Urusi yawatimua wanadiplomasia wa Muungano wa EU kwa kuunga mkono maandamano ya Navalny

Maandamano yalifanyika kila mahali nchini Urusi ili kumuunga mkono Alexei Navalny

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Maandamano yalifanyika kila mahali nchini Urusi ili kumuunga mkono Alexei Navalny

Urusi imewatimua wanadiplomasia kutoka Ujerumani, Sweden na Poland kwa kuhudhuria maandamano ya kumuunga mkono mkosoaji wa Putin Alexei Navalny.

Wizara ya masuala ya kigeni ilisema katika taarifa kwamba wanadiplomasia hao wa EU walihudhuria katika maandamano haramu , yaliofanywa kumuunga mkono Alexei Navalny .

Tangazo hilo lilijiri saa chache baada ya mkuu wa masuala ya kigeni katika Muungano wa Ulaya EU Josep Borrel kukutana na waziri wa masuala ya kigeni ya Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow.

Bwana Navalny ni mkosoaji mkubwa wa rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mwezi Agosti iliopita alipatiwa sumu mashariki mwa Urusi na kupelekwa Ujerumani ili kufanyiwa matibabu.

Alirudi nyumbani mwisho wa mwezi Januari , licha ya onyo kutoka kwa serikali ya Urusi kwamba atakamatwa.

Baadaye alifungwa kifungo cha miaka mitatu na nusu kwa kile ambacho waendesha mashtaka wanasema ni ukiukaji wa masharti ya hukumu uliositishwa ya ulaghai mwaka 2014.

Msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni nchini Sweden amekataa kwamba balozi wake alishiriki katika maandamano yoyote.

Mamia ya maelfu ya watu walishiriki katika maandamano hayo kumuunga mkono bwana Navalny kote Urusi mnamo tarehe 23 na 31 mwezi januari .

Maelfu ya walioshiriki walikamatwa.

Wizara ya masuala ya kigeni nchini Ujerumani ilipinga kufukuzwa kwa wanadiplomasia hao ukisema kuwa hakuna thibitisho , na kuonya kulipiza kisasi iwapo Urusi haitabadili msimamo wake.

Je Alexei Navalny ni nani?

Bwana Navalny, mwenye umri wa miaka 44, ni mwanaharakati wa kisiasa ambaye amekuwa akifanya kampeni dhidi ya ufisadi na rais Putin tangu 2011.

Bwana Navalny anamshutumu rais Putin kwa kuendesha serikjali ilioja ufisadi.

Muda mfupi baada ya kurudi nchini Urusi , alitoa kanda ya video katika mtandao wa Youtube akionesha jumba moja la kifahari alilodai kuwa zawadi iliotolewa na bilionea mmoja wa Urusi kwa rais Putin.

Zaidi ya watu milioni 100 wametazama kanda hiyo ya video. Bwana Putin amekana kumiliki jumba hilo.

Wiki iliopita Arkady Rotenberg, bilionea na mfanyabiashara wa karibu wa bwana Putin alijitokeza na kusema kwamba alilinunua kasri hilo miaka miwili iliopita.