Emmanuel Macron: Kwa nini Rwanda inasubiri kuombwa radhi na rais wa Ufaransa?

Macron na Kagame

Chanzo cha picha, Chesnot/Getty

Maelezo ya picha, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amerejesha mahusiano mazuri na Rais Paul Kagame wa Rwanda
    • Author, Yves Bucyana
    • Nafasi, BBC Swahili, Kigali

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kufanya ziara nchini Rwanda siku ya Alhamisi ,ziara inayoangaziwa kufungua ukurasa mpya wa historia ya uhusiano kati ya nchi mbili.

Bwana Macron atakuwa rais wa pili wa Ufaransa kutembelea Rwanda baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 tangu rais wa zamani Nicolas Sarkozy alipotembelea taifa hilo mnamo 2010. Rwanda ilivunja uhusiano wake na Ufaransa mwaka 2006 kwa shutuma za mauaji ya kimbari.

Kabla ya mauaji ya kimbari nchi mbili zilikuwa na urafiki wa kipekee.

Rais Macron alisema ziara yake nchini Rwanda itakuwa ya "sera ya ukumbusho, uchumi na kuangazia siku zijazo." Na kuongeza kwamba yeye pamoja na Rais Kagame walikubaliana ''kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano na kufanya miradi ya maendeleo.''

Mashirika ya manusura yataka kuombwa radhi

Ziara ya Macron nchini Rwanda imeelezwa na mashirika ya manusura wa mauaji ya kimbari kuwa ishara nzuri katika kuweka mambo sawa.

Mwenyekiti wa shirika la manusura la IBUKA Bwana Egide Nkuranga ameiambia BBC kwamba ni ziara ya matumaini kuwa hatimae huenda waliofanya mauaji ya kimbari na kukimbilia Ufaransa watashikwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Juni 1994 - Wanajeshi wa Ufaransa kwenye doria wakilipita kundi la vijana wa kuhutu wenye silaha

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Juni 1994 - Wanajeshi wa Ufaransa kwenye doria wakilipita kundi la vijana wa kuhutu wenye silaha

''Tunachosubiri kwa ziara ya Bwana Macron ni kutoa haki ya sheria kwa manusura wa mauaji ya kimbari kwa kuwakamata waliohusika na kuwafikisha mahakamani,''alisema Egide Nkuranga .

Kadhalika jumuiya ya IBUKA inaona kwamba itakuwa vyema Rais Macron akiomba radhi kutokana na nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari.

Egide alisema: ''Litakuwa jambo la kututia moyo ikiwa Rais Macron ataomba radhi kwa yaliyotokea. Ni vizuri kwamba ripoti ya Ufaransa ilisema nchi hiyo ilikuwa na majukumu mazito katika mauaji ya kimbari. Tunasubiri kwa hamu hotuba yake, kama ataomba msamaha tutafurahi, ni kitendo cha kishujaa.''

Nchi za Ubelgiji, Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa ziliomba radhi kwa kushindwa kusaidia kukomesha mauaji ya kimbari.

Wachambuzi wa siasa wanasemaje?

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba ziara ya Rais Macron ni hatua kubwa ya kurejesha uhusiano baina ya Rwanda na Ufaransa.

Mchambuzi wa siasa za maziwa makuu Halidi Hassan ameiambia BBC Kwamba kila nchi itanufaika pakubwa na kurejea kwa mahusiano.

''Kwanza Rwanda ilikuwa ikikumbana na vikwazo katika jumuia ya kimataifa kutokana na shinikizo la kidiplomasia kutoka kwa Ufaransa.kadhalika ,Rwanda itanufaika na Ufadhili kutoka kwa Ufaransa na washirika wakem,hatua moja wapo ikiwa ni uzinduzi wa kituo cha utamaduni wa Ufaransa mjini Kigali,'' anaeleza Hassan.

''Kumbuka pia kwamba Rwanda imekuwa ikitumia ushawishi wake kwa mataifa ya Afrika kusimama kidete na kupinga kila kinachoitwa 'ukoloni mamboleo ' wa Ufaransa. Hayo pia Rwanda itayasitisha,'' aliendelea kusema Halid Hassan.

Jinsi ripoti mpya zilivyobadili hali

Rais Sarkozy akiwa Kigali

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwaka 2010 Nicolas Sarkozy alikua Rais wa kwanza wa Ufaransa kutembelea Rwanda baada ya mauaji ya kimbari na kukiri kuwa nchi yake "ilifanya makosa makubwa katika kuelewa [nini kilikuwa kinatokea]".

Alipoingia madarakani mnamo 2017, Emmanuel Macron alisema alitaka kusuluhisha suala la uhusiano uliovunjika kati ya Rwanda na Ufaransa baada ya mauaji ya kimbari.

Serikali ya Rwanda iliituhumu Ufaransa kwa kuhusika katika upangaji, utekelezaji na kuwatorosha waliofanya mauaji ya kimbari, shutuma ambazo Ufaransa inazipinga na ambazo ziliendelea kuwa sababu kuu ya uhusiano kudorora.

