Siasa za Tazania: Je, CCM wana uwezo gani wa kuhimili migogoro?

Chanzo cha picha, Chama Cha Mapinduzi
- Author, Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Fukuto la mgogoro wa ndani limekikumba chama tawala CCM nchini Tanzania ikiwa imebaki miezi nane kabla ya Uchaguzi Mkuu wa urais,wabunge na madiwani.
Hali ambayo imetafsiriwa na wachanganuzi wa siasa kuwa ishara ya kudidimia uhuru wa maoni, taswira ya chama machoni pa wanachama na wapigakura, na demokrasia nje na ndani na chama chenyewe pamoja na kudhibitiwa kwa siasa za maslahi binafsi kuwa miongoni mwa vyanzo vinavyokisumbua chama hicho.
Inaelezwa kuwa mgogoro uliotamalaki sasa unachochewa na hali ya uongozi wa chama hicho na serikali kukataza mikutano ya hadhara ambayo ilitumika kama nyenzo ya wanasiasa wa chama chawala na wapinzani kwa kile kinachoitwa 'kupumua'.
Pia kubanwa kila kona kwa taasisi za kisiasa kushindwa kushiriki kwa uhuru siasa za majukwaani dhidi ya washindani wao, badala yake CCM wamejikuta wakiwa wao wenyewe hivyo kuanza kuzua tafrani za ndani.
Aidha, migogoro mingi ya CCM ni kama utamaduni kila unapowadia uchaguzi mkuu, ambapo huibuka na kusababisha makundi yanayosigana, na kuchochea baadhi ya wanasiasa kujiuzulu na kujiunga vyama vya upinzani au kuanzisha vyama vyao au kuhamia vyama vingine kama ilivyotokea kwa Augustine Lyatonga Mrema na Edward Lowassa kwa nyakati tofauti.
Mgogoro wa sasa unawahusisha makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho, Kanali Abdulrahman Kinana na Luteni Yusuf Makamba, pamoja na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mtama, waziri wa mambo ya nje katika serikali ya awamu ya nne na mtia nia ya urais wa CCM mwaka 2015, Bernard Membe.
Makada hao waliitwa kuhojiwa mbele ya Kamati ndogo ya Maadili ya chama hicho kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwemo madai ya kumhujumu mwenyekiti wao na rais John Magufuli ikiwemo kupanga mikakati ya kupinga uteuzi wa kiongozi huyo anayemaliza muda wake ndani ya chama tawala katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Chanzo cha picha, Chama Cha Mapinduzi
Kutakiwa kuhojiwa kwa Makamba na Kinana ambao kwa nyakati tofauti wamekitumikia kama watendaji wakuu, walilalamika hadharani juu ya hatua ya mwanaharakati mmoja kuwachafua viongozi wastaafu pamoja na kuwatuhumu kuhusika katika njama mbalimbali pasipo kuweka wazi ushahidi.
Aidha, viongozi hao wastaafu sauti zao za mazungumzo ya simu zilivuja na kusambazwa katika mitandao ya kijamii, walisikika wakisema wanashangazwa na namna CCM kinavyopoteza dira yake, ikiwa ni kauli inayofanana na iliyowahi kutolewa na aliyewahi Katibu mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba ambaye wakati wa uhai wake alitamka hadharani namna chama kilivyopoteza dira ya uongozi nchini humo.
Awali, Kinana na Makamba walipaswa kuitika wito wa kuhojiwa mnamo Februari 7 mwaka huu makao Makuu Dodoma, badala yake walihojiwa Februari 10 mwaka huu jijini Dar es salaam ikiwa ni siku tatu baada ya kuhojiwa Membe.
Duru za kisiasa zinasema kuwa makatibu hao waligoma kwenda kuhojiwa na Kamati hiyo mjini Dodoma kama ilivyokuwa kwa Membe. Yameibuka makundi mawili yanayopingana kuwa ni sahihi viongozi hao wastaafu kuhojiwa, huku wengine wakidai hawastahili kwa sababu uhuru wa maoni unalindwa na katiba Ibara ya 18.
