Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed awataka raia kuwasaidia wanajeshi kupigana vita dhidi ya waasi wa TPLF Tigray

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri mkuu wa Ehiopia ametoa wito kwa raia kujiunga na jeshi katika vita dhidi ya waasi katika jimbo la Tigray
Abiy Ahmed aliwaomba raia wote walio na uwezo kuonyesha uzalendo wao kwa kushiriki katika vita hivyo , vinavyoendelea katika eneo la kaskazini mwa taifa hilo.
Mapigano yameongezeka tangu mwezi Juni wakati waasi , wanaoongozwa na chama cha TPLF walipoteka eneo kubwa la Tigray katika vita.
Hatua hii inajiri baada ya jeshi kuondoka na kutangaza kumalizika kwa vita.
Katika ishara za kuonesha jinsi jeshi hilo linavyohitaji kila mbinu , bwana Abiy - mshindi wa tuzo ya Nobel , alisema kwamba taifa lote linapaswa kuwasaidia wanajeshi ili kuwashinda wapiganaji wa TPLF.
''Vyombo vya habari, wasanii, na wanaharakati wa kijamii wanatarajiwa kuchangia katika kuimarisha uungwaji mkono wa raia kwa taifa lao'', alisema waziri mkuu katika taarifa hiyo.
''Kila raia wa Ethiopia lazima afanye kazi kwa bidii na vyombo vya usalama ili kuwa macho na masikio ya taifa ili kuwasaka majasusi na maajenti wa magaidi wa TPLF''.
Wapiganaji wa TPLF wametajwa kuwa shirika la kigaidi na serikali.
Lakini kundi hilo linasema ndilo linaloendesha serikali rasmi ya jimbo hilo la Tigray.
Mapiganao yalizuka mwezi Novemba 2020 kati ya serikali na wapiganaji wa chama chaTPLF , ambacho kilitawala Ethiopia kwa miongo kadhaa na sasa kinadhibiti Tigray.
Mzozo huo umewalazimu zaidi ya watu milioni 2 kutoroka makazi yao , huku mamia ya maelfu wakijipata katika hali ya ukame..

Wiki sita zilizopita , serikali ilitangaza kusitishwa kwa vita kwasababu ya hali ya kibinadamu , baada ya kupoteza udhibiti wa maeneo muhimu ikiwemo mji mkuu wa jimbo hilo Mekelle.
Ilisema kwamba kusitishwa kwa vita hivyo kutaendelea hadi msimu wa kilimo utakapokamilika.
Msimu wa upanzi unaanza mwezi Juni na kuisha mwezi Septemba.
Wiki iliopita , kamanda wa waasi hao aliambia BBC kwamba kuingia kwa wapiganaji wake katika majimbo jirani kulilenga kuondoa vizuizi ambayo vimekuwa vikizuia misaada kuingia katika eneo hilo.
Lakini taarifa ya waziri mkuu iliwashutumu waasi hao kwa kutafuta msaada na badala yake kutowaruhusu wakulima kuendelea na upanzi wa mimea."Imeonekana kuwa wakulima wa Tigray hawataweza kulima kwa usalama isipokuwa tu Watigray watatenganishwa na kundi la kigaidi," Bw Abiy alisema.
Taarifa hiyo pia ililenga wengine katika jamii ya kimataifa. Waziri mkuu alilaumu "mikono ya kigeni" kushiriki katika vita, na alidai wengine walikamatwa "mikono mitupu inayounga mkono [vikosi vya Tigray] chini ya mwamvuli wa misaada ya kibinadamu."
Serikali ya Ethiopia wakati mmoja iliita mzozo wa Tigray "operesheni ya sheria na utulivu", na mnamo Novemba ilitangaza ushindi. Lakini ni ishara ya mabadiliko makubwa ambayo Waziri Mkuu Abiy Ahmed sasa anatoa wito kwa kila Muethiopia wa umri kujisajili.
Sio Tigray pekee ambayo iko hatarini, mikoa ya karibu ya Afar na Amhara inaonekana kukabiliwa na tishio.
Wiki iliyopita, vikosi vya Tigray viliteka mji wa kale wa Lalibela huko Amhara - inaonekana bila vita.
Mapigano pia yameripotiwa katika mji wa kimkakati wa Weldiya.
Wakati vikosi na wanamgambo wameendelea kupigana serikali inasisitiza jeshi la shirikisho liliacha kushiriki katika mzozo mkali mwishoni mwa Juni - wakizingatia usitishaji mapigano wa pamoja kwa sababu za kibinadamu.
"Wito kwa silaha" ya kitaifa ni taarifa ya ujasiri lakini kuna maswali juu ya nguvu ya kweli ya jeshi la shirikisho.












