Kwa nini wahadhiri wanaotuhumiwa kwa rushwa ya ngono kufika mbele ya kamati maaalum Ghana

Ransford Gyampo NA Dr Paul Kwame Butakor
Maelezo ya picha, Profesa Ransford Gyampo na Dr Paul Kwame Butakor walinaswa na kamera ya siri ya waandishi wapekuzi wa BBC

Wahadhiri wawili wa Ghana walioangaziwa katika makala ya BBC Africa Eye kwa kuhusika na rushwa ya ngono wanatarajiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Chuo Kikuu cha Ghana.

Hii ni baada ya uchunguzi wa ndani kubaini kuwa walikiuka kanuni ya kimaadili ya chuo hicho.

Profesa Ransford Gyampo na Dkt. Butakor walisimamishwa kazi mwezi Oktoba kusubiri uchunguzi kamili.

Uchunguzi wa awali kuhusu sakata hiyo ulifanywa chini ya uwenyekiti wa jaji mstaafu wa mahakama ya juu zaidi, Vida Akoto-Bamfo.

Wahadhiri hao wawili walifika mbele ya kamati hiyo mwezi Oktoba baada ya kuonekana katika kanda ya video ilionaswa kupitia kamera za siri zilizotumiwa na waandishi waliojidai kuwa wanafunzi katika chuo hicho.

Wahadhiri wote wawili wamepinga kuhusika na madai hayo.

Maelezo ya video, BBC Africa Eye: Unyanyasaji wa kingono wa wanafunzi katika Chuo kikuu cha Lagos na Ghana.

Kitu gani kingine kilioneshwa katika Makala ya BBC Africa Eye?

Makala hii ya urefu wa saa moja pia iliwaonesha wahadhiri wawili kutoka chuo kikuu cha Ghana wakihusika na vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa wanafunzi.

Wote wawili Profesa Ransford Gyampo na Dr Paul Kwame Butakor wamekanusha kuhusika na kuomba rushwa kwa kutoa alama za darasani.

Profesa Gyampo ameambia vyombo vya ndani vya habari kuwa ana mpango wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya BBC.

Chuo kikuu cha Ghana kimetoa taarifa kuwa kitafanya uchunguzi kwa wahadhiri hao na kusisitiza kuwa hawahusiki na kumtetea mhadhiri yoyote ambae ameshukiwa kujihusisha na rushwa ya ngono chuoni.

Swala la unyanyasaji wa kingono
Maelezo ya picha, Swala la unyanyasaji wa kingono

Swala la unyanyasaji wa kingono ni kubwa kiasi gani

Unyanyasaji wa kingono ni tatizo kubwa la kiafya na hata la kibinadamu linalomuathiri mtu kwa muda mrefu au mfupi hayo ni kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) .

Kulingana na utafiti uliofanywa nchini Kenya na Shirika la ActionAid pamoja na viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini Kenya asilimia 49 ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu hunyanyaswa kijinsia huku asilimia 24 ya wanafunzi wa kiume pia wakinyanyaswa na wafanyikazi katika vyuo hivyo.