Matumaini yameibuka kwa wanawake wanaotatizwa na ovari baada ya wanasayansi kutengeneza ovari bandia

Mpango wa upandikizaji wa ovari ni kwa ajili ya wanawake kutopata ugumba baada ya matibabu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mpango wa upandikizaji wa ovari ni kwa ajili ya wanawake kutopata ugumba baada ya matibabu

Wanasayansi wamechukua hatua za mwanzo kuelekea kutengeneza Ovari bandia hatua ambayo itasaidia kuboresha matibabu na kuondoa changamoto za masuala ya uzazi.

Mpango huu ni kwa ajiliya kuwasaidia wanawake walio kwenye hatari ya kuwa wagumba na wale wanaofanyiwa tibakemikali(Chemotherapy)

Wanasayansi wa Denmark waliondoa sehemu za ovari na kuzibadilisha ili ziweze kupandikizwa baadaye wakati mwanamke anapotaka kushika ujauzito.

Matibabu ya saratani, kama tibakemikali na matibabu kwa njia ya Xray, yanaweza kuharibu Ovari na kumfanya mwanamke awe mgumba.

Njia moja ambayo wanawake wanaweza kulinda wasipate shida hiyo ni njia ya upandikizaji wa tishu za ovari,ambapo ovari yote au sehemu ya ovari inaondolewa na kugandishwa kabla haijaharibiwa ili iweze kutumika baadae.

Lakini kuna hatari kidogo kwa wale wenye saratani kuwa tishu za ovari zinaweza kuwa na seli za saratani, hali inayoleta uwezekano wa maradhi kurejea baada ya zoezi la upandikizaji kufanyika.

Ingawa uwekano wa kutokea hatari hii ni ''mdogo sana'', inamaanisha wanawake wenye aina fulani ya saratani, kama vile saratani ya damu na saratani nyingine zinazojitokeza tumboni hawawezi kupandikizwa.

Wanawake watakaofanyiwa upandikizaji wataweza kushika mimba

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanawake watakaofanyiwa upandikizaji wataweza kushika mimba

Mtaalamu wa afya ya uzazi, Stuart Lavery amesema upandikizaji wa tishu za ovari huwa una maelfu ya mayai ambayo yanawaweza kumsaidia mwanamke kupata ujauzito kwa njia ya asili tofauti na njia ya upandikizaji baada ya yai kurutubishwa kwenye maabara na kurejeshwa tumboni (IVF)

Faida nyingine ya kufanyika upandikizaji huu ni kuwa wanawake wanaweza kuanza kupata hedhi baada ya matibabu na kuzuia uhitaji wa kupandikiza homoni.

Matibabu haya yanapaswa kufanyiwa majaribio kwa binaadamu kwanza, zoezi litakaloanza miaka mitatu au minne ijayo.