Mzozo wa Tigray Ethiopia: Simulizi ya mwandishi wa BBC aliyezuiliwa

Mwandishi wa BBC Girmay Gebru, ambaye alikuwa miongoni mwa wanahabari kadhaa waliozuiliwa Mekelle, mji mkuu wa Jimbo la Tigray linalokumbwa na mzozo nchini Ethiopia, aelezea kilichomkuta:
Nilikamtwa mkesha wa siku yangu ya kuzaliwa.
Nilidhani maaskari waliokua wamejihami kwa silaha, walikua wakimtafuta mtu walipozingira duka la kahawa ambapo nilikuwa nikikutana mara na marafiki siku ya Jumatatu.
Mmoja wa maafisa hao alikuja na kuwaambia watu wawe watulivu nasi tukaendelea na gumzo letu. Lakini dakika chache baadae, tulifuatwa na maajenti wa kintelijensia waliokuwa wamevalia nguo za nyumbani.
"Nyinyi ni kina nani?" mmoja wao aliuliza kwa sauti ya hasira.
"Tuambieni majina yenu!"
"Mimi ni Girmay Gebru,"Nilisema.
Kuzabwa kofi usoni
"Ndio wewe, wewe ndiye mtu tunayemtaka." Na hapo wakanishika pamoja na marafiki zangu watano.
Kisha mbele ya watu waliokuwa wakifuatilia tukio hilo, mmoja wa maafisa hao wa intelijensia alinizaba kofi usoni, hata baada ya mimi kuwasilisha kitambulisho changu cha kitaifa na kitambulisho cha kazi cha BBC
Askari mwengine aliingialia kati na kumuomba asinipige na baada ya hapo niliingizwa kwenye gari na kuondoka.
Mambo yalifanyika haraka kiasi cha kuwa nilisahau kuulizia kwanini nimekamatwa.

Mzozo wa Tigray

Chanzo cha picha, AFP
- Mapigano yalizuka Novemba 4, 2020
- Serikali ya Ethiopia ilianzisha oparesheni dhidi ya kuvunja Tigray People's Liberation Front baada ya wapiganaji wake kuteka kambi za jeshi la muungano.
- Maelfu ya watu walikimbilia Sudan (kama unavyoona katika picha hapo juu)
- Huduma za intaneti na simu zilikatizwa na wanahabari hawakua na uwezo wa kuangazia kinachoendelea katika jimbo hilo.
- Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema vita vimemalizika mwisho wa mwezi Novemba lakini mapigano yaliendelea.
- Kumekuwa na hofu ya ukiukwaji wa haki za binadamu na hali wa watu katika eneo hilo.

Hata tulipofikishwa katika kambi ya jeshi katika mji huo hatukupewa ufafanuzi wowote.
Lakini mmoja wa maafisa wa kiintelijensia aliniambia: "Girmay, sisi ni serikali na tunajua kile unachofanya kila siku- nikamuuliza anamaanisha nini, akanijibu... najaribu kutuma ujumbe gani. Tunajua unachokula kuanzia kiamsha kinywa, chakula cha mchana na usiku."
"Niambie nimekuwa nikifanya nini," Nilimjibu. "Niambie nimekuwa nikipitisha ujumbe gani."
Tangu mzozo ulipozuka mwezi Novemba mwaka jana, Sijakua nikiwasilisha taarifa yoyote kwa niaba ya BBC kwa kuwa nialiagizwa kutilia maanani usalama wangu kwanza.
"Ni wewe utuambie kile ambacho umekuwa ukisema na kufikiria. Utaniambia baadae," alisema.
Nafasi yakupiga Simu moja
Huu sio uchunguzi bali ni onyo tu.
Tulirudishiwa simu zetu ambazo zilikuwa zimechukuliwa na maafisa wa jeshi na kuambiwa tupige simu moja
Mke wangu aliingiwa na wasiwasi nilipomueleza kilichotokea lakini nikamwambia asiwe na wasiwasi

Hatukusumbuliwa katika kambi hiyo, lakini sote tulilala sakafuni katika chumba kimoja na kupewa ndoo za plastiki kutumia kama choo.
Sote tulikuwa na wasi wasi ni nini kitakachofuata. Sikupata lepe la usingizi.
Asubuhi ilipofika, maafisa wa intelijensia waliniambia wanataka kupekua nyumba yangu na kwamba watachukua kombuyuta na simu yangu ili kupakua data zote kutoka kwa vifaa hivyo. Lakini baadae nilifahamu kuwa hawakupekua nyumba yangu kama walivyosema.
Harufu kutoka kwa shimo la choo
Pia waliniambia kwamba wanataka kunihoji mimi wakisema taarifa zote wanazohitaji ziko akilini mwangu.
Lakini licha ya hayo hawakusema kwanini wanatuzuilia.
Nilijiamini kuwa sijafanya kosa lolote.
"Mimi ni mwanahabari. Mimi ni mtu huru na unaweza kuniuliza chochote," nilisema.
Lakini sikuhojiwa siku hiyo, badala yake, asubuhi ya Jumanne tulipelekwa hadi kituo cha polisi katikati ya mji wa Mekelle na kufungiwa hapo
Hali katika kituo hicho ilikuwa mbaya sana.
Niliwekwa katika seli ndogo ambayo haikuwa na kitanda na ukubwa wake ni mita 2.5 kwa mita 31 na kujumuishwa na watu wengine watatu. Kulikuwa na joto kali na harufu mbaya kutoka kwa shimo la choo lililokuwa karibu na hapo.

Asubuhi ya Jumatano afisa wa polisi alikuja na kuniambia kukusanye vitu vyangu, akisema huenda nikaruhusiwa kwenda nyumbani.
Lakini sikupewa maelezo kwanini nimezuiliwa, japo nafahamu kwamba BBC imeomba serikali ya Ethiopia kutoa kuelezea chanzo cha kukamatwa kwangu.
Mke wangu, mama yangu mzazi na watoto wangu wote walikuwa nyumbani, walilia machozi ya furaha waliponiona
Kilichonitia hofu zaidi ni kuwa mgonjwa ndani ya seli ya polisi. Sasa sina wasi wasi napumzuka baada ya kuachiwa huru.