Wanasiasa wengine waliotuhumiwa kumhujumu Rais Magufuli ni William Ngeleja, Nape Nnauye ambao sauti zao nazo zilimsema vibaya mwenyekiti wao waliomba radhi na kusamehewa.
Katika hatua nyingine mgogoro wa sasa umechangia kuondolewa kwa January Makamba aliyekuwa waziri wa nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira katika nafasi yake, licha ya Rais Magufuli kueleza alimwondoa waziri huyo kutokana na kuchelewesha mpango wa kukataza matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na kubainika ubadhirifu katika wizara hiyo.
January aliondolewa siku chache baada ya barua kali iliyoandikwa na baba yake Yusuf Makamba akishirikiana na Kinana iliyoeleza kushangazwa na viongozi wa chama na serikali kumtomshughulikia mwanaharakati anayetajwa kuwachafua viongozi wastaafu.
Kusambaratishwa timu ya kampeni 2015
Vilevile mgogoro wa sasa unaotimua vumbi ndani ya CCM umejikita katika makundi mawili; kundi la kwanza ni lile ambalo lilipambana na kupigania utawala mpya ulioingia Novemba mwaka 2015. Kundi hili ndilo linawahusisha Abdurahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe na wafuasi wao.
Kundi la pili ni lile la uongozi mpya ambalo sasa lipo chini ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali na uongozi mpya wa CCM. Ni Dk.Bashiru Ali aliyepata kutamka hadharani kumtuhumu Bernard Membe kuwa anasuka mipango ya chini chini kuomba ridhaa ya kugombea urais ndani ya CCM ifikapo mwaka 2020.
Duru za kisiasa zinaonesha kubadili timu ya kampeni kisiasa ni jambo la kawaida, lakini namna inavyobadilishwa na kilichowatokea wanatimu hiyo ndani ya CCM ya sasa ndicho kinachozua minong'ono.

Chanzo cha picha, IKULU, TANZANIA
Aidha, zinasema kuwa timu ya kampeni iliyoundwa wakati wa uchaguzi mwaka 2015 kutafuta kura za mgombea wa CCM, imesambaratishwa na ambapo sasa makada wanakabiliwa na tuhuma za kukosa maadili hivyo kuitwa kujieleza.
Muktadha wa timu hiyo kusambaratishwa ndio haswa unachochea mgogoro wa chini chini, ambao unaungana na wa sasa unaowahusisha watu walewale. Kinana, Yusuf Makamba, January Makamba, Bernard Membe, Nape Nnauye.
Duru zinasema namna timu hiyo ilivyokoma ni ajabu kwani asilimia kubwa makada wote wametuhumiwa kwa mambo mbalimbali.
Migogoro sugu ndani ya CCM
CCM kimeshuhudia mitafaruku ya wanasiasa wazito kama Oscar Kambona (aliyegombana na mwenyekiti na rais wake Julius Nyerere), Zuberi Mtemvu (aliyejitoa TANU/CCM na kuunda chama chake), na wengine walioingia migogoro na chama hicho ni Bibi Titi Mohammed, Kassela Bantu,Horace Kolimba, na Augustine Mrema (aliyeamua kukihama na kujiunga NCCR-Mageuzi), ambayo kwa namna moja au nyingine imewahi kukitikisa chama hicho.
Edward Lowassa ndiye mwanasiasa ambaye ameonekana kukitikisa vilivyo chama hicho kiasi kwamba kililazimika kutumia nguvu nyingi kupata ushindi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Lowassa alikihama CCM baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali kuelekea kupata jina la mgombea wa chama hicho ambayo ilizua mgogoro ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.
Wajumbe wawili Dk. Emmanuel Nchimbi na Sophia Simba wakisusia kikao cha kumchagua mgombea wa urais ndani ya CCM. Inafahamika kuwa makada hawa wawili walikuwa kambi ya waziri mkuu huyo wa zamani, Edwaard Lowassa iliyokuwa na nguvu kubwa.
Mzozo wa kukatwa mgombea wao ulisababisha wasusie mchakato mzima, na kuzua mgogoro kuhusiana na mustakabali wa CCM.
