Pandora Papers: Utajiri wa siri na shughuli za viongozi wa ulimwengu wafichuliwa

Vladimir Putin, Ilham Aliyev, King of Jordan
    • Author, Na Pandora Papers reporting team
    • Nafasi, BBC Panorama

Utajiri wa siri na shughuli za viongozi wa ulimwengu, wanasiasa na mabilionea umefichuliwa katika moja ya uvujaji mkubwa wa nyaraka za kifedha.

Baadhi ya viongozi wa sasa na wa zamani 35 na zaidi ya maafisa 300 wa umma wameonyeshwa kwenye faili kutoka kwa kampuni zilizosajiliwa katika mataifaya nje , zilizopewa jina la Pandora Papers.

Zinafichua jinsi Mfalme wa Jordan alikusanya kwa siri mali ya thamani ya £ 70m Uingereza na Marekani

Nyaraka hizo zinaonyesha pia jinsi Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair na mkewe waliokoa £ 312,000 kwa ushuru wa stempu wakati walinunua ofisi ya London.

Wanandoa hao walinunua kampuni moja ya pwani iliyomiliki jengo hilo.

Stakabadhi hizo zilizovuja pia zinamhusisha Rais wa Urusi Vladimir Putin na mali za siri huko Monaco, na inaonyesha Waziri Mkuu wa Czech Andrej Babis - anayekabiliwa na uchaguzi baadaye wiki hii - alishindwa kutangaza kampuni ya uwekezaji iliyofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru iliyotumika kununua majengo mawili ya kifahari kwa pauni milioni 12 kusini mwa Ufaransa .

Ni ya hivi karibuni katika safu ya uvujaji kwa miaka saba iliyopita, kufuatia FinCen Files, the Paradise Papers, the Panama Papers na LuxLeaks.

Uchunguzi wa faili hizo ni mkubwa zaidi uliyoandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ), na zaidi ya waandishi wa habari 650 wakishiriki.

BBC Panorama katika uchunguzi wa pamoja na Guardian na washirika wengine wa vyombo vya habari wamepata nyaraka milioni 12 kutoka kwa kampuni 14 za huduma za kifedha katika nchi zikiwemo Visiwa vya Virgin vya Uingereza, Panama, Belize, Cyprus, Falme za Kiarabu, Singapore na Uswizi.

Graphic showing size of Pandora Papers leak
1px transparent line

Baadhi ya waliotajwa wanakabaliwa na madai ya ufisadi, utakatishaji fedha na ukwepaji kodi ulimwenguni.

Lakini moja ya ufichuzi mkubwa ni jinsi watu mashuhuri na matajiri wamekuwa wakianzisha kihalali kampuni kununua mali kwa siri nchini Uingereza.

Hati hizo zinafichua wamiliki wa kampuni zingine 95,000 zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru nyuma ya ununuzi huo.

Inadhihirisha kutofaulu kwa serikali ya Uingereza kuanzisha daftari la wamiliki wa mali za pwani licha ya kuahidiwa mara kwa mara kufanya hivyo, huku kukiwa na wasiwasi wanunuzi wa mali wanaweza kuwa wanaficha shughuli za utakatishaji fedha.

Rais wa Azabajani, Ilham Aliyev na familia yake, ambao wameshtumiwa kwa kupora nchi yao wenyewe, ni mfano mmoja.

Uchunguzi uligundua kuwa Aliyevs na washirika wao wa karibu wamehusika kwa siri katika mikataba ya ununuzi wa mali nchini Uingereza yenye thamani ya zaidi ya pauni milioni 400.

Ufichuzi huo unaweza kuifedhehesha serikali ya Uingereza, kwani Aliyevs wanaonekana walipata faida ya pauni milioni 31 baada ya kuuza moja ya mali zao London kwa Crown Estate - himaya ya mali ya Malkia ambayo inasimamiwa na Hazina na inaleta pesa kwa taifa.

Shughuli nyingi kwenye hati hazihusishi makosa ya kisheria.

Lakini Fergus Shiel, kutoka ICIJ, alisema: "Hakujawahi kuwa na kitu chochote kwa kiwango hiki na inaonyesha ukweli wa kile kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru zinaweza kusaidia watu kuficha pesa taslimu au kuepuka ushuru."

Aliongeza: "Wanatumia akaunti hizo za kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru, amana hizo za pwani, kununua mamia ya mamilioni ya dola za mali katika nchi zingine, na kutajirisha familia zao, kwa gharama ya raia wao."

ICIJ inaamini uchunguzi huo ni kama "kufungua sanduku juu ya mambo mengi kwa hivyo jina la Pandora Papers.

Mfalme wa Jordan na majumba ya Malibu

Properties bought by the King of Jordan in Malibu

Hati za kifedha zilizovuja zinaonyesha jinsi Mfalme wa Jordan alivyokusanya milki ya mali nchini Uingereza na Marekani yenye thamani ya zaidi ya pauni milioni 70 (zaidi ya $ 100m).

Wanatambua mtandao wa kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza na sehemu zingine zisizotoza ushuru zinazotumiwa na Abdullah II bin Al-Hussein kununua nyumba 15 tangu alipochukua madaraka mnamo 1999.

Ni pamoja na majumba matatu ya £ 50m kwenye karibu na fuo za bahari huko Malibu, California, na mali huko London na Ascot nchini Uingereza.

Mali yake imejengwa huku Mfalme Abdullah akishtumiwa kwa kusimamia serikali ya kimabavu, na maandamano yalifanyika katika miaka ya hivi karibuni wakati wa hatua za kubana hali ya maisha na kuongezeka kwa ushuru.

