Wafanyakazi wa Ericsson walitekwa nyara baada ya kutumwa kufanya mazungumzo na IS

An Islamic State of Iraq and the Levant (ISIL) militant holds up a black banner and a rifle on a street in the city of Mosul on 23 June 2014

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanamgambo wa IS walichukua udhibiti wa Mosul mnamo Juni 2014 kabla ya kusonga mbele kaskazini mwa Iraq.

Kampuni ya simu ya Ericsson iliweka maisha ya wakandarasi hatarini kwa kusisitiza waliendelea kufanya kazi katika eneo linalodhibitiwa na kundi la Islamic State [IS] nchini Iraq, kulingana na ripoti iliyovuja ya Ericsson iliyoonekana na BBC News Arabic.

Hii ilisababisha kutekwa nyara na wanamgambo wa IS, ripoti imegundua.

Ericsson ni mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya mawasiliano duniani na mdau mkuu katika usambazaji wa mitandao ya 5G nchini Uingereza, baada ya kuchukua nafasi ya kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei baada ya wasiwasi wa kiusalama.

Ufichuzi wa hivi punde unafuatia kukiri kwa wiki iliyopita kwa Mtendaji Mkuu wa Ercisson Borje Ekholm - katika kujibu waraka uliovuja - kwamba pesa zililipwa na kampuni kufikia njia za haraka za usafiri nchini Iraq wakati huo, na kwamba IS inaweza kuwa wapokeaji.

Zaidi ya $5bn ilifutwa kutoka kwa thamani ya soko ya Ericsson baada ya maoni ya Bw Ekholm.

Hati hiyo, iliyopatikana na Muungano wa Kimataifa wa Wanahabari [ICIJ] na kushirikiwa na BBC na washirika wengine 29 wa vyombo vya habari, ni ya uchunguzi wa ndani wa 2019 kuhusu shughuli za ufisadi na hongo katika nchi 10.

Ufichizu mwingine mkubwa zaidi ulihusu shughuli zake nchini Iraq.

Wakati IS ilipouteka mji wa pili wa Iraq, Mosul, mnamo Juni 2014, mwanasheria mkuu wa Ericsson alipendekeza kuzima operesheni ya kampuni hiyo nchini Iraq, lakini mameneja wakuu walipuuza hili, ripoti iligundua.

Walihisi kuwa kitendo kama hicho "kilikuwa cha haraka", na "itaharibu", biashara ya Ericsson nchini, waraka unasema.

Msisitizo wake kwamba wakandarasi wa kampuni hiyo waliendelea kufanya kazi katika eneo linaloshikiliwa na IS uliweka maisha hatarini kwa sababu kundi hilo la wanamgambo kisha lilishika mateka wanakandarasi kadhaa, ripoti hiyo iligundua.

Affan alikuwa miongoni mwa kundi la wahandisi waliokuwa wakifanya kazi kwa Ericsson wakati IS ilipotwaa jiji hilo.

Alitumwa na barua kwa niaba ya kampuni hiyo kuomba ruhusa kutoka kwa kikundi cha kigaidi ili waendelee kufanya kazi huko.

Lakini mara tu alipowasili, walikutana na lori lililojaa watu wenye silaha waliomkamata, aliambia shirika la utangazaji la Ujerumani NDR, mshirika mwingine wa vyombo vya habari vya ICIJ.

Kisha mpiganaji wa IS alitumia simu yake kuwapigia mameneja wa Ericsson na kuitaka kampuni hiyo kulipa $2.4m kufanya kazi katika eneo hilo, anasema.

"Yeye [mwanachama wa IS] alisema kwamba ikiwa wewe [Ericsson] hutalipa, mtu huyu uliyemtuma na wengine wote wanaokufanyia kazi watawindwa na sisi, tutawaleta hapa. Mmoja baada ya mwingine".

Affan aliwekewa kizuizi cha nyumbani kulingana na meneja wa Ericsson kisha akaacha kujibu simu zake. "Alinitelekeza, alizima simu na kutoweka."

