Binti mfalme Latifa: Haki za wanawake Dubai ni zipi?

Kesi ya binti mfalme Latifa imeshtua dunia.
Ni binti ya mfalme wa Dubai. Kisiri alirekodi video iliyowasilishwa na BBC.
Binti huyo wa mtawala wa Dubai amemshutumu baba yake kwa kumshika mateka katika mji huo tangu alipojaribu kutoroka mwaka 2018 na kusema kwamba anahofia maisha yake.
Tangu wakati huo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa utaanzisha uchunguzi baada ya video ya mwana mfalme Latifa kuhakikiwa na kuwa kuhoji nchi ya Falme za Kiarabu.
Lakini Latifa sio mtu pekee wa familia aliyetoroka mji huo. Juni 2019, Malkia Haya binti Hussein, mke wa mtawala huyo, 45, alitorokea Ujerumani na kutafuta hifadhi ya kisiasa.
Dada yake Latifa, Shamsa pia naye alitoroka.
Ni simulizi yenye kutatanisha kwa madai ya unyanyasaji, kukandamizwa na udhibiti dhidi mwanaume mmoja mwenye nguvu zaidi katika taifa hilo.
Lakini vipi kuhusu wanawake wengine huko Dubai na nchi ya Falme za Kiarabu kwa ujumla?
Je ni kwa kiasi gani haki za fursa kwa wanawake kunategemea wanaume waliopo kwenye maisha yao?

Wanawake huko UAE wanaruhusiwa kujiendesha, kupiga kura, kufanyakazi na kumiliki na kurithi mali.
Ripoti kutoka Jukwaa la Kiuchumu Duniani iliorodhesha UAE ya pili kama nchi bora Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kuhusiana na masuala ya usawa wa jinsia.
Kwanza, ripoti kutoka Jukwaa la Kiuchumu Duniani iliorodhesha nchi za eneo chini kabisa yaani hakuna ambayo iliingia katika nchi 100 za kwanza.
UAE iliorodheshwa ya 120 duniani kati ya nchi 153.
Wanawake wana haki, chini ya sheria ya mtu kibinafsi mara nyingi mume au jamaa wa kiume ndio wanaotoa ruhusa kwa mwanamke ya kufanya jambo fulani.
Ingawa sheria za uangalizi UAE sio zenye masharti makali sana kama ilivyo kwa nchi jirani ya Saudi Arabia, zinaathiri wanawake.
Wakati mwingine, wanawake wanapokuwa na haki, kiutamaduni ni vigumu kutetea haki hizo kwa misingi ya sheria mahakamani.
Moja ya yalioathirika katika maisha binafsi ya wanawake ni ndoa: mwanamke anahitaji ruhusa ya mwanamume anayemtunza ili kuruhusiwa kufunga ndoa.
Maeneo mengine ni pamoja na haki ya kulea watoto na kurithi.
Lakini pia kuna uangalizi usio rasmi kisheria lakini huwa unatekelezwa kama utamaduni.
Hiba Zayadin, Mtafiti wa haki za binadamu eneo hilo amezungumza na BBC .
"Bila shaka kuna matukio ambayo huwa sio sheria lakini baadhi ya kesi utaona watu wanauliza mwanamke kama amepewa ruhusa na anayemtunza wakati maombi ya kutafuta kazi yanafuatiliwa au kama wanatafuta nyumba ya makazi," Bi. Zayadin anasema.
"Lakini hilo haliko kwenye sheria. Inakuwa sheria linapokuja suala la ndoa na talaka."
Pia talaka ni jambo jingine ambalo ni mtihani mkubwa kwa wanawake.
Wakati wanaume wanaweza kutalaki wake zao pale wanapotaka, wanawake wanaotaka kupewa talaka lazima watume maombi kupata agizo la mahakama.
Dhuluma za nyumbani ni eneo jingine ambapo wanawake wanaendelea kunyanyaswa.
Miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na mabadiliko yanayoleta mtazamo chanya. Kwa mfamo, sheria iliyokuwa inaruhusu wanaume kufanyia wake zao ghasia iliondolewa mwaka 2016.
Hitaji la Sheria ya Mtu Binafsi kwa wanawake inayowataka kuwa "watiifu" kwa waume zao iliondolewa mwaka 2019.
Machi mwaka jana, sheria mpya ilianza kutekelezwa iliyowaruhusu wanawake kulindwa, hii ikiwa ni mara ya kwanza.
Hata hivyo, wanaharakati wanasema sheria hizo zilizoaandikwa tena hazileti mabadiliko makubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa yeyote anayeishi au kutembelea UAE anatarajiwa kufuata sheria hizo: Kuna watalii wachache wa ngazi ya juu ambao waliwahi kujipata mashakani hasa wakiwa likizoni huko Dubai.
Mwaka 2017, kwamfano, mwanake mmoja raia wa Uingereza alikamatwa na kufungwa jela mwaka mmoja gerezani kwa kukubali kwa hiari kufanya mapenzi na mwanaume ambaye hakuwa mume wake.
Lakini swali ni je ikiwa sheria hizi zinatekelezwa kwa sawa kwa jinsia zote?
Pia kulingana na Shirika la Wafanyakazi Kimataifa (ILO), mwaka 2017 wafanyakazi wahamiaji ndio wanaolipwa kima cha chini zaidi UAE.
Wahamiaji wanawake hasa ndio walioathirika zaidi kwasababu wao mara nyingi ndio wanaofanya kazi za ndani na sera zao ni mbaya mno.

Chanzo cha picha, Getty Images
Akizungumza na BBC " Devin Kenney, mtafiti wa eneo hilo wa Shirika la kutetea haki za binadamu duniani Amnesty International, amezungumza na BBC News.
"Wahamiaji wafanyakazi wanawake ambao wamefika hospitalini na kubainika kwamba ni wajawazito, UAE, na kushindwa kusema baba wa mtoto ni nani, wamefunguliwa mashitaka mahakamani kulingana na nchi hiyo," Bwana Kenney amesema.
Wanawake wanaopata mimba nje ya ndoa wanakabiliwa na kifungo gerezani cha hadi mwaka mmoja - kwa wafanyakazi wahamiaji, hiki ni kifungo ambacho ni lazima wakihudumie kabla ya kuondoka nchini humo.
Kulingana na taarifa za UAE zilizonukuliwa na gazeti la Guardian mwaka jana, maelfu ya wahamiaji wanawake nchini humo wana watoto waliowazaa nje ya ndoa.
Waathirika wa kubakwa, pia nao wameshitakiwa chini ya sheria inayopinga mahusiano ya nje ya ndoa.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na BBC Arabic mwaka 2015, ulibaini kuwa mamia ya wanawake ikiwemo waathirika wa kubakwa, walikuwa wanafungwa gereza chini ya sheria hiyo kila mwaka na kuwa wafanyakazi wa nyumbani ndio waliokuwa katika hatari zaidi.