Mnamo 2006 uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulisimama baada ya Jaji wa Ufaransa Jean Louis Bourgiere kutoa hati za kuwakamata maafisa wa jeshi walio karibu na Rais Paul Kagame kwa tuhuma za kuhusika na kutungua ndege iliyokuwa imembeba Rais wa zamani Juvénal Habyarimana na mwenzie wa Burundi Cyprien Ntaryamira mnamo April, 6 mwaka 1994.

Mnamo 2010 Nicolas Sarkozy alikua Rais wa kwanza wa Ufaransa kutembelea Rwanda baada ya mauaji ya kimbari 1994. Akiwa mjini Kigali Sarkozy alikiri kwamba nchi yake "ilifanya makosa makubwa katika kuelewa [nini kilikuwa kinatokea]".

Baada ya kumtimua balozi wa Ufaransa nchini Rwanda ,jumba la utamaduni wa Ufaransa lililokuwa katikati ya mji wa Kigali lilibomolewa mnamo 2014, mamlaka nchini Rwanda zilisema, jengo hilo halikufwata kanuni na ramani ya ujenzi mjini.

Katika miezi miwili iliyopita, serikali zote zilitangaza ripoti kuhusu nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda. Rais Macron na mwenzake Kagame wanakubaliana juu ya ripoti hizo kwamba zinaonyesha jukumu fulani la mamlaka ya zamani ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari.

Udunguaji wa ndege ya Habyarimana

Kufuatia mfululizo wa uchunguzi juu ya jukumu la Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda 1994, mamlaka katika nchi zote mbili yameonyeshwa kupendezwa na yaliyomo.

Wiki iliyopita , Rais wa Rwanda Paul Kagame alihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Kiafrika ulioitishwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema kuwa wanasiasa wa nchi hizo mbili wanapuuza kesi nzito kuhusu aliyedungua ndege ya Rais Juvénal Habyarimana, ambayo kwa sasa iko katika korti ya Ufaransa.

Waendesha mashtaka wanadai kwamba ndege hiyo ilidunguliwa na wanajeshi wa RPF,chama tawala nchini Rwanda kinachokanusha madai hayo.

Mmoja wa mawakili wa wathiriwa wa mkasa huo , Philippe Meilhac, ameiambia BBC kwamba baada ya mahakama mbili kutupilia mbali kesi hiyo sasa waliwasilisha kesi katika mahakama ya juu mjini Paris na kwamba wanasubiri uamuzi utakaotolewa na mahakama hiyo:

''Mahakama ya Ufaransa kupitia majaji wanaofanya upelelezi kwanza iliamuru kesi kusitishwa mnamo mwaka 2018,uamuzi uliothibitishwa na mahakama ya rufaa mwaka 2020,lakini tulikata rufaa katika mahakama ya juu kabisa ambayo ndiyo ya mwisho nchini Ufaransa.Swala la kesi ya udunguaji wa ndege iko katika mahakama hiyo tunasubiri uwamzi wa mahakama hiyo utakaotolewa mnamo miezi michache ijayo.''

Kuhusu swala la kuboreka kwa uhusiano baina ya Rwanda na Ufaransa kuweza kukwamisha kwa namna moja ama nyingine wakili Philippe Meilhac amesema matumaini yako ni kwamba vyombo vya sheria Ufaransa viko huru:

''Sikiliza…uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia kati ya Rwanda na Ufaransa naweza kusema kwamba uliathiri sana kesi ya utunguaji wa ndege imepita sasa miaka 20.Wakati uhusiano ulipokuwa mbaya ushirikiano ulikuwa hauwezikani.Sasa kama kuna uhusiano mzuri bila shaka nchi mbili zitakuwa na mwelekeo ulio sawa.Hata viongozi wa Ufaransa wanajua kwamba ili kurejesha uhusiano masharti ya kwanza ambayo Rwanda iliweka ni kufutilia mbali kesi kuhusu udunguaji wa ndege.Nafikiri wanasiasa wa Ufaransa watafanya kila liwezekanalo ili kesi isifanyike.Matumaini tuliyo nayo tu ni kwamba nchini Ufaransa ngazi ya sheria iko huru na hatujafika kipindi cha wanasiasa kushinikiza mahakama isipokuwa mwendesha mashtaka ambaye anafuata maagizo ya wanasiasa na alishachukua maamuzi yanayoelekea kulinda maslahi ya Ufaransa kwa kufanya kila awezavyo ili kesi hii isifanyike.Hicho ndicho kitendawili tunachokabiliana nacho''

Ripoti zilizofanywa kuhusu udunguaji wa ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana zilitayarishwa na majaji wa Ufaransa,moja ilidai kwamba ndege ilitunguliwa na askari wa RPF na ripoti ya pili iliyofanywa na Jaji Marc Trevidic ikabainisha kwamba ndege hiyo ilidunguliwa na maafisa waliokuwa karibu wa Rais Habyarimana.