Mawakili wa Mfalme Abdullah walisema mali zote zilinunuliwa na utajiri wake kibinafsi, ambao pia hutumia kufadhili miradi kwa raia wa Jordan.

Walisema ni kawaida kwa watu mashuhuri kununua mali kupitia kampuni za pwani kwa sababu za faragha na usalama.

Miongoni mwa ufichuzi mwingine katika Pandora papers:

• Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na watu sita wa familia yake walimiliki kwa siri mtandao wa kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru. Wamehusishwa na kampuni 11 - moja ambayo ilithaminiwa kuwa na mali ya $ 30m

• Wanachama wa duru ya ndani ya Waziri Mkuu wa Imran Khan, pamoja na mawaziri wa baraza la mawaziri na familia zao, wanamiliki kwa siri kampuni na amana zinazoshikilia mamilioni ya dola

• Kampuni ya sheria iliyoanzishwa na Rais Nicos Anastasiades wa Kupro inaonekana kutoa wamiliki bandia kumficha mmiliki halisi wa safu ya kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru - mwanasiasa wa zamani wa Urusi ambaye alikuwa ameshtakiwa kwa ubadhirifu. Walakini, kampuni ya sheria inakataa hii

• Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alihamisha hisa yake katika kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru kabla tu ya kushinda uchaguzi wa 2019

• Rais wa Ecuador Guillermo Lasso, mfanyakazi wa zamani wa benki, alibadilisha wakfu mmoja wa Panama ambao ulitoa malipo ya kila mwezi kwa wanafamilia wake wa karibu na amana iliyoko South Dakota nchini Marekani

Hakuna ushuru wa stempu kwenye ofisi ya Blair iliyonunuliwa

Tony and Cherie Blair in 2020

Chanzo cha picha, Getty Images

Hakuna maoni katika Pandora Papers kwamba Tony na Cherie Blair walikuwa wakificha utajiri wao.

Lakini hati zinaonyesha ni kwanini ushuru wa stempu haukulipwa wakati wenzi hao walinunua mali ya pauni milioni 6.45.

Waziri mkuu wa zamani wa Labour na mkewe Cherie ambaye ni wakili walipata jengo huko Marylebone, London katikati, mnamo Julai 2017 kwa kununua kampuni iliyofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru iliyokuwa inamiliki jengo lenyewe

Ni halali kupata mali nchini Uingereza kwa njia hii na ushuru wa stempu haulazimiki kulipwa - lakini Bwana Blair hapo awali alikuwa akikosoa mianya ya ushuru.

Jumba hilo la mjini huko Marylebone, katikati mwa London, sasa ni makao ya kampuni ya ushauri wa kisheria ya Bi.Blair, ambayo inashauri serikali ulimwenguni kote, na pia wakfu wake wa wanawake.

Bi Blair alisema wauzaji walikuwa wamesisitiza wanunue nyumba hiyo kupitia kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru

Alisema walirudisha mali chini ya sheria za Uingereza na watawajibika kulipa ushuru wa faida ikiwa wataiuza siku zijazo.

Wamiliki wa mwisho wa mali hiyo walikuwa familia yenye uhusiano wa kisiasa nchini Bahrain - lakini pande zote mbili zinasema kuwa hapo awali hawakujua ni nani walikuwa wakishughulika naye.

Mvulana ambaye alikuwa na mali ya £ 33m London

Mayfair office building bought by
Maelezo ya picha, Jngo hili la Mayfair liliuzwa kwa kampuni ya muda mwaka 2009

Nyaraka zingine zinaonyesha jinsi familia tawala ya Azerbeijan Aliyev imepata mali ya Uingereza kwa siri kwa kutumia kampuni zilizofunguliwa katika maeneo yenye unafuu wa ulipaji ushuru

Faili hizo zinaonyesha jinsi familia hiyo - iliyoshtumiwa kwa muda mrefu kwa ufisadi katika taifa hilo la Asia ya Kati - ilinunua majumba 17, pamoja na jengo la ofisi ya pauni milioni 33 huko London kwa mtoto wa rais wa miaka 11 Heyder Aliyev.

Jengo hilo huko Mayfair lilinunuliwa na kampuni inayomilikiwa na rafiki wa familia ya Rais Ilham mnamo 2009. lilihamishiwa mwezi mmoja baadaye kwa Hedyer.

Utafiti pia unaonyesha jinsi ofisi nyingine inayomilikiwa na familia iliyo karibu iliuzwa kwa Crown Estate kwa pauni milioni 66 mnamo 2018.

Crown Estate ilisema ilifanya ukaguzi unaohitajika kisheria wakati wa ununuzi lakini sasa inaangalia suala hilo.

Serikali ya Uingereza inasema inadhibiti utapeli wa pesa na sheria kali na utekelezaji, na kwamba itaanzisha rejista ya kampuni za pwani zinazomiliki mali za Uingereza iwapo muda wa bunge utaruhusu

Pandora Papers banner

Nyaraka za Pandora ni uvujaji wa hati na faili karibu milioni 12 zinazoonyesha utajiri wa siri na shughuli za viongozi wa ulimwengu, wanasiasa na mabilionea. Takwimu hizo zilipatikana na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi huko Washington DC na imesababisha moja ya uchunguzi mkubwa zaidi ulimwenguni. Zaidi ya waandishi wa habari 600 kutoka nchi 117 wameangalia utajiri uliofichwa wa watu wenye nguvu zaidi duniani. BBC Panorama na Guardian wameongoza uchunguzi nchini Uingereza.