"Nimetishiwa kuuawa" Jacob Zuma alifahamisha jopo linalomchunguza

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kuwa mtu asiyejulikana alimpigia simu na kumtishia kifo yeye na watoto wake siku moja baada ya jopo maalum lilobuniwa kuchunguza kashfa ya rushwa dhidi yake.
Bwana Zuma amelifahamisha jopo hilo kuwa, msaidizi wake binafsi aliyepokea simu hiyo usiku wa Jumatatu aliambiwa: ''Mwambie Zuma tutamuua yeye na watoto wake na watu wote waliokaribu nae.''
Jaji Ray Zondo ambaye anaongoza jopo hilo amesema vitisho na vurugu "havikubaliwi kabisa", na kuongeza kuwa shahidi aliyepokea simu hiyo lazima apatiwe ulinzi wa kutosha.
Jaji Zondo aidha ametilia shaka ikiwa kuna kiwango cha kutosha cha ulinzi kumhakikishia usalama rais huyo wa zamani: "Kile ambacho sifahamu ni kama una ulinzi wa kutosha kuliko ule ulionao hivi sasa. Sijui kama unaweza kupata ulinzi zaidi ya hapo."
Jopo hilo linachunguza madai kuwa Bw. Zuma aliongoza mtandao wa ufisadi wakati alipokuwa rais wa Afrika Kusini.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY
Mashitaka dhidi ya Zuma yanaangazia uhusiano wake na familia yenye utata ya Gupta, ambayo inatuhumiwa kwa kutumia vibaya uhusiano wao na Zuma kuingilia uteuzi wa mawaziri na kujipatia kandarasi za serikali kwa njia za kifisadi.
Pia anakabiliwa na tuhuma ya kupokea rushwa kutoka kwa kampuni ya Bosasa, ambayo inamilikiwa na familia ya Watson.
Bw. Zuma amekanusha madai hayo yote.
Hapo jana alilifahamisha jopo hilo kuwa ameonewa na kutuhumiwa kuwa mfalme wa watu wafisadi.
"Watu wamenibandika majina ya kila aina na sijawahi kujibizana nao kuhusu na suala hilo," aliongeza. Zuma alisema.
Zuma kuhusiana na 'hujuma' dhidi yake
Alielezea kwa kina- na kwa hasira - kile alichotaja kwa miongo kadhaa ya hujuma dhidi yake.
Alidai kuwa mataifa ya Uingereza na Marekani - bado ni washirika wa - sehemu ya mpango wa kumkosoa japo amejaribu kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini Afrika Kusini.

Zuma na familia ya Gupta
Alisema aliona familia hiyo ya wazaliwa wa kihindi walikuwa ''marafiki zake''.
"Sikufanya jambo lolote kinyume cha sheria nao. Walikuwa marafiki zangu tu, sawa na jinsi walivyokuwa marafiki wa watu wengine," Bw. Zuma alisema.
Aliongeza kuwa familia hiyo ilikuwa na uhusiano wa karibu na rais wa kwanza wa nchi hiyo Nelson Mandela na Thabo Mbeki.
Alipinga madai kuwa aliiruhusu familia hiyo kuingilia kati uongozi kwa "kuteka nchi" na kuipiga mnada.
"Nilipiga mnada Table Mountain? Je nilipiga mnada jiji la Johannesburg?"alisema.














