Iran yasema shambulio limeuharibu vibaya mtambo wake wa nyuklia

Chanzo cha picha, Reuters
Iran itarutubisha madini ya uranium kwa asilimia 60 kujibu shambulio dhidi ya mtambo wa nyuklia linaloshukiwa kutekelezwa na Israel, Rais Hassan Rouhani anasema, hatua hiyo itaiwezesha kufikia kiwango kinachohitajika kutengeneza silaha.
Mlipuko ulilipua mfumo wa umeme wa kiwanda cha nyuklia cha Natanz siku ya Jumapili, kusababisha uharibifu wa mitambo ya kuhuisha madini ya uranium.
Bw. Rouhani ameonya waliofanya uharibifu huo kuwa hatua hiyo ni ya kulipiza kisasi "uovu wako".
Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimeelezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu hatua hiyo, zikisema haina "sababu ya msingi ya kuhuisha madini haya kwa kiwango hiki".
Maelfu ya mashine zinazotumika kurutubisha nyenzo za nyuklia zimeharibiwa katika shambulio lililotokea kwenye mtambo muhimu, Jumapili, maafisa wa Iran wamesema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Iran imelaumu Israel kwa kile ilichokiita kitendo cha "ugaidi wa kinyuklia".
Israel bado haijathibitisha wala kukanusha madai hayo, lakini kituo cha redio cha Israel kinachomilikiwa na serikali kimenukuu vyanzo vya kijasusi vikisema ilikuwa operesheni ya kimtandao ya Masaad.
Iran imesema itabadilisha mashine zilizoathirika - zile zinazotumika kuimarisha au kurutubisha, kemikali ya urani inayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia au mabomu ya nyuklia - na hata kuweka mashine za kisasa zaidi.
Pia, Jumatano imetangaza kuwa itaongeza kiwango chake cha urutubishaji - kutoka asilimia 20 hadi 60. Kiwango hicho kimekatazwa chini ya mkataba wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, huku asilimia 60 ikiwa karibu sana na asilimia 90 inayohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Israel na Uarabuni vimesema kuwa meli inayomilikiwa na Israel imeharibiwa katika shambulizi lililotokea pwani ya Milki za Kiarabu.
Maafisa ambao hawakutajwa wamenukuliwa na kituo cha televisheni cha Israel Channel 12, wamelaumu Iran kwa shambulio lililotokea katika meli ya Hyperion Ray. Ikiwa itathibitishwa, hilo litakuwa shambulizi la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya meli za Israel na Iran.

Chanzo cha picha, EPA
Je uharibifu huo ni wa kiwango gani?
Iran ilikubali kuwa mashine zake zimeharibiwa lakini haikutoa maelezo zaidi.
Hata hivyo, akizungumza katika kituo cha redio kinachomilikiwa na serikali cha Ofoq, Bwana Zakani amesema uharibifu uliofanyika ni mkubwa.
Mgogoro wa nyuklia wa Iran: Ya msingi
- Nchi zenye nguvu duniani hazina imani na Iran: Baadhi ya nchi zinaamini Iran inatafuta kuwa na nguvu ya nyuklia kwasababu inataka kutengeneza mabomu ya nyuklia - lakini Iran imekanusha madai hayo.
- Kwahiyo makubaliano yalifikiwa: Mwaka 2015, Iran na nchi 6 zilikifia makubaliano ya kihistoria. Iran ingesitisha baadhi ya shughuli zake za nyuklia kwa mabadilishano ya kumaliza adhabu kubwa, au vikwazo, ambavyo vinadororesha uchumi wake.
- Sasa tatizo liko wapi? Iran ilianza tena shughuli za nyuklia zilizopigwa marufuku baada ya aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump kujiondoa kwenye makubaliano hayo na kuiwekea tena Iran vikwazo. Hata ingawa Rais mpya Joe Biden anataka kujiunga na makubaliao hayo, pande zote zinasema kuwa zinataka kila mmoja wao achukue hatua wa kwanza.
Suala la mashine za Iran ni tata. Ikiwa zitarutubishwa kwa kiwango cha juu - jambo ambalo Iran imelikanusha - madini ya urani yanaweza kutumiwa katika utengenezaji wa mabomu ya nyuklia. Iran imesema mashine zake zinarutubisha madini ya urani katika kiwango ambacho tu kinatumika kwa matumizi ya binadamu kama vile mafuta ya nyuklia, kilimo na tiba.

Iran ilikuwa na mashine za kisasa zaidi - ambazo zilipigwa marufuku katika makubaliano ya mwaka 2015 - katika mtambo wa Natanz, siku moja kabla ya kituo hicho kushambuliwa.
Maafisa wa Marekani wa kiintelijensia wameliambia gazeti la New York Times kuwa mlipuko mkubwa umeharibu kabisa mtambo wa nyuklia uliokuwa unatoa mashine katika kituo cha chini.
Walikadiria kuwa inaweza kuchukua karibu miezi 9 kwa shughuli kuanza tena kwenye mtambo huo.
Jumatatu, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema kuwa nchi yake "italipiza kisasi" huku ikilaumu Israel kwa shambulizi lililotokea Jumapili.
Kituo kimoja cha habari cha Iran chenye kuhusishwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kilinukuliwa kikisema kuwa "mhusika mkuu" wa shambulizi hilo amebainika na operesheni inaendelea ya kuwakamata.
Taarifa zaidi kuhusu mzozo wa nyuklia wa Iran
Hivi karibuni, Israel ilitoa onyo kali dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran huku juhudi zikiendelea za kufufua makubaliano ya nyuklia ambayo yalitupiliwa mbali na aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump.
Marekani na maafisa wa Iran wanafanya mazungumzo yasio ya moja kwa moja katika mji mkuu wa Austria, Vienna, kujaribu kuondoa mkwamo uliopo huku maafisa wa nchi za Ulaya wakichukua jukumu la mpatanishi.