BBC na ICIJ ziliwasiliana na mameneja wa Ericsson - ambaye mmoja wao bado anafanya kazi na kampuni - ambaye alipokea simu kutoka kwa IS, lakini walikataa kutoa maoni.

Affan, ambaye ametajwa katika ripoti ya Ericsson, aliachiliwa baada ya mwezi mmoja.

Wakati Affan anashikilia kuwa aliachwa na Ericsson, ripoti inasema kwamba mmoja wa washirika wa kampuni hiyo, "alifanya mipango "na IS ili kuhakikisha kuachiliwa kwake na kuiruhusu kampuni hiyo kuendelea na kazi yake huko Mosul.

Ripoti hiyo haitambui mipango hiyo ilikuwa nini.

Huu haukuwa mwingiliano wa Ericsson tu na IS.

Mkandarasi wa uchukuzi wa kampuni hiyo alitumia njia ya haraka kupitia nchi iitwayo "Speedway" ambayo ilikwepa vituo vya ukaguzi vya serikali lakini ikapitia eneo la IS, ripoti hiyo iligundua.

Wachunguzi wa Ericsson walisema walipata ushahidi wa uwezekano wa malipo ya hongo kwa wanamgambo katika njia hii.

Afisa mmoja mkuu wa serikali ya mawasiliano ya simu mjini Mosul ambaye hataki jina lake litajwe kwa kuhofia kupoteza kazi yake, aliwaambia washirika wengine wa ICIJ wa vyombo vya habari: "Ericsson alijua vyema kinachoendelea. Hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye angeshughulika moja kwa moja na IS, wote wanafanya hivyo kupitia kwa wakandarasi wadogo. Wanamgambo wangechukua asilimia kutoka kwa kila senti inayolipwa Mosul kwa mradi au kazi yoyote. Hivi ndivyo walivyokusanya mamilion

Hati ya ndani ya Ericsson inafichua utamaduni ulioenea wa shughuli za ufisadi na kutoa hongo ya jumla ya mamilioni ya dola katika nchi 10 tofauti.

Makao makuu ya Ericsson Stockholm, Sweden

Chanzo cha picha, Getty Images

Ufisadi huo ulienea hadi kwenye mfuko duni wa maafisa wa Lebanon kwa miaka kadhaa ambao ulikuwa na jumla ya karibu $1m pamoja na zawadi kama vile safari ya kifahari ya $50,000 kwenda Stockholm kwa Waziri wa zamani wa Telecom ya Lebanon, Boutros Harb.

Bw Harb aliambia BBC kwamba alikuwa ameenda kwa safari ya kikazi ya siku tatu nchini Uswidi iliyogharamiwa na Ericsson.

Lakini hajapokea zawadi au kupata manufaa yoyote.

Aliongeza kuwa hakufahamu uchunguzi wowote wa ndani wa Ericsson.

Wachunguzi pia waligundua malipo ya $50,000 kwa shirika la hisani lililounganishwa na familia ya bilionea Barzani, inayotawala eneo lenye uhuru wa Kurdistan ya Iraq na kumiliki mtandao wa simu za mkononi wa Korek.

Ripoti haikuweza kubaini pesa zilienda wapi.

Msemaji wa Sirwan Barzani hakujibu maswali yetu maalum lakini alisema "Sirwan Barzani anatazamia siku ambayo Daesh (IS) haitakuwa tishio tena na yeye na wenzake Peshmerga wanaweza kutumia muda zaidi na familia zao."

Mnamo mwaka wa 2019, Ericsson ilifikia makubaliano ya $ 1bn na mamlaka ya Marekani kufuatia madai ya ufisadi ulioenea katika nchi tano.

Ericsson haijafafanua ikiwa ufichuzi huo mpya ulifichuliwa kwa Idara ya Haki ya Marekani wakati wa suluhu hiyo.

Idara ya Haki ilikataa kutoa maoni kuhusu kesi ya Ericsson.

Ericsson hakujibu maswali mahususi ya BBC lakini alisema inaendelea kufanya kazi na wakili wa nje - kukagua matokeo na urekebishaji unaotokana na uchunguzi wa 2019 ili kubainisha hatua zozote za ziada ambazo kampuni inapaswa kuchukua.