Gavana wa Sonko wa Nairobi aondolewa madarakani

Chanzo cha picha, MIKE SONKO/TWITTER
Bunge la Seneti nchini Kenya limepiga kura kumuondoa Mike Mubuvi Sonko kama gavana wa Nairobi , katika hatua ambayo imekomesha miaka mitatu ya utawala wake uligubikwa na utata.
Bw. Sonko anatuhumiwa kwa ukiukaji wa katiba, utumizi mbaya wa mamlakaa, utovu wa nidhamu, na uhalifu chini ya sheria.
Maseneta 27 walipiga kura kuunga mkono kuondolewa ofisini kwa Bw Sonko kwa kudumisha mashtaka yote manne yaliyowasilishwa na Bunge la Kaunti ya Nairobi, ambalo lilipiga kura ya kutokuwa na imani naye mnamo Desemba 3.
Kuondolewa madarakani kwa Bw. Sonko kumetoa nafasi kwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Ben Mutura kushikilia wadhifa huo hadi uchaguzi wa gavana na naibu wake utakapofanywa katika kipindi cha siku 60 zijazo.
Sonko ni nani?
Gavana aliyeondolewa sio mgeni katika masuala yenye utata. Maafisa wa magereza nchini Kenya hivi karibuni walimshtaki kwa kutoroka kutoka jela miaka 20 iliyopita. Bwana Sonko amekiri hadharani kutoroka jela wakati wa mahojiano ya moja kwa moja ya runinga.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati mmoja alijumuisha chuma za pombe aina ya Hennessy kama sehemu ya kifurushi cha kujitakasa cha Covid 19 sanitation kilichosambaziwa wakazi wa Nairobi akidai " kiwango cha pombe katika kinywaji hicho kinaweza kuzuia virusi vya corona'
Mnamo Desemba iliyopita, alikamatwa kwa tuhuma za ufisadi.
Bw. Sonko alichaguliwa kuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi mwaka 2017, kupitia chama cha Jubilee cha Rais Uhuru
Lakini wawili hao wametofautiana kufikia hatua ya Rais Kenyatta kushinikiza mageuzi yaliyochangia majukumu makuu ya Kaunti ya Nairobi kuhamishiwa serukalai ya kitaifa.
Rais Kenyatta pia alimteua jenerali wa kijeshi kuendesha shughuli za kaunti, hali iliyomfanya Bw. Sonko kuwa gavana 'asiye na mamlaka'
Sonko, ambaye alishiriki hafla ya kukabidhi serikali kuu baadhi ya majukumu ya kaunti kwa serikali baadaye alidai kwamba alikuwa mlevi aliposaini nyaraka za kuidhinisha hatua hiyo.
Safari yake ya siasa
Sonko alijipatia umaarufu kutokana na mtindo wake usio wa kawaida alipokuwa mbunge wa eneo la Makadara, Nairobi.
Anafahamika kwa kuvalia vito, mikufu na bangili za thamani.
Alipokuwa mbunge, alikuwa akiandamana 'kutetea wanyonge' na wachuuzi walipokuwa wanafurushwa kutoka maeneo yao ya kazi na serikali ya jiji.

Chanzo cha picha, MIKE SONKO/TWITTER
Atakumbukwa pia kwa kuongoza waandamanaji Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) The Hague, Uholanzi kulalamikia kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo baadaye ilisitishwa.
Alipokuwa Seneta, alianzisha kundi kwa jina Sonko Rescue Team ambalo lilikuwa likitoa huduma kama vile maji, matibabu na misaada wakati wa mazishi.
Wakati mmoja alipoitwa kusaidia familia zilizokuwa zimeathiriwa na bomoa bomoa jijini mwaka 2014, alimpigia simu Rais Kenyatta na kumuweka kwenye kipaza sauti. Rais alitoa agizo ubomoaji usitishwe.
Alipoingia uongozini kama gavana wa Nairobi, ameonekana kuchukua hatua ambazo zinaenda kinyume na aliyokuwa akitetea.

Mambo Muhimu kuhusu Mike Sonko
- Alizaliwa Februari 1975
- Alikuwa mbunge wa Makadara 2010-2013
- Alichaguliwa seneta wa Nairobi Machi 2013
- Alichaguliwa kuwa gavana wa Nairobi Agosti 2017
- Serikali ilitangaza kupunguza walinzi wake hadi watano 16 Mei, 2018












