Mfahamu Dkt. Riek Machar, na imani zake za msituni kwenye mgogoro wa Sudan Kusini

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mfululizo wa Makala ya wiki hii tunawaangazia wanasiasa ambao wamekuwa mwiba kwa serikali zilizopo madarakani katika eneo la Afrika mashariki na jinsi wanavyoziwajibisha serikali hizo.
Baadhi ya wanasiasa ni maafisa wa serikali wanaopigana dhidi ya serikali hizo kutoka ndani.

Sudan Kusini, ni nchi ambayo iko kwenye vita, kwa miongo kadhaa sasa eneo hilo limekuwa kama uwanja wa vita huku maelfu ya watu wakiuawa.
Miongoni mwa watu muhimu wanaozungukwa na mgogoro wowote wa Sudan Kusini, basi huwezi kuacha kumtaja Dkt. Riek Machar Teny Dhurgon ambaye ndiye Makamu wa Rais wa sasa wa taifa hilo changa kabisa Afrika chini ya Rais Salva Kiir, akirejea kwenye nafasi hiyo mwezi Februari mwaka 2020.
Machar ndiye kiongozi wa kundi la waasi la SPLM-IO ambalo liliasisiwa mwaka 2014 kufuatia vita vya mwaka 2013 na amekuwa mpinzani wa kihistoria wa Rais Kiir.
Dkt. Riech ni nani hasa?

Chanzo cha picha, Reuters
Riek Machar Teny Dhurgon alizaliwa mnano Novemba 26, 1952 huko Leer, katika jimbo la Unity , akiwa mtoto wa 27 wa Chifu Ayod na Leer.
Anatokea kwenye jamii ya Dok-Chiengluom ya watu wa Nuer, na amesomea uhandisi katika chuo kikuu cha Khartoun Sudan, kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Bradford, Uingereza na kupata shahada yake ya uzamivu (PHD) ya masuala ya uhandisi wa mitambo, mwaka 1984.
Machar alikuwa anaitwa tuut dhoali au Doth kwa kiingereza, kwa maana ya 'kijana mtu mzima', au kijana ambaye ni kama mtu mzima kutokana na fikra zake za kiutu uzima zisizolingana na umri wake kwa wakati huo.
Machar alimuoa Emma McCune, mfanyakazi wa kutoa misaada kutoka Uingereza. Alikufa mwaka 1993 kwenye ajali ya gari jijini Nairobi akiwa na miaka 29 tena mjamzito. Mke wake wa pili , Angelina Teny, ni mmoja wa wanasiasa wanawake wenye sifa kubwa nchini Sudan Kusini. Alikuwa waziri wa nishati na madini katika serikali ya mpito kati ya mwaka 2005 na 2010.
Harakati za kisiasa zilizomuingiza madarakani Machar
Katika harakati zake za kuleta fikra mpya Sudan na mabadiliko mapya, akiwa na John Garang, Dr. Machar alikuwa miongoni wa waliokuwa mstari wa mbele kwenye mgogoro kati ya watu wa Nuer and Dinka.
Machar alijiunga na kundi la SPLM/A wakati wa vita kubwa ya pili ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vilivyodumu kati ya mwaka 1983-2005. Lakini mwaka 1991 akakorofishana na swahiba wake na aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo la SPLM/A, Garang na kuamua kuanzisha kundi lingine aliloliita SPLM/A-Nasir.
Mwaka 1997 Riek akaingia kwenye makubaliano na serikali ya Sudan na kuwa kiongozi wa serikali chini ya vikosi vya majeshi ya Ulinzi ya Sudan Kusini (SSDF). Mwaka 2000 akajiondoa SSDF na kuanzisha kundi lake la wapiganaji aliloliita SPDF, kabla ya mwaka 2002 kujiunga tena na SPLA safari hii akiwa kama kiongozi wa jeshi mwandamizi..
Baada ya kifo cha John Garang, mwezi Julai mwaka 2005, Riek Machar akawa makamu wa Rais wa Sudan, cheo alichotawazwa nacho katika Sudan Kusini iliyo huru kuanzia Julai 9, 2011.
Salva Kirir na Machar na undugu wao wa Paka na Panya

