Kim Jong-nam: Korea Kaskazini yawaachilia raia wa Malaysia

Chanzo cha picha, European Photopress Agency
Raia tisa wa Malaysia waliokuwa wamezuiliwa Korea Kaskazini wamewasili nyumbani, baada ya mataifa hayo mawili kuafikiana na kumaliza mzozo wa kidiplomasia.
Mzozo ulizuka baina ya mataifa hayo mawili mwezi uliopita kutokana na kuuawa kwa Kim Jong-nam, ndiguye wa kambo wa Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong-un katika uwanja wa ndege mjini Kuala Lumpur.
Mataifa hayo yaliwazuia raia wa nchi pinzani kuondoka.
Malaysia pia imekubali kuachilia mwili wa Kim.
Kumekuwa na uvumi kwamba Pyongyang ilihusika katika mauaji ya Bw Kim.
Mwana huyo wa kwanza wa kiume wa Kim Jong-il anadaiwa kutoroka Korea Kaskazini baada ya kukosa kupatiwa uongozi wa taifa hilo kufuatia kifo cha babake.
Raia wa Malaysia walioruhusiwa kuondoka Korea Kaskazini walilakiwa na jamaa na wanahabari katika uwanja wa ndege wa 'Kuala Lumpur mapema Ijumaa.

Chanzo cha picha, European Photopress Agency
Miongoni mwa waliolerejea ni mwanabalozi wa Malaysia aliyekuwa akihudumu Korea Kaskazini Mohd Nor Azrin Md Zain, maafisa wa ubalozi na jamaa zao.
Mwanabalozi huyo alisema waliingiwa na wasiwasi sana serikali ya Korea Kaskazini ilipowaambia kwamba hawawezi kurejea nyumbani.
Walisafirishwa kwa ndege ya kibiashara iliyoendeshwa na maafisa wa jeshi la wanahewa la Malaysia.
Bw Kim aliuawa 13 Februari katika uwanja wa ndege Kuala Lumpur. Korea Kaskazini iliitaka Malaysia kuachilia mwili wake lakini ombi hilo likakataliwa.

Chanzo cha picha, AP
Taarifa zinasema raia wote wa Korea Kaskazini nao wataruhusiwa kuondoka Malaysia, ikiwa ni pamoja na washukiwa wawili raia wa Korea Kaskazini waliokuwa wanasakwa na polisi wa Malaysia.
Shirika la habari la Japan Kyodo limesema watu wawili waliofanana na washukiwa wawili wanaotafutwa, walionekana kwenye ndege ya kuelekea Beijing ambayo ilikuwa imeubeba mweili wa Bw Kim Ijumaa.
Washukiwa hao wawili ni Hyon Kwang Song, katibu wa pili wa ubalozi wa Korea Kaskazini mjini Kuala Lumpur, na Kim Uk Il, mfanyakazi wa shirika la ndege la Korea Kaskazini Air Koryo.

Chanzo cha picha, Kyodo/Reuters
Wawili hao walikuwa wamekatalia ndani ya ubalozi na walikataa kushiriki katika uchunguzi wa mauaji hayo.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
O












