali".
"Hata sasa katika vita watu wakati mwingine huwauliza makasisi kufanya hivyo," alisema.
Kaskazini mwa Ukraine miji ya Kharkiv, Chernihiv na Sumy imezingirwa na wanajeshi wa Urusi na mashambulizi ya makombora yameua raia wengi huko pia.
Mnamo tarehe 6 Machi Oleksandra Matviichuk, mwanaharakati wa haki za raia, alituma picha ya majeneza kwenye handaki kwenye Twitter, ikiambatana na ujumbe: "Kwa hivyo, raia waliouawa katika shambulio la bomu la Urusi huko Chernihiv wamezikwa kwenye mitaro. Kwa kuwa makaburi ya jiji kuu huko Yatsevo yako chini ya mashambulizi ya makombora kila mara na wakaaji wa Urusi, wahasiriwa huzikwa kwenye msitu wa Yalivshchyna."
Oleksandr Lomako, katibu wa baraza la jiji la Chernihiv, aliambia BBC kwamba waathiriwa wa mashambulizi ya anga na makombora ya Urusi walikuwa wanazikwa katika makaburi ya muda. Alithibitisha kuwa makaburi makuu ya jiji hilo sasa hayafikiki, huku wanajeshi wa Urusi wakizunguka jiji hilo kwa pande tatu, umbali wa karibu kilomita 10 (maili sita).
"Baada ya vita tutawazika tena wafu," alisema, na kukadiria idadi ya vifo vya raia wa jiji hilo katika shambulio la bomu la Urusi kuwa karibu 200.
Shambulio moja la anga liliua watu 45 huko Chernihiv - idadi kubwa zaidi, Bw Lomako alisema - akiongeza kuwa mashambulizi ya usiku yanaua raia saba kwa wastani. "Ndege ziliangusha mabomu matatu hadi manne kwenye nyumba za makazi. Pia moja liliigonga hospitali, lakini bado inafanya kazi. Makumi ya nyumba za makazi zimeharibiwa pembezoni mwa jiji."
Pamoja na ushahidi wa maziko ya watu wengi, kuna maelezo ya makaburi ya muda.
Mama na mwana walizikwa katika ua wa jengo lao jipya la ghorofa huko Irpin, ambalo limepigwa makombora sana na Warusi. Picha ya kaburi ilishirikiwa sana na Waukraine, na ujumbe wa twitter wa mwandishi wa habari Olga Rudenko ilionyesha Marina Met na mtoto wake Ivan wakifurahia maisha huko Kyiv kabla ya uvamizi.
Kwa wale ambao wapendwa wao wamekumbana na athari za kuzingirwa na kushambuliwa kwa makombora na majeshi ya wavamizi, bila shaka kuzikwa katika makaburi ya muda kutakuwa na aibu ya mwisho.