Chanzo cha picha, Getty Images
Salva Kiir, amekuwa Rais wa Sudan Kusini toka ilipopata uhuru mwaka 2011, akiongoza taifa hilo kwa tabu, kutokana na mapigano ya mara kwa mara, ambayo kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa na msaidizi wake, Dr. Machar.
Wanacheka pamoja asubuhi kama viongozi wa nchi, Rais na makamu wake , lakini usiku wanatafutana kama paka na panya, vikosi vya serikali chini ya Rais Kiir, na kundi la Machar linalopambana kutaka ukuu wa taifa hilo.
Pamoja na kuingia makubaliano mara kadhaa, bado viongozi hao wanaohasimiana na walio katika serikali moja, wanatazamana kwa jicho la paka na panya.
Machar alitangaza mbele ya umma mwezi Februari 2013 kwamba ana mpango wa kumuondoa Rais Kiir kwenye kiti hicho cha urais. Salva Kiir akaona isiwe tabu akamtimua yeye na baraza zima la mawaziri. Badaa ya kutimuliwa Machar alisema hatua hiyo ya Rais Kiir ilikuwa ni ya kidikteta.
Bahati mbaya kutimuliwa kwake kukachochea mgogoro mkubwa na ukawa mwanzo wa vita kubwa ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, vilivyodumu kwa miaka karibu mitano na kusababisha vifo vya watu karibu 400,000.
Baada ya jitihada za muda mrefu za jumuiya za kimataifa hatimaye Rais Kiir na Machar walikubaliana na Machar akateuliwa tena kushika nafasi hiyo ya umakamu wa rais Februari 22, mwaka 2020 akiwa sehemu ya serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa chini ya Salva Kiir.
Nafasi hiyo ilirejea mikononi mwake, baada ya makubaliano ya Amani ya Septemba mwaka 2018, ambayo yalieleza kwamba atachukua wadhifa huo kuanzia Februari 2019 , lakini ikasogezwa mbele mpaka Februari 2020.
'Haonekani kama mtu mzuri'
Pamoja na kwamba, Machar ni mtu anayemnyima sana usingizi, Rais Kiir, haonekana kama mtu anayeweza kuja na suluhu mbadala wa matatizo ya Wasudan Kusini. Anaonekana kama mtu anayewagawa zaidi wasudan kuliko kuwaunganisha. Anaonekana hivyo ndani ya kundi la SPLA/SPLM linalotawala nchi hiyo.
Analaumiwa kwa mauaji ya mwaka 1991 yaliyosababisha vifo vya maelfu ya Wasudan, akionekana na wapiganaji wengi wa wakati huo kama msaliti katika mazungumzo ya Amani ya Khartoum ya mwaka 1997.
Alisaini makubaliano ya Amani na serikali ya Sudan, ambayo yalimpa cheo cha makamu wa Rais na mwenyekiti wa Baraza ambalo kiufundi ndilo lililokuwa linatawala Serikali.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alirejea SPLA mwaka 2002, baada ya mazungumzo, mengine ya Amani ya mwaka 2005 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kupatikana kwa uhuru wa Sudan Kusini.
Aliendelea kushika wadhifa huo hata baada ya Sudan Kusini kupata uhuru mwaka 2011 mpaka alipotimuliwa mwaka 2016.
"Ana historia tete sana. Sidhani kama watu wengi wa Sudan Kusini wanamuona kama kiongozi wa taifa," alisema Jok Madut Jok, afisa wa zamani wa serikali.
"Ni mtu mwenye tamaa ya madaraka ya juu, hakuna lingine muhimu analowaza," aliiambia Reuters.
Tangu kifo cha kiongozi wa SPLA, John Garang, kilichotokana na ajali ya helkopta, kundi hilo limekuwa likihaha kutafuta mbadala wake, ambaye anaweza kuirejesha utulivu nchini humo, Dr. Machar haonekani kama mtu wa suluhu, akitazamwa kama miongoni mwa wapenda suluhu za msituni zaidi ambazo zimegharimu maisha ya raia wengi wa Sudan Kusini.
Hatahivyo kuna wale wanaomsifu
Akitoka katika kabila la pili kwa ukubwa nchini Sudan Kusini, Machar mwenye mwanya alionekana kuwa mtu muhimu uongozini kwa lengo la kukuza umoja kati ya kabila lake na lile la Dinka walio wengi.
Akimkumbuka mwaka wa 2005 , mwandishi wa BBC David Amanor alisema kwamba ni mtu mwenye maumbile ya uongozi.
"Ana sura nzuri lakini pia mpole. Anaongea vizuri na ameelimika vizuri," alisema.
Wakati huo, Bwana Machar alikuwa amebadilisha gwanda lake la kijeshi kwa suti ya Kiingereza, akichukua jukumu la mpatanishi kati ya serikali ya Uganda na LRA.
Aliona LRA kama tishio kubwa, akiamini kuwa inaweza kuyumbisha Sudan Kusini, kwasababu ilikuwa na kambi za kijeshi nchini humo.














