Uchaguzi Kenya: Upinzani wasema mkutano na IEBC haujazaa matunda

Chanzo cha picha, AFP/Getty
Muungano wa upinzani Kenya National Super Alliance (Nasa) umesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) imekataa kutekeleza mageuzi ambayo umekuwa ukitaka yafanywe kabla ya uchaguzi mpya wa urais kufanyika baadaye mwezi huu.
Viongozi wakuu wa Nasa, wakiwemo mgombea urais Raila Odinga na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka, walikutana na viongozi wa IEBC akiwemo mwenyekiti Wafula Chebukati katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.
Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo, Seneta wa jimbo la Siaya James Orengo amesema hakukuwa na maafikiano yoyote kuhusu matakwa yaliyotolewa na Nasa.
Bw Orengo amesema muungano huo utaendelea kuandaa maandamano kila Jumatatu na Ijumaa hadi mabadiliko hayo yatekelezwe.
Miongoni mwa mengine, Nasa wanataka afisa mkuu mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba na wakuu wengine kadha katika tume hiyo waondolewe kazini.
Nasa pia wanataka kampuni ya OT-Morpho ambayo iliunda mfumo wa teknolojia uliotumiwa wakati wa uchaguzi ipokonywe kandarasi hiyo sawa na kampuni ya Al-Ghurair iliyochapisha karatasi za kupigia kura.
Mwezi uliopita mahakama ya juu zaidi ilibatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti kutokana na inachokitaja kuwa ni hitilafu na makosa yalioshuhudiwa wakati wa zoezi hilo. Viongozi wa muungano wa upinzani NASA na wa chama tawala Jubilee, leo wamekutana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini IEBC Wafula Chebukati katika kujaribu kutatua masuala kadhaa kabla ya uchaguzi huo wa marudio Oktoba 26.

Tume ya IEBC ilitisha mkutano na wagombea hao wakuu wa urais kabla ya uchaguzi wa tarehe 26 mwezi huu, kujadiliana kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, baada ya mkutano uliohusisha wawakilishi wa wagombea hao kutozaa matunda.
Mkutano huo umefanyika siku moja baada kufanya mazungumzo na wajumbe 12 kutoka nchi za kigeni wakiongzowa na balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec na naibu balozi wa Uingereza nchini Kenya, Susie Kitchens, ambao waliwataka wanasiasa kuheshimu uhuru wa tume ya uchaguzi.
Bw Orengo hata hivyo amewashutumu mabalozi hao na kusema kuwa upinzani una haki ya kueleza hisia zao kuhusu maandalizi ya uchaguzi.
Rais Uhuru Kenyatta aliwakilishwa na Naibu William Ruto ambaye baadaye alisema mazungumzo yake na maafisa wa IEBC yalikuwa ya kufana.
"Chama cha Jubilee hakijatoa masharti yoyote kwa tume ya uchaguzi na tuko tayari kwa uchaguzi," aliambia wanahabari.
Aidha, alisema wameishauri IEBC kuchangia katika majadiliano yanayoendelea kuhusu marekebisho ya sheria za uchaguzi kupitia Bunge.

Mabalozi wa nchi za Magharibi walikuwa wameshutumu juhudi za chama hicho tawala za kutaka kurekebisha sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi wa marudio kufanyika.
Jubilee imesema mabadiliko hayo yanahitajika kuziba mianya ambayo wanasema ilichangia uamuzi wa Mahakama ya Juu wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi Agosti, uamuzi ambao umeshutumiwa na chama hicho cha Rais Kenyatta.
IEBC imeahidi kuweka wazi maafikiano yaliyotokana na mikutano ya leo na wagombea.
"Tume ilikuwa na mazungumzo ya kufana na Nasa na Jubilee. Tutachapisha mammbo tuliyokubaliana hivi karibuni," tume hiyo imeandika kwenye Twitter.
"Tunatekeleza kwa makini mapendekezo ya Mahakama ya Juu. Hili litadhihirika wazi katika mambo ambayo tutaendelea kuwapasha."
Tume hiyo imeahidi kuweka wazi mkataba wake na kampuni ya OT-Morpho.