Kutokana na Lowassa kukatwa alihamia Chadema ambako makada na wenyeviti mbalimbali wa mikoa wa CCM waliungana naye kwenda upinzani.
Ushahidi wa Lowassa kukitikisa CCM ni idadi ya kura alizopata kwenye uchaguzi, kwa mujibu wa matokeo ya Tume yanaonesha alipata takribani kura milioni 6, ikiwa ni rekodi ya kipekee ya mgombea wa upinzani.
Majeruhi ya mgogoro huo yalisababisha mwenyekiti mpya wa CCM, John Magufuli kuwaadhibu na kuwafukuza uanachama baadhi ya wanasiasa akiwemo Sophia Simba kutokana na tafrani za uchaguzi mwaka 2015.
Kivumbi cha kuvuana gamba
Mwaka 2012 chini ya mwenyekiti Jakaya Kikwete, CCM kilitangaza operesheni ya kujivua gamba nchi nzima, ambapo wanasiasa mbalimbali wa chama hicho walitakiwa kujitafakari kabla ya kuchukuliwa hatua.
Hoja kubwa iliyotajwa wakati huo ilikuwa ufisadi uliotamalaki ndani ya chama na kukichafua taswira mbele yake mbele ya wanachama na wapigakura wa Tanzania. Wanasiasa waliolengwa katika mkatati huo walikuwa Edward Lowassa, aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Frank Banka, mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini Tanzania, amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, mgogoro wa CCM kwa sasa na wa zamani una tofauti kuu mbili. Kwanza mgogoro wa zamani ulikuwa wa kulinda maslahi binafsi. Pili, mgogoro wa sasa ni maslahi binafsi yameguswa kama sio kuharibiwa.
"Wakati wa kuvuana magamba walikuwa na kila mmoja ana uhakika wa kula. Chini ya uenyekti wa rais mstaafu Jakaya Kikwete kila kada CCM aliweza kumtunishia kifua mwenyekiti. Kikwete hakuwa akiadhibu na mkakati wa kuvua gamba ulileta matokeo hasi vilevile na walengwa hawakuondoka, isipokuwa Mbunge wa Igunga mkoani Tabora, Rostam Aziz.
"Tathmini inaonyesha zama zimebadilika, CCM ya Magufuli inajaribu kuwadhibiti wote ndani ya chama na nje. Udhibiti huwa na matokeo hasi na chanya. Upande hasi unatengeneza makundi ya waliojeruhiwa hata kama ni halali yao, ndio maana unaona Membe amejipatia wafuasi pande zote mbili; upinzani na chama tawala. Kuondoka hapo walipo ni kuweka silaha zote chini na kurekebisha kiungwana. Kinyume chake ni migogoro mingine,"
Je, CCM wana uwezo gani wa kuhimili migogoro?
Mtaalamu wa Falsafa na mchambuzi wa siasa na utawala bora, Paul Nduru anasema, "Naweza kusema kwa sasa kuna fukuto la ndani kwa ndani, makundi kama awali,, na huenda yameongezeka. Baadhi ya wanasiasa sio wawazi, wanaishi ndani ya ngozi ya kondoo. Wengi wanahofia kuzungumza hadharani changamoto au kukikosa chama kwa kuzingatia wakati tuliopo, utawala kutopenda kukosolewa. Uwanja wa kusemea haupo, tofauti na zama za katikati kwa tawala tatu zilizopita. Ingawaje naiona kama hatari, ni sawa na bomu linalofuka moshinndani ya nyumba ikichelewa kuteguliwa linaweza kulipuka mbeleni.
Alipoulizwa kuhusu uimara wa CCM katika migogoro, alisema, "natambua kuwa CCM wana uwezo mkubwa sana kuhimili mikikimikiki ya aina hiyo na hata kuimaliza kimya kimya bila kuleta athari kubwa sana wakisaidiwa na mifumo yake, tofauti na vyama vingine vya upinzani ambavyo kwao migogoro midogo midogo tu huathiri sana mustakabali wao."
*Makala haya ni mawazo binafsi ya mchambuzi na si msimamo wa BBC